Sunday, November 26, 2017

VETA IRINGA WATAKIWA KUSIMAMIA MAFUNZO STADI KULINGANA NA UHITAJI WA SOKO LA AJIRA



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, IRINGA
Mamlaka ya elimu na mafunzo ya ufundi stadi imetakiwa kuendelea kusimamia na kuratibu mafunzo studi nchini ili mafunzo yanayotolewa yawe na ubora unaokidhi mahitaji ya soko la ajira.

Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Katibu Tawala Msaidizi- Mipango na Uratibu katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Nuhu Mwasumilwe katika mahafali ya 21 ya chuo cha mafunzo ya ufundi stadi na huduma Iringa yaliyofanyika katika viunga vya chuo cha VETA mjini Iringa.

Mkuu wa Mkoa alisema “kimsingi mamlaka ya elimu na mafunzo ya ufundi stadi bado ina kazi kubwa ya kusimamia, kuratibu, kugharamia, kutoa na kuendeleza mafunzo ya ufundi stadi nchini ili kufikia dhamira kuu ambayo ni kuhakikisha mafunzo yanayotolewa yanakuwa na ubora unaokidhi mahitaji ya soko la ajira”. Aidha, aliitaka mamlaka kuendelea kuboresha fani nyingine zinazohitaji maboresha makubwa kama karakana ya magari.

Akiongelea hitaji la wahitimu la kuunganishwa na fursa zinazohusu vijana ili kuwawezesha kuendana na mbadiliko ya teknolojia na soko la ajira, alisema kuwa sualaa hilo ni changamoto. “Suala hili ni changamoto kwa mamlaka, wazazi na hata wahitimu pia. Ninapenda kutumia mahafali haya kuwashauri wazazi kushiriki kikamilifu kuwasaidia ninyi katika hali ya mmoja mmoja, lakini nikishauri zaidi kwamba ninyi wahitimu kuunda na kusajili vikundi vyenye utaratibu mzuri wa usimamizi na uzalishaji wenye faida ambavyo vitaweza kuwapa fursa ya kupata mitaji kupitia taasisi mbalimbali za kifedha pamoja na mifuko ya vijana inayosimamiwa na halmashauri zetu” alisema mkuu wa Mkoa.

Akiongelea ombi la serikali kugharamia mafunzo ya vitendo, mkuu wa Mkoa alisema kuwa suala hilo linahitaji majadilianao na mamlaka husika. Aidha, aliwakumbusha wazazi kuwa wanawajibu wa kuwasaidia watoto wao kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Katika risala ya wahitimu wa chuo hicho iliyosomwa na Geofrey Simon ilieleza kuwa changamoto ni kutokuwa na walimu wa kutosha kukidhi mahitaji na uwiano sahihi katika kufundisha baadhi ya masomo. Alisema kuwa jambo hilo hupelekea walimu waliopo kuwa na mzigo mkubwa wa kufundisha idadi kuwa ya wanafunzi katika masomo ya hisabati, kiingereza, ujasiriamali na michoro ya maumbo. Changamoto nyingine ni chuo kukosa gari la kusafirishia wanafunzi waendapo kutembea maeneo ya mafunzo na michezo.

Simon aliongeza kuwa karakana nyingi za chuo zina vifaa na mitambo ya kufundishia iliyopitwa na wakati na kufanya mafunzo kutokidhi ubora wa soko la ajira. “Serikali kutokuwadhamini wanachuo fedha ya kufanya mafunzo ya vitendo, hivyo wazazi wengi kushindwa kumudu gharama husika imekuwa ni changamoto kubwa” alisema Simon.

Katika taarifa ya mkuu wa chuo cha mafunzo ya ufundi stadi na huduma iringa, Raphael Ng’wandu alisema kuwa chuo chake kimefanikiwa katika kugharamia mafunzo kwa wanafunzi wote waliodahiliwa. Alisema kuwa mamlaka imekuwa ikigharamia chakula na malazi kwa wanafunzi wanaokaa bweni.

Ng’wandu alisema kuwa chuo chake kinakabiliwa na changamoto ya kuwa na vifaa vya muda mrefu visivyoendana na teknolojia ya sasa. Alisema kuwa chuo chake kina mkakati wa kuboresha karakana za mafunzo kwa kununua vifaa vipya vya mafunzo vya kufundishia. Aidha, mamlaka imeendelea kuboresha bajeti ya mafunzo mwaka hadi mwaka.

Chuo cha mafunzo ya ufundi stadi cha Iringa kilianzishwa mwaka 1987 chini ya idara ya mafunzo na majaribio ya ufundi (NVTD) iliyokuwa chini ya wizara ya kazi. Fani za kwanza kutolewa zilikuwa ni uashi, bomba, useremala na umeme.  
=30=

No comments:

Post a Comment