Tuesday, December 10, 2013

HOTUBA YA MKUU WA MKOA WA MKOA IRINGA, WAKATI WA KONGAMANO LA MAADHIMISHO YA MIAKA 52 YA UHURU LILILOFANYIKA 9/12/2013 SIASA NI KILIMO




Ndugu, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa,
Viongozi wa Wanafunzi kutoa Vyuo Vikuu,
Wawezeshaji,
Maafisa Mbalimbali wa Serikali,
Wanafunzi wote wa Vyuo Vikuu,
Wageni Waalikwa,
Mabibi na Mabwana,

Awali ya yote napenda kuungana nanyi nyote kumshukuru mwenyezi Mungu kwa kutulinda sisi na Nchi  yetu ya Tanzania tangu tupate uhuru 09/12/1961 hadi leo hii, ikiwa ni miaka 52 Nchi yetu imeendelea kuwa na amani na utulivu pamoja na mafanikio makubwa katika Nyanja za Kiuchumi na Huduma na jamii. Hatuna budi sote kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa Baraka na ukarimu wake.

Aidha, nichukuwe fursa hii pia kutoa shukrani zangu za dhati kwa wanafunzi wa Vyo Vikuu vyote Mkoani Iringa kwa kuhudhuria katika Kongamano hili. Ni imani yangu mtajifunza mengi ambayo yatakuwa na manufaa kwenu na kwataifa kwa ujumla.


Ndugu Washiriki,
Sio rahisi kusherehekea Miaka 52 ya Uhuru bila kukumbuka juhudi zilizofanywa na Baba wa Taifa na Muasisi wa Chama cha TANU katika harakati za kupigania Uhuru. Ni ukweli usiopingika kuwa hali ya nchi yetu ilikuwa duni sana wakati  wa uhuru kutokana na ujenzi wa mfumo wa Ubepari, Ukabaila na Unyonyaji uliojengwa wakati huo na wakoloni.

Hali hii ilihitaji juhudi zenye dhamira ya Kizalendo zilizofanywa kupitia Azimio la Arusha, Siasa ya Ujamaa na kujitegemea, Siasa ni kilimo, Operation Vijiji, Kisomo chenye Manufaa, kuunganishwa kwa TANU na  ASP  na kuzaliwa kwa CCM, kurejeshwa kwa serikali za Mitaa, kuanzishwa kwa Utaratibu wa kung’atuka kwa viongozi(MARAIS) kwa mujibu wa Katiba nk.

Ndugu Washiriki,
Mwaka huu ni mwaka wa 52 wa Uhuru, tumepata maendeleo makubwa katika kipindi chote hiki. Nichambue kwa ufupi wapi “tulikotoka”.

Mwaka 1982 chini ya Sheria ya Serikali za Mitaa na 7 – 12 ilipitishwa kama maandalizi ya awali kuanzisha serikali za Mitaa nchini.

Nchi ilipopata uhuru haikuwa Taifa ila nchi ya watu wasiozisi milioni 8 wa makabila karibu 126 ambao hawakuwa na mawasiliano ya karibu wala lugha moja ya kitaifa, Tanzania sasa ni nchi na Taifa kamili huru na imara yenye umoja mshikamano, amani na utulivu ikiwa mfano wa kuigwa barani Africa.

Leo hii, Watanzania bila kujali hali halisi ya maisha yao  ya kila siku wanajisikia kuwa huru wana jeuri ya utu wao na wanajisikia kuwa  sawa na binadamu wengine kokote duniani. Wakati wa uhuru na miaka iliyopita baada ya uhuru, nchi haikuwa na wasomi wengi Wazalendo.  Wote tutakumbuka wakati wa uhuru Tanzania bara ilikuwa wahitimu wa kiwango cha Chuo Kikuu 120(wanasheria 2, wahandisi 2, Madaktari wa binadamu 12 na wengineo. Sasa Tanzania bara inao wasomi na wataalam wengi walioshika nafasi za ushauri na uamuzi serikali na katika Taasisi nyeti za kitaifa.

Tulipopata uhuru, kilikuwepo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kimoja kilichokuwa na wanafunzi 14 wa kitivo cha Sheria tu. Sasa Tanzania ina vyuo vikuu na vyuo vishiriki zaidi ya 30 ambapo Mkoa wa Iringa unavyo Vikuu 5. Tumepiga hatua kubwa.

Ndugu Washiriki,
Hali ya Miundombinu ya Mawasiliano ilikuwa duni sana mwaka 1961 wakati wa Uhuru.

Mawasiliano ya barabara yalikuwa mabovu ambapo barabara zote zilikuwa za udongo zisizokuwa na Madaraja /Makaravati na zisizopitika wakati waote wa masika. Hakukuwepo na mawasiliano ya simu, Redio wala Televisheni, sasa kuna Televishen, Simu za mkononi, Fax, e-mael na Radio za masafa yote.
Katika kipindi cha miaka 52 ya uhuru wa nchi yetu, barabara zimeboreshwa na mpya kujengwa. Mfano mzuri barabara ya Iringa – Dodoma, Iringa Dar es Salaam, Iringa Mbeya, Iringa Njombe nk. Haya ni mafanikio Makubwa. Haya ni baadhi tu ya mafanikio lakini, tumepata mafanikio katika Nyanja zote, na mafanikio haya yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na vijana.


Ndugu Washiriki,
Kauli mbiu ya Miaka 52 ya Uhuru ni; “Vijana ni nguzo ya rasilimali watu; Tuwaamini, Tuwawezeshe, na Tuwatumie kwa Manufaa ya Taifa letu”.

Mkoa wetu una bahati kubwa ya kuwa na vijana wengi wenye shauku na ari ya kufanya kazi ambao ni rasilimali muhimu sana katika vita ya kupambana na umaskini. Vijana hawa wanawezeshwa na Wadau mbalimbali kupata elimu katika Vyuo Vikuu tulivyo navyo hapa Iringa. Aidha, Mkoa unawahadhiri wengi ambao ni hazina ya mawazo ya kimaendeleo kwa Vijana hawa, wahadhiri hawa hutoa ushirikiano mkubwa kwa Vijana. Hivyo, nitoe wito kwa Vijana kutumia elimu na fursa zilizopo kujiletea maendeleo yao wenyewe na Taifa kwa ujumla. Kwani Taifa linawategemea sana Vijana.

Aidha, Tuunganishe fikra zetu na nguvu tulizo nazo, tuunde vikundi, tufanye kazi kwa bidii, tutumie muda vizuri, tutambue wajibu wetu katika kulijenga Taifa letu, hakika tutafanikiwa. Fursa za kujiletea maendeleo ni nyingi sana, tuungane pamoja ili tutoke. Naamini tutapata maendeleo makubwa.


Baada ya maelezo haya machache, nimefungua Kongamano hili.

Ahsanteni kwa kunishiliza.

No comments:

Post a Comment