Thursday, February 17, 2011

Watu kadhaa wauawa kwenye mlipuko wa ghala la silaha Dar

Hali ya taharuki imetanda mji wa Dar Es Salaam, huku wakaazi wakiamka kuomboleza vifo vya zaidi ya watu kumi na zaidi ya wengine 60 kujeruhiwa kufuatia milipuko iliyotokea kwenye ghala la kuhifadhi silaha za kijeshi, lililo karibu na uwanja wa kimataifa wa ndege.
Wakaazi wa eneo la Gongo la Mboto lililo karibu na ghala hilo wamekesha nje baada ya makaazi yao kubomoka kutokana na mtikisiko wa milipuko hiyo iliyodumu kwa saa kadhaa. Milipuko hiyo ilisikika kwa umbali wa zaidi ya kilomita ishirini kutoka kituo hicho cha kijeshi.
Kwa mujibu wa Neema Mwaipopo aliyeshuhudia taharuki hiyo ameuambia mtandao huu kuwa milipuko hiyo ilianza mwendo wa saa mbili usiku ambapo wakazi wa maeneo ya jirani walilazimika kukimbia pasina kufahamu wapi waelekeapo na nini kilichotokea. Aidha, ameshuhudia mparaganyiko baina ya familia kupotezana na watoto wao wadogo.
Kamanda wa polisi jijini Dar-es-Salaam, Suleiman Kova, ametoa wito kwa raia wa mji kuwa watulivu huku maafisa wa ulinzi wakiendelea na mikakati ya kurejesha hali ya uthabiti.
Kova amesema uchunguzi wa awali umebainisha kuwa mlipuko huo ni ajali na wala sio shambulio la kigaidi.
Hii ni mara ya pili kwa milipuko kama hiyo kutoka jijini Dar es Saalam katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.
mwaka wa 2009 zaidi ya watu ishirini waliuawa na wengine 300 kujerihiwa
kwa msaada wa bbcswahili.com

No comments:

Post a Comment