Sunday, November 26, 2017

JAMII YATAKIWA KUAMKA KUTETEA USAWA WA KIJINSIA



Na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa-Iringa
Wanawake na watoto wameendelea kuwa wahanga wa vitendo vya ukatili wa kijinsia na kukabiliwa na mgawanyo usio sawa wa rasilimali na madaraka kutokana na mwamko mdogo wa jamii kuhusu usawa wa kijinsia.

Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza katika hotuba yake ya uzinduzi wa kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia, uliofanyika ngazi ya mkoa katika halmashauri ya wilaya ya Kilolo na kusomwa kwa niaba yake na mganga mkuu wa mkoa Dr Robert Salim.

Mkuu wa Mkoa alisema “katika mkoa wetu wa Iringa, vitendo vya ukatili wa kijinsia vimekuwa vikifanyika katika maeneo mbalimbali, wanawake na watoto wamekuwa ndiyo wahanga wakubwa. Kwa mfano, wanawake wameendelea kukabiliwa na mgawanyo usio sawa wa rasilimali na madaraka kati yao na wanaume, kukosekana kwa usawa kunakichangiwa na mfumo dume uliopo katika jamii, wanawake kunyanyaswa, kubaguliwa, kupigwa, kutelekezwa na watoto, kutokushirikishwa katika maamuzi hata yale yanayohusu maisha yao”. 

Aliongeza kuwa watoto pia wamekuwa wakinyimwa haki zao za msingi katika jamii.

Mkuu wa mkoa alisema kuwa kumekuwa na matukio ya watoto kubakwa na kulawitiwa, mimba za utotoni, kupigwa na kuterekezwa. ”Idadi ya watoto waliofanyiwa ukatili wa aina tofauti kwa kipindi cha kuanzia Julai 2016- hadi Oktoba, 2017 imefikia watoto 606. Watoto 306 wameripotiwa kufanyiwa ukatili wa kingono na watoto 300 ukatili mwingine kama kupigwa na kadharika. Inashangaza kuona kwamba idadi kubwa ya vitendo vya ukatili dhidi ya watoto vimekuwa vikifanywa majumbani, shuleni au njiani, ukatili huu umekuwa ukifanywa na watu au ndugu wa karibu wa familia husika” alisisitiza Mkuu wa Mkoa.

Mkuu wa Mkoa alisema kuwa kwa kipindi cha miaka miwili, wanawake 904 wamefanyiwa ukatili. Ukatili huo umewaathiri kiafya, kijamii, kisaikolojia na kiuchumi. Ukatili wa kijinsia umekuwa ukichangia kuongezeka kwa maambukizi ya virusi vya ukimwi na magonjwa mengine yatokanayo na ngono.
 =30=

No comments:

Post a Comment