Monday, December 16, 2013

KINAMAMA WA KIKUNDI CHA SONGAMBELE WAONESHA MFANO MZURI KWA KUHUDUMIA WATOTO YATIMA




Jamii imetakiwa kutenga muda wa kuwasaidia watoto walio katika mazingira magumu ili kuwatia moyo na kuwasaidia kufikia malengo yao.


          Mkuu wa Kituo cha Amani, Mama Erica Mwakalebela 



Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa kituo cha kulelea watoto yatima cha Amani kilichopo wilayani Kilolo Erica Mwakalebela alipokuwa akiwasilisha taarifa fupi ya kituo kwa akina mama wa kikundi cha Songambele chenye makazi yake Manispaa ya Iringa walipotembelea kituo hicho kuongea na watoto na kuwapatia zawadi mbalimbali.

Erica amesema kuwa watoto yatima wanahitaji kusaidiwa kwa hali na mali. Amesema “hatuwezi kuwa wakamilifu kama hatutatoa muda wetu kuwasaidia watoto yatima. Watoto hawa ni wetu hivyo jukumu la kuwahudumia ni letu sote”. Ametoa rai kwa jamii mzima kutenga muda na rasilimali kuwahudumia watoto yatina na watoto walio katika mazingira magumu. Amesema kuwa watoto yatima kama walivyo watoto wengine wanamalengo mbalimbali katika maisha yao ambayo ili waweze kuyatimiza ni lazima jamii iweze kuwasaidia kuyafikia. Amesema kuwa kuwawezesha kuyafikia malengo hayo kutawasaidia kutimiza jukumu lao katika ujenzi wa familia zao na Taifa kwa ujumla. 


Akiongelea mafanikio ya kituo hicho, mkuu wa kituo hicho ameyataja kuwa ni kuwalea na kuwasomesha watoto katika hatua mbalimbali kuanzia shule ya msingi, sekondari, vyuo vya ufundi, utalii hadi chuo kikuu. Ameyataja mafanikio mengine kuwa ni kuwasaidia watoto katika kituo hicho hadi kupata ajira kwa wale waliokamilisha masomo yao. Aidha, amesema kuwa kituo hicho kimekuwa kikiajiri pia watoto wanaofanya vizuri katika masomo yao na fani mbalimbali katika miradi inayoendeshwa kituoni hapo.


Erica amezitaja baadhi ya changamoto zinazokikabili kituo chake kuwa ni elimu, chakula na ajira kwa watoto hao. Aidha, ametoa wito kwa wafadhili na wadau wengine kujitokeza na kukisaidia kituo hicho katika kukabiliana na changamoto hizo.


Mwenyekiti wa Kikundi cha Songambele, Mama Rehema Dunga
Akitoa nasaha zake kwa watoto yatima wa kituo cha Amani, Mwenyekiti wa kikundi cha kinamama cha Songambele, Rehema Dunga amewataka watoto hao kutokukata tamaa katika maisha yao na kusongambele. Akielezea lengo la kutembelea kituo hicho, Mwenyekiti wa Songambele amesema kuwa lengo ni kukutana na kuzungumza na watoto hao ili kuwasaidia kusongambele. 

Amewataka watoto hao kuwa wasikivu na wenye kujituma katika kile wanachofundishwa ili waweze kufanikiwa. “Wakinamama wa Songambele tumekuja hapa kuwaonesha upendo na kuwatia moyo msirudi nyuma bali msongembele katika kila jambo mnalolifanya katika maisha yenu” alisisitiza Rehema. 


Katika ziara ya kikundi hicho kwa kituo cha kulelea watoto yatima Amani, kinamama wa Songambele walipika chakula cha mchana kwa watoto hao zaidi ya 100. Aidha, walipeleka zawadi mbalimbali kama sabuni, madaftari, kalamu, mafuta, maji, juisi, dawa za meno, miswaki pamoja na vitu vingine vyote vikiwa na thamani ya zaidi ya Tshs. 650,000/=


 Miongoni mwa zawadi zilizotolewa na kinamama wa Songambele kwa kituo cha Amani

Kikundi cha kinamama cha Songambele kilianzishwa miaka miwili iliyopita kwa lengo la kuwawezesha kina mama na familia zao kusonga mbele kimaendeleo. Kikundi kina wanachama 24 kikiwa na makao makuu eneo la Lugalo, Manispaa ya Iringa. 

                                                      Kinamama wa Songambele


       Kinamama wa Songambele wakiwa katika Pozi la pamoja
=30=

No comments:

Post a Comment