Sunday, December 9, 2012



HOTUBA YA MKUU WA MKOA WA IRINGA MHESHIMIWA DR. CHRISTINE G. ISHENGOMA (MB) WAKATI WA MAADHIMISHO YA SIKU YA UHURU WA TANZANIA BARA 09/12/2012 KIMKOA KATIKA TARAFA YA MAHENGE WILAYA YA KILOLO

Ndugu Kaimu Katibu Tawala Mkoa,
Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya,
Mheshimiwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo,
Mheshimiwa Mbunge,
Mhe. Mwenyekiti wa CCM (W),
Ndugu Katibu wa CCM (W),
Makatibu Tawala Wasaidizi Sekretarieti ya Mkoa,
Waheshimiwa Madiwani,
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Kilolo,
Viongozi wa Madhehebu ya Dini,
Viongozi wa Vyama vya Siasa,
Waandishi wa Habari,
Mabibi na Mabwana.
Ndugu Wananchi,

Awali ya yote napenda kuchukua fursa hii kutoa shukrani zangu za dhati kwa wananchi wa Tarafa ya Mahenge kukusanyika katika Viwanja hivi tukiwa na lengo la kuadhimisha na kuyakumbuka yale yote yaliyofanyika toka tumepata uhuru 9/12/1961.


Aidha, natumia fursa hii kuwashukuru Viongozi na Wananchi wa Wilaya ya Kilolo kwa maandalizi mazuri na kwa kukubali kwao kuadhimisha siku hii muhimu kwa Watanzania wote.

Vilevile, nawashukuru Vikundi vya burudani kwa kutumbuiza vizuri, na kwa ujumbe ambao mumetuachia na kutuasa. Nasema asanteni sana.


Ndugu Wananchi,
Mkoa wa Iringa ulianzishwa Mwaka 1964 kutoka Mkoa wa zamani ambao uliitwa Jimbo la Kusini la Nyanda za Juu. Makao Makuu yakiwa Mbeya. Mkoa ulikuwa na Wilaya mbili ambazo ni Njombe na Iringa. Wilaya ya Mufindi ilianzishwa Mwaka 1964, Wilaya ya Ludewa Mwaka 1975, Makete Mwaka 1979 na Kilolo  Mwaka 2002.
Na Mwaka huu 2012 Mwezi Julai Mkoa wa Iringa uligawanywa rasmi na kuunda Mkoa mpya wa Njombe. Haya ni mafanikio makubwa sana.

Mkoa wetu wa Iringa kiutawala umegawanyika katika Wilaya tatu ambazo ni Iringa, Kilolo na Mufindi. Mkoa pia umegawanyika katika Halmashauri nne ambazo ni Halmashauri ya Manipaa ya Iringa na Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Kilolo na Mufindi.  Aidha Mkoa umegawanyika katika Tarafa 15 Kata 93, vijiji 357 na Mitaa 164.

Ndugu Wananchi,
Shughuli kuu za uchumi za Mkoa wa Iringa ni Kilimo, ufugaji, upasuaji mbao, uvuvi, biashara na ajira za maofisini na viwandani.  Asilimia 85 ya wakazi wa Iringa hujishughulisha na kilimo au kilimo na ufugaji na katika shughuli hizi tumepata mafanikio makubwa.

Ndugu Wananchi,
Tuko hapa leo kuadhimisha sherehe za miaka 51 ya uhuru wa Tanzania bara. Kauli mbiu ya sherehe za uhuru mwaka huu ni uwajibikaji , uadilifu na uzalendo ni nguzo ya maendeleo ya Taifa letu.

Ni ukweli usio pingika tukiwajibika ipasavyo, tukiwa waadilifu, na wazalendo kuanzia kweye kaya hadi Taifa tutalitumikia Taifa na kupata maendeleo yanayohitajika. Hivi vitu 3 ni msingi mkubwa sana wa maendeleo ya Nchi yetu, hivyo kila mmoja inampasa kutimiza kauli mbiu hii.


Ndugu Wananchi,
Mkoa wa Iringa umepata mafanikio makubwa toka tulipopata uhuru mpaka sasa kutokana na Waasisi wetu, wazazi na walezi wetu kuwajibika, kuwa waadilifu na kuwa wazalendo wa kweli katika kutekeleza majukumu yao. Miongoni mwa Mafanikio hayo ni pamoja na:- Mwaka 1961 pato la Mkoa lilikuwa ni Sh. 5,693,000 na Wastani wa pato la mtu kwa mwaka lilikuwa ni Sh. 103. Aidha, pato la Mkoa kwa mwaka 2011 lilikuwa Sh. 1,985,708,000 na pato la mkazi lilikuwa Sh. 1,225,503. Hii ni hatua kubwa kwa Mkoa wa Iringa.

Katika ukusanyaji wa Mapato ya Halmashauri mwaka 2011/12 Sh.9,357,013,391 zilikusanywa kutoka vyanzo vya ndani, kumekuwa na ongezeko la Sh. 9,355,366,502 ikilinganishwa na mapato ya Sh. 1,646,889 ya mwaka 1961/62.

Ndugu Wananchi,
Kilimo,  
Eneo linalolimwa mazao mbalimbali limeongezeka kutoka Hekta 305,208.65 mwaka 1961/62 hadi kufikia Hekta 411,116 zilizolimwa msimu 2011/12. Elimu ya kilimo bora ilitolewa kwa wakulima na jumla ya mashamba darasa 1,603 yalianzishwa na jumla ya wakulima 49,075 wamepatiwa mafunzo kwa vitendo kupitia mashamba haya kwa kipindi cha 1961 hadi 2011.Pia ili kufikisha Elimu kwa Wakulima waliowengi Mkoa umeanzisha vituo vya rasilimali watu wa Kilimo katika Kata 17.

Mbolea,
Mbolea zilizotumika mwaka 1961/62 zilikuwa tani 16,826 na tani 300 za mbegu. Ukilinganisha na tani 42,250 za mbolea na tani 3,142 za mbegu mwaka 2011 hii ni sawa na ongezeko la asilimia 251 kwa matumizi ya mbolea.

Ndugu Wananchi,
Mifugo,
Mwaka 1961 Mkoa ulikuwa na Idadi ya Ng`ombe wa Kienyeji 9,176, Idadi ya ng’ombe wa maziwa na nyama 19,  Majosho 69, Uzalishaji wa Maziwa lita 1,592,662. Hadi kufikia mwaka 2012 Mkoa una Ng’ombe kienyeji 568,749, Ng’ombe wa Maziwa 28,081, Majosho 211, uzalishaji wa Maziwa Lt 7,676,481.

Sekta ya Ushirika
Mwaka 1961 Mkoa ulikuwa na Vyama vya ushirika 2 vyenye Idadi ya Wanachama 460 na mtaji wa Tsh. 1,620,000. Hadi sasa Mkoa una jumla ya Vyama vya Ushirika hai 205 Vyenye Idadi ya Wanachama 36,873 na Mtaji wa Tsh 7,870,145,046.

Viwanda na Biashara
Mkoa hadi sasa unavyo viwanda 29 vinavyojihusisha na usindikaji wa bidhaa mbalimbali.  Sekta ya Viwanda na Biashara, inaajiri watu takriban 15,000 hii ni sawa na   asilimia 1.5 ya wakazi 1,006,731 wa Mkoa wa Iringa. 

Vyanzo vya maji
Hadi kufikia 2012 jumla ya vyanzo vya maji 2600 vilikuwa vimetambuliwa na jumla ya vyanzo 1752 vimehifadhiwa. Mkoa unaendelea na jitihada za kuhakikisha vyanzo vyote vinahifadhiwa.

Upandaji wa miti
Mwaka 1961 Jumla ya miti 3,507,802 ilipandwa katika Mkoa wa Iringa, Mwaka 2011 Mkoa umefanikiwa kupanda Jumla ya miti 43,515,611. Wananchi wanahamasishwa kuendelea kupanda miti ili kuweza kujipatika kipato na kuhifadhi mazingira. Mizinga hadi kufikia 2012 Mkoa unajumla ya Mizinga 25,783 ya asili ni 17,389 na ya Kisasa ni 8394.

Utalii
Katika kipindi cha 1961 hadi 2012, Mkoa umeainisha vivutio vya Utalii na unaendelea na zoezi hili kwa kushirikiana na wadau mbalimbali. Zaidi ya vivutio 78 vilikuwa vimetambuliwa hadi kufikia 2012.


Ndugu Wananchi
Elimu,
Kwa kipindi cha 1961 hadi 2012 yamepatikana mafanikio yafuatayo:
·        Kuongezeka kwa madarasa ya awali toka 67 hadi 425.
·        Kuongezeka kwa wanafunzi toka 3,015 Hadi 28,725.

Elimu ya Msingi.
Mkoa umekuwa na Maendeleo ya kuridhisha ya utoaji taaluma kwa kutumia kigezo cha matokeo ya mtihani wa kuhitimu Elimu ya Msingi. Katika kipindi cha 1961 hadi 2011 idadi ya wanafunzi waliofaulu imeongezeka kutoka 347 hadi 27,899 ikiwa ni ongezeko la wanafunzi 27,552.


Elimu ya Sekondari
Mwaka 1961 Mkoa ulikuwa na shule za Sekondari zipatazo 6, hadi Mwaka 2012 Mkoa unajumla ya shule za Sekondari 148, kati ya hizo za umma 104 na za Binafsi (Non-Government Secondary Schools) i.e. Seminari, na za Watu na Mashirika mbalimbali ya Binafsi 44.

Ndugu Wananchi,
Afya,
Mkoa wa Iringa hadi kufikia mwaka 2012 una jumla ya vituo vya kutolea huduma za Afya 254 vilivyogawanyika kama ifuatavyo; Hospitali 7, Vituo vya Afya 21 na Zahanati 226.

Kiwango cha mama wajawazito wanaojifungulia katika vituo vya tiba imeongezeka kufikia asilimia 88 mwaka 2011 ikilinganishwa na asilimia 5 mwaka 1961.

Ndugu Wananchi
Maji,
Asilimia ya wakazi wa Mkoa wa Iringa waliokuwa wakipata huduma ya maji safi na salama Desemba 1961 ni 10%.  Asilimia ya wakazi wanaopata huduma ya maji safi na salama Desemba 2011 ni 67.3 %.  Ongezeko la asilimia ya wakazi wanaopata huduma ya maji ni 56.4%.
Ndugu Wananchi,
Barabara,
Mwaka 1961 Mkoa ulikuwa na mtandao wa barabara upatao Km. 1,209.5 kati ya hizo Km. 76.0 ni barabara za vumbi na Km. 1,133.5 ni changarawe.  Mtandao huo Desemba 2011 umeongezeka hadi kufikia Km. 4,786 kati ya hizo Km. 359 ni Lami, Km. 2123 changarawe  na Km.2,304 ni udongo. 

Ndugu Wananchi, Teknolojia,
Mwaka 1961 Technolojia ya Kompyuta, Mawasiliano na habari haikuwepo Mkoani Iringa. Tulikuwa na Radio moja tu,  Radio Tanzania. Lakini hadi kufikia Mwaka, 2012 Mkoa wa Iringa umekuwa na Technolojia ya Habari, TV, Radio katika maeneo yote ya Mkoa wa Iringa. Mawasiliano yameimarika na wananchi wanafurahia maendeleo ya habari Mfano radio Ebony, Nuru, Country, Furaha, Ovecomers, Qibraten N.k.

Ndugu Wananchi,
Pamoja na mafanikio haya mkoa umepata changamoto mbalimbali ambazo ni pamoja na Mkoa wa Iringa umeathirika kwa kiwango kikubwa sana na tatizo la UKIMWI (asilimia 15.7). Hivyo nawaasa kila mmoja wetu anapaswa kubadili tabia ili kupunguza kiasi cha maambukizi.

Pia, naomba akibnababa msiwanyanyase akinamama na pia akinamama msiwanyanyase akinababa. Muendelee kuishi kwa upendo, utulivu na amani katika maisha yenu yote. Tupunguze kabisa unyanyasaji wa kijinsia.

Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ubariki Mkoa wetu wa Iringa.


Asanteni kwa Kunisikiliza.


Saturday, December 8, 2012

USHIRIKIANO BAINA YA WANANCHI NA WAWEKEZAJI UDUMISHWE



Serikali imepongeza ushirikiano uliopo baina ya wananchi wa kijiji cha makungu na muwekezaji wa kiwanda cha karatasi cha Mgololo (MPM) katika kuchangia maendeleo ya wananchi.

Pongezi hazi amezitoa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma alipozindua mradi wa maji wa kijiji cha Makungu uliofadhiliwa na kiwanda cha karatasi cha Mgololo wilayani Mufindi.

Dkt. Christine amesema  “ushirikiano baina ya muwekezaji kiwanda cha karatasi cha Mgololo na wananchi ni jambo la kupongezwa sana katika kusogeza huduma za kijamii karibu zaidi na wananchi”. Amesema “mtu anayekupa maji anakupa uhai hivyo mnawajibu wa kutunza na kulinda miundombinu hii ya maji ili muweze kujihakikishia wahakika wa maji na kuufanya mradi huu kuwa endelevu”. Aidha, ametoa wito kwa wawekezaji wengine kuona kuwa wanawajibu wa kuisaidia jamii inayowazunguka kwa kufadhili miradi nashuighuli za kijamii ili kudumisha ushirikiano na uhusiano mwema.

Katika taarifa ya kijiji iliyowasilishwa na Afisa Mtendaji wa kijiji Ephaim Mhelela amesema kuwa kijiji kupata mradi huo kimefanikiwa kupunguza tatizo la maji kutokana na kuwa na bomba moja tu  la maji lililokuwa katika kitongoji kimoja kabla ya mradi huo.  

Amezitaja changamoto katika mradi huo kuwa ni pamoja na ukubwa wa eneo la kijiji jambo linalofanya baadhi ya vitongoji visifikiwe kwa urahisi kutokana na umbali. Changamoto nyingine ameitaja kuwa ni maji kutotosheleza kwa watumiaji wote waliofungiwa bomba kutokana na uchache wa naji yanayopatikana katika tenki na ukosefu wa fedha za kuendeshea mradi ili huduma hiyo iwafikie wananchi wote.

Aidha, ameitaja baadhi ya mikakati ya kukabiliana na changamoto hizo kuwa ni pamoja na kutumia nguvu kazi ya wananchikwa kuchimba mitaro ya maji pindi pale bomba zinapopatikana za kusambaza maji na kuanzisha mfuko wa maji kwa kuwachangisha wananchi wenyewe.

Mradi huo wa maji unahudumia kijiji cha Makungu chenye vitongoji saba na idadi ya kaya 1,445 na wakazi 6,125, wakiwepo wanawake 3,230 na wanaume 2,895. aidha jumla ya watu wenye uwezo wa kufanya kazi ni 3202.
=30=
RC ATAKA BONDE LA MGOLOLO LITUMIKE VIZURI


Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma amewataka wananchi wa Kata ya Makungu na Kiyowela kulitumia vizuri bonde la Mgololo kwa kujihakikishia chakula cha kutosha na kulima klibiashara.

Ushauri huo ameutoa alipofanya ziara ya siku mbili ya kutembelea, kuhamasisha na kukagua shughuli za maendeleo katika wilaya ya Mufindi.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma

Dkt. Christine amesema kuwa ili bonde hilo liweze kuwa na manufaa kwa wananchi ni lazima litumiwe vizuri kwa wananchi kulima kwa kufuata nanuni la kilimo bora ili waweze kujihakikishia chakula cha kutosha. Amesema kuwa uhakika wa chakula cha kutosha ni muhimu sana kumuwezesha mwananchi kutekeleza majukumu yake ya kujiletea maendeleo. Amesema “ili mtu uweze kufanya shughuli za maendeleo ni lazima awe ameshiba, ili awe ameshiba, ni lazima awe na chakula na uhakika wa chakula cha kutosha, hivyo litumieni bonde hili kwa kujihakikishia chakula cha kutosha”.

Aidha, amesisitiza kutanuliwa kwa skimu ya umwagiliaji maji katika bonde hilo ili kuongeza uzalishaji wa mazao. Amesema “katika kilimo cha umwagiliaji hakuna kupumzika, yaani unapanda, unavuna na kupanda tena”. Amesema kupitia kilimo cha umwagiliaji, wakulima hao waangalie kuboresha zaidi kilimo chao na kuwa kilimo cha kibiashara. Amesema kuwa kufanya hivyo kutawakikishia uhakika wa chakula na kuuza mazao yao jambo litakalowawezesha kuwa na fedha nyingi kwa ajili ya matumizi mengine.

Akiwasilisha taarifa ya mradi wa umwagiliaji maji Mgololo kwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Emelitha Nganung’a amesema kuwa ujenzi wa banio na mfereji mkuu wa mita 400 ulifanyika mwaka2007/2008 sambamba na barabara ya Lugolofu hadi mashambani yenye km 9 ilitengenezwa. Mwaka 2009-2011 ujenzi wa mfereji mkuu wenye urefu wa km 4.8 na mifereji ya kati km 12.33 pia ilijengwa. Amesema kuwa aktika mfereji mkuu madaraja matano makubwa na madaraja matano madogo yamejengwa. Aidha, amesema vigawa maji 12 na makaravati 13 vilijengwa. Mifereji ya kati vijawa maji 54 vilijengwa. Mifereji midogo ilipimwa na kuwa na urefu wa km 23.80. Amesema jumla ya hekta 259 zimepimwa kati ya hekta 600 na wakulima 91 wamegawiwa mashamba.

Akizungumzia ushirika wa wakulima, Nganung’a amesema kuwa mwaka 2007 wakulima waliunda ushirika wa vijiji vya Lugolofu na Makungu ambao ni ushirika wa wamwagilia maji Mgololo. Amesema kuwa idara ya kilimo wilaya ya Mufindi iliwezesha mafunzo ya uundaji na uendeshaji wa ushirika huo na kufikisha wanachama 788. katika kuleta ufanisi kwa vitendo, wanachama 50 waliwezeshwa kutembelea skimu ya umwagiliaji ya Igomelo na Uturo zilizopo wilaya ya Mbalali mkoani Mbeya. 

Akielezea shughuli walizofanya wanachama, amesema kuwa walishiriki katika katika upandaji majani kuzunguka inteki, kupanga mawe chiin ya kibanio, kufyeka eneo lote la shamba kabla ya upimaji mifereji midogo ya ndani na kushiri katika uchimbaji wa mifereji midogo ndani.
=30=


 




Saturday, December 1, 2012

UMASIKINI CHANZO CHA UKIMWI IRINGA




Hali ya umasikini na mila potofu zimeendelea kuchangia katika maambukizi ya VVU na UKIMWI katika Mkoa wa Iringa na kusababisha madhara makubwa kuanzia ngazi ya familia.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa akipata maelezo ya shughuli zinazofanywa na AMREF katika banda lao katika uwanja wa RUCO.

 Mkuu wa Mkoa wa Iringa Dkt. Christine Ishengoma alipotembelea banda la Ushauri nasaha na kupima VVU.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma wakati wa maadhimisho ya siku ya UKIMWI Duniani katika Mkoa wa Iringa yalifanyika katika Chuo Kikuu kishiriki cha Ruaha.

Dkt. Christine amesema “hali ya maambukizi inatisha, madhara ya maambukizi ya VVU na UKIMWI ni makubwa hasa kutokana na sababu za umasikini, mila na desturi. Madhara haya ambayo huanzia katika ngazi ya familia, jamii na Taifa kwa ujumla ni pamoja na kuongezeka kwa idadi ya vifo vya watu ambao ni nguvu kazi ya Taifa la Tanzania”.

Amesema kuwa vifo vya wazazi husababisha kuongezeka kwa watoto yatima ambao wanahitaji msaada wa elimu, malazi, chakula na matibabu.

Katika kukabiliana na hali hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Iringa amesema kuwa Mkoa wake kwa kushirikiana na Halmashauri na mashirika yasiyo ya kiserikali wanatekeleza shughuli mbalimbali katika kukabiliana na kasi ya maambukizi ya VVU na UKIMWI.

Ameyataja maeneo maeneo ya ushirikiano kuwa ni katika kinga, huduma za kuzuia maambukizi mapya kwa watu ambao hawana maambukizi pamoja na wale wenye maambukizi kutokupata maambukizi mengine. Eneo lingine amelitaja kuwa ni tiba na huduma kwa walioathirika na janga la UKIMWI.

Dkt. Christine amesema kuwa katika kipindi cha kuanzia Julai 2011 hadi Juni 2012 jumla ya watu 130,882 walipata ushauri nasaha na kupima afya zao na kati yao 15,361 walikuwa na maambukizi ya VVU sawa na asilimia 10.5%.

Akiongelea utoaji wa huduma za upimaji wa VVU baada ya kushauriwa na mtoa huduma kwa mteja yoyote aendae hospitali akiwa anaumwa magonjwa mengine au kusindikiza, imesaidia sana kuwafanya watu wengi kujua hali ya afya zao kuhusiana na maambukizi ya VVU. Amesema katika jumla ya watu 23,184 waliopata huduma ya upimaji wa VVU baada ya kushauriwa na mtoa huduma,jumla ya watu 1,772 waligundulika kuwa na maambukizi ya VVU.

Aidha, huduma ya tohara kwa wanaume ni miongoni mwa njia zinazotumika katika kupunguza maambukizi ya VVU kwa wanaume.
Amesema kuwa huduma za tohara zimekuwa zikitolewa katika vituo vya huduma kama huduma ya kawaida. Mkuu wa Mkoa amesema “katika zoezi hilo jumla ya wanaume 113,076 wamekwisha tahiriwa katika mikoa ya Iringa na Njombe. Ili tohara kwa wanaume ilete mafanikio katika kupunguza maambukizi ya V.V.U., Mkoa unatarajia kutahiri jumla ya wanaume 264,990 ifikapo mwaka 2015”.

Wakati huohuo, Halmashauri ya Manispaa ya Iringa imetoa msaada wa zaidi ya shilingi milioni tano kwa vituo vinne vya watoto yatima leo. Akitoa maelezo ya msaada huo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Iringa, Theresia Mahongo amesema kuwa Manispaa ya Iringa inao utaratibu wa kutoa misaada mbalimbali kwa watoto yatima kulingana na majira na mahitaji. Miongoni mwa vitu vilivyotolewa kwa ajili ya watoto yatima ni pamoja na mchele, mafuta ya kupikia, maharage, unga, unga wa ngano, sabuni za kufulia na kuoga.
=30=

Friday, November 30, 2012

WAHASIBU WATAKIWA KUBADILIKA


Wahasibu nchini wametakiwa kubadilika na kuendana na mabadiliko ya kimfumo hasa imapoanzishwa kwa ajili ya kuboresha ufanisi wa kazi na kupunguza upotevu wa fedha za Serikali.

Waziri wa Fedha, Dkt. William Mgimwa
 
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Fedha, Dkt. William Mgimwa alipokuwa akiongea na maafisa wa Serikali Mkoani Iringa muda mfupi kabla ya kuhudhuria Mahafari ya Chuo kikuu cha Ruaha Iringa (RUCO).

Akifafanua kuhusu changamoto za mfumo wa Epicor 9.05 katika utekelezaji wa kazi za kihasibu na malipo, Dkt. Mgimwa ambae pia ni mbunge wa jimbo la Kalenga amesema kuwa lengo la Serikali kuanzisha mfumo huo ni kuhakikisha ufanisi katika matumizi ya fedha za serikali na kuondoa mianya ya upotevu wa fedha hizo. Amesema “tumekuwa na kipindi kifupi sana cha kuwawezesha wahasibu wetu juu ya kuutumia mfumo wa Epicor 9.05”. Akiufafanua mfumo huo, amesema kuwa mfumo huo ulianzia Marekani mwaka 1996 na kuanzishwa nchini kutokana na uwezoz wake wa kuchukua maagizo ya kimalipo kwa wingi, ukubwa, wepesi na haraka na sifa yake nyingine ni kukidhi viwango vya kihasibu vya kimataifa. Amesema kuwa mfumo huo pia unauwezo mkubwa wa kuhifadhi taarifa nyingi kwa wakati. 

Amesema kuwa ili kuweza kuenda vizuri na mfumo huo ni lazima wahasibu wakubali kubadilika na kuwa wepesi zaidi kuyakubali mabadiliko hayo.

Akiongelea uidhinishwaji wa fedha za miradi ya maendeleo ambao umekuwa ukilaumiwa sana kuwa umekuwa ukichelewa sana, Waziri wa Fedha amesema kuwa mchanganuo wa matumizi ya fedha za miradi ya maendeleo ni muhimu sana na ndio unaozingatiwa kabla ya kuidhinishwa malipo wengine ya miradi ya maendeleo. Amesema kuwa thamani ya fedha ni jambo linalopewa uzito katika miradi yote ya maendeleo ili fedha ya serikali inayotolewa iendane na mradi uliokusudiwa. Amesema kuwa changamoto iliyopo katika kodi ya Serikali ikihusishwa na miradi ya maendeleo, amesema “tunaruhusiwa kutoa asilimia tano tu iliyopatikana na kupeleka katika miradi ya maendeleo na asilimia nyingine inabaki kwa ajili ya kulipa mishahara na shughuli nyingine za uendeshaji wa Serikali” amesisitiza Dkt. Mgimwa.  

Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Nuhu Mwasumilwe ameelezea changamoto inayoukabili Mkoa wa Iringa kuwa ni ukomo wa bajeti hasa katika miradi ya maendeleo. Amesema kuwa katika miradi ya maendeleo fedha hizo zimepungua kutoka shilingi bilioni 1 hadi milioni 274. Ametolea mfano miradi inayoendelea kuwa ndiyo inayoathirika zaidi, kama ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Iringa mwaka 2012/2013 imetengewa shilingi milioni 51 tu kati ya milioni 700 zinazohitajika.

Aidha, Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Iringa ameiomba Hazina kuwa inatoa kipaumbele kwa miradi ya maendeleo inayoendelea. Akiongelea fedha za matumizi ya kawaida amesema kuwa kupungua kwa fedha hizo kumekuwa kukisababisha kutokueleweka katika maeneo mengine ikiwa ni pamoja na Ofisi za Wakuu wa Wilaya. Amesema mfano mwaka 2011/ 2012 fedha za matumizi mengine Mkoa ulipangiwa shilingi bilioni 2.7 ingawa hazikutolewa zote. Aidha, mwaka 2012/2013 Mkoa umepangiwa shilingi bilioni 1.9.

Nae Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma amempongeza Waziri wa Fedha kwa kuteuliwa kwake katika nafasi hiyo na kuomba ushirikiano wa viongozi na wadau wote katika kuwaletea wananchi maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
=30=