Sunday, November 18, 2012

MASHINE YA ULTRASOUND YAFUNGWA AGA KHAN



Hospitali ya Aga Khan Iringa imefunga mashine mpya ya kisasa ya Ultrasound iitwayo Sonoace R5 iliyotengenezwa na kampuni ya Samsung Medison kwa lengo la kutoa huduma bora za Ultrasound mkoani Iringa na maeneo ya jirani.


Mtaalamu wa kuendesha mashine ya Ultrasound katika Hospitali ya Aga Khan Iringa John Mwega akifanya uchunguzi muda mfupi baada ya kufungwa kwa mashine ya kisasa ya Ultrasound  Sonoace R5 jana.


Mashine ya kisasa ya Ultrasound Sonoace R5

Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti la Uhuru, Mratibu wa huduma za matibabu (PMC) kwa hospitali za Aga Khan, Saidu Beyai amesema kuwa hospitali ya Aga Khan imeamua kufunga mashine hiyo kwa lengo la kuboresha huduma za uchunguzi kwa wagonjwa wanaohitaji uchunguzi huo kwa njia ya Ultrasound. Amesema kuwa mashine hiyo pia itaboresha uchunguzi wa ubora wa huduma hiyo na matokeo yake kwa wanawake wajawazito kwa haraka na ubora unaokubalika.

Nae mtaalamu wa uendeshaji wa mashine hiyo, John Mwega amesema kuwa mashien hiyo italeta mapinduzi ya kimatibabu katika uchunguzi na matibabu kwa sababu mashine hiyo inazo probu tatu tofauti na ile ya awali iliyokuwa ndogo na kuwa na probu moja jambo lilikuwa likizuia uchunguzi wa baadhi ya magonjwa katika mwili wa binadamu. Amesema kuwa tofauti na ile mashine ya awali, mashine hii mpya itakuwa ikiwezesha uchunguzi wa matatizo ya ndani zaidi ya wanawake tofauti na mashine ya awali iliyokuwa inatumika zaidi nje (juu ya tumbo la mwanamke).

Mwega amesema kuwa mashine hii kubwa zaidi itasaidia hata matatizo ya mishipa ya damu kuweza kuangaliwa vizuri tofauti na awali sambamba na ubora wa picha zitakazopigwa.
Akielezea umuhimu wa mashine hiyo katika kumsaidia daktari kumhudumia mgonjwa wake vizuri, mtaalamu huyo wa uendeshaji mashine amesema “unapoweza kutambua ugongwa mapema unaweza kumhudumia mgonjwa wako mapena na kwa haraka hivyo kuweza kuhudumia wagonjwa wengi kwa haraka tofauti na ilivyokuwa awali”. Amesema mashine hiyo mpya inaweza kufanya uchunguzi kwa ogani za mwili kwa wanaume na wanawake.

Amesema kuwa mashine hiyo ni mzuri zaidi kwa sababu inao uwezo mkubwa wa kuhifadhi picha na taarifa za mgonjwa jambo linaloweza kumsaidia daktari kuweza kufanya ulinganifu na kushauriana na madaktari wengine katika kupata ufanisi wa tiba. Aidha, ametoa wito kwa wananchi kuweza kufika katika hospitali hiyo kwa ajili ya huduma hizo bora na za kisasa za Ultrasound.

Ikumbukwe kuwa hospitali ya Aga Khan imekuwa ikipokea kati ya wagonjwa 10-25 kwa siku kwa huduma za Ultrasound.
=30=

Picha IMG 7863 mashine ya Ultrasound  Sonoace R5 jana ikioa majibu ya kipimo.

No comments:

Post a Comment