Sunday, November 18, 2012

JESHI LA POLISI LAFANYA KAZI NZURI IRINGA


Serikali imelipongeza jeshi la polisi mkoani hapa kwa kazi nzuri linayofanya katika kuhakikisha ulinzi wa wananchi na mali zao unalindwa na wananchi wanaendelea kuishi na kufanya kazi kwa amani na utulivu.
Waziri wa Nchi, OWM- Sera, Uratibu na Bunge William Lukuvi (katikati) akimjulia hali Padri Angelo Burgeo hatika hospitali ya mkoa wa Iringa

Pongezi hizo zimetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu mwenye dhamana ya Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvu alipokuwa akiongea na waandishi wa habari katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Iringa alipofanya ziara ya kiserikali pamoja na mambo mengine kuwajulia hali na kuwapa pole mapadri Angelo Burgio (60) kutoka Italia na msaidizi wake Herman Myala wa kanisa katoliki, parokia ya Isimani, jimbo la Iringa waliojeruhiwa vibaya na watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi.

Lukuvi amesema “napenda kulipongeza jeshi la polisi chini ya kamanda wa mkoa wa Iringa, Michael Kamhanda kwa jitihada zao za kuhakikisha kuwa wananchi wanakuwa katika hali ya usalama wao na mali zao”. Aidha, amezipongeza jitihada za jeshi hilo za kuhakikisha watuhumiwa wa uhalifu uliofanyika katika parokia ya Isimani wanakamatwa na kufikishwa katika mkondo wa sheria. Amesema kuwa ndani ya siku mbili jeshi hilo limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa wanane jambo linalodhihirisha utendaji makini wa jeshi hilo.

Kutokana na kazi hiyo nzuri, Waziri huyo amevitaka vyombo vya habari mkoani hapa kuhakikisha vinatangaza utendaji na ufanisi wa jeshi hilo ili wananchi waweze kufahamu utendaji huo na kuondokana na hofu inayoweza kujitokeza na kuendelea na utendaji kazi wao wa kila siku. Amewahakikishia wananchi kuwa serikali yao ipo makini kuhakikisha usalama wao.

Amesema kuwa ipo dhana iliyojengeka ndani ya jamii hasa wanapowaona wazungu wanadhani kuwa ni watu wenye fedha nyingi hivyo kushawishika kufanya uhalifu.

Wakati huohuo, Waziri Lukuvi amesema kuwa tukio hilo la ujambazi wa kutumia silaha ni uhalifu wa kawaida kama unavyofanyika uhalifu mwingine wa aina hiyo nchini hivyo usihusishwe na hisia nyinyine kwa namna yoyote ile.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Kamishna Mwandamizi Msaidizi Michael Kamhanda, amesema kuwa wananchi wa Isimani wametoa ushirikiano mkubwa kwa jeshi hilo katika tukio hilo na kuhakikisha watuhumiwa wa uhalifu huo wanakamatwa mapema na kufikishwa katika mikono ya sheria. Amesema kuwa watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani hivi karibuni baada ya upelelezi kukamilika. Amesema kuwa jeshi la polisi limeanzisha program maalumu kwa mkoa mzima ya kuwaelimisha wananchi na taasisi juu ya ulinzi shirikishi na mbinu za kujilinda wenyewe.   
Waziri wa Nchi, OWM- Sera, Uratibu na Bunge William Lukuvi (kulia) akimpongeza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa Kamishana Mwandamizi Msaidizi, Michael Kamuhanda (kushoto) (katikati) ni Afisa Muuguzi Muuguzi msaidizi mkuu Lustica Tun’gombe. 

Akiongelea maendeleo ya mapandri hao, Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Iringa, Dk. Faustine Gwanchele amesema kuwa mapadri hao wanaendelea vizuri kwa ujumla.
=30=

No comments:

Post a Comment