Monday, December 4, 2017

RAS WAMOJA AWATAKA WANAFUNZI WANUFAIKA WA TASAF KUSOMA KWA JUHUDI



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Wanafunzi wanufaika wa mpango wa kunusuru kaya masikini (TASAF) wametakiwa kusoma kwa juhudi na maarifa na kuacha utukutu ili wawe raia wenye mchango kwa Taifa lao.

Kauli hiyo ilitolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu alipofanya ziara ya kutembelea wanufaika wa TASAF kupitia elimu katika Manispaa ya Iringa.

Ayubu alisema “serikali tunategemea msome kwa bidii sana na msiwe watukutu. Nia ya serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dr. John Magufuli ni kujenga msingi imara kwa wananchi wake kupitia elimu. Tunataka kuwa na Taifa lenye wananchi wenye uwezo wa kufanya kazi na kujitegemea”. 

Alisema kuwa wanafunzi hao wamepata fursa ya kupata elimu bila malipo na fedha kupitia TASAF kwa ajili ya kununua mahitaji muhimu ya shule.

Katibu Tawala Mkoa, alisema kuwa wapo wazazi wanaozembea kuwanunulia watoto wao wanufaika wa TASAF wafuatiliwe ili waweze kutimiza wajibu huo. Alisema kuwa lengo la fedha hizo ni kuwawezesha watoto hao kupata sare za shule, madaftari, kalamu na mahitaji mengine muhimu ya shule. 

“Hapa lazima ifahamike kuwa, fedha hizi si za wazazi wla walezi, ni fedha kwa ajili ya kuwasaidia wanafunzi wanufaika kupata mahitaji yao ya lazima kwa ajili ya shule ili wasijisikie wanyonge pindi wanapokuwa shuleni” alisisitiza Ayubu.

Katibu Tawala Mkoa wa Iringa alifanya ziara maalum ya ufuatiliaji kwa wanafunzi wanufaika wa mpango wa TASAF kupitia elimu katika Manispaa ya Iringa kujifunza changamoto zinazowakabili. Katika ziara hiyo aliambatana na mratibu wa TASAF Mkoa, afisa mipango, mhasibu, mkaguzi wa ndani na afisa habari.
=30=

WANUFAIKA WA TASAF WATAKIWA KUZINGATIA LISHE



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Wanufaika wa mpango wa kunusuru kaya masikini mkoani Iringa wametakiwa kuzingatia suala la lishe wakati wanawake wanapokuwa wajawazito na wanapojifungua ili kuwa na watoto wenye hali nzuri ya lishe.

Kauli hiyo ilitolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu alipokuwa akiongea na wanufaika wa mpango wa TASAF na kamati ya usimamizi ngazi ya jamii alipotembelea wanufaika wa elimu wa mpango wa TASAF katika Kata ya Kitwiru Manispaa ya Iringa hivi karibuni.

Ayubu aliitaka kamati ya usimamizi ngazi ya jamii na serikali ya kijiji kuwasisitiza wanufaika waa TASAF wanapokuwa wajawazito kuhudhuria vituo vya afya ili kupewa elimu ya lishe. Alisema kuwa elimu ya lishe ni muhimu kwa makuzi ya mtoto tokea akiwa tumboni kwa mama yake. 

“Siku 1,000 ni muhimu sana kwa lishe katika mchango wa makuzi ya mtoto. Ukosefu wa lishe husababisha kutokuwa vizuri na kudumaa kiakili” alisema Ayubu. Alisema kuwa hali hiyo isipoangaliwa mapema inasababisha mzunguko wa umasikini katika familia na jamii kwa ujumla. Aliwasisitiza wanufaika wa fedha za kliniki kuhudhuria kliniki kwa sababu serikali imekopa fedha ili kunusuru wananchi wake katika suala la lishe.

Katibu Tawala Mkoa wa Iringa alifanya ziara maalum ya ufuatiliaji kwa wanafunzi wanufaika wa mpango wa TASAF kupitia elimu katika Manispaa ya Iringa kujifunza changamoto zinazowakabili. Katika ziara hiyo aliambatana na mratibu wa TASAF Mkoa, afisa mipango, mhasibu, mkaguzi wa ndani na afisa habari.
=30=

TASAF KUNUFAISHA WANAFUNZI KUSOMA KWA BIDII



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Mpango wa kunusuru kaya masikini (TASAF) una lenga kuhakikisha wanafunzi wanufaika wa mpango huo wanapata huduma za msingi zitakazowawezesha kusoma kwa bidii.

Kauli hiyo ilitolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu alipokuwa akiongea na wanafunzi wanufaika wa mpango wa TASAF kupitia elimu katika shule ya msingi Kibwabwa iliyopo Kata ya Kitwiru Manispaa ya Iringa hivi karibuni.

Ayubu alisema kuwa serikali kupitia TASAF imelenga kumuwezesha mtoto wa kitanzania kufikia malengo yake kupitia fursa ya elimu. Alisema kuwa kutokana na umuhimu wa elimu kwa wananchi, serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi wa Rais Dr. John Magufuli iliamua kutoa elimu bila malipo ili watoto wote wa kitanzania wapate fursa hiyo. 

“Kupitia mpango wa TASAF, serikali inatoa fedha ili wanafunzi wanaotoka katika kaya zisizo na uwezo waweze kugharamia mahitaji ya muhimu kwa mwanafunzi. Mahitaji hayo ni sare, viatu, madaftari, kalamu na masweta ili kujikinga na baridi” alisema Ayubu.

Wakati huohuo, Katibu Tawala Mkoa aliwashukuru kamati ya usimamizi ngazi ya jamii (CMC) kwa kazi nzuri kuwasimamia wanufaika katika kufikia malengo ya mpango wa TASAF. “Tuendelee kusimamia vizuri ili kuleta mafanikio yaliyokusudiwa. Lazima kuwakumbusha wanufaika kuwa pesa za TASAF si za burebure, serikali inaona wananchi wake wanakosa baadhi ya mahitaji ya msingi, hivyo fedha hiyo ni kwa ajili ya kusaidia kufikia mahitaji hayo” alisema Ayubu.

Katibu Tawala Mkoa wa Iringa alifanya ziara maalum ya ufuatiliaji kwa wanafunzi wanufaika wa mpango wa TASAF kupitia elimu katika Manispaa ya Iringa kujifunza changamoto zinazowakabili. Katika ziara hiyo aliambatana na mratibu wa TASAF Mkoa, afisa mipango, mhasibu, mkaguzi wa ndani na afisa habari.

MATUKIO KATIKA PICHA ZIARA YA KATIBU TAWALA MKOA KUTEMBELEA WANUFAIKA WA ELUMU KUPITIA TASAF

MATUKIO KATIKA PICHA ZIARA YA KATIBU TAWALA MKOA KUTEMBELEA WANUFAIKA WA ELUMU KUPITIA TASAF

Sunday, November 26, 2017

MATUKIO KATIKA PICHA MAHAFARI YA CHUO CHA VETA IRINGA

MATUKIO KATIKA PICHA MAHAFARI YA CHUO CHA VETA IRINGA

MATUKIO KATIKA PICHA UZINDUZI WA SIKU 16 ZA KUPINGA UKATILI WA KIJINSIA MKOANI IRINGA

VETA IRINGA WATAKIWA KUSIMAMIA MAFUNZO STADI KULINGANA NA UHITAJI WA SOKO LA AJIRA

VETA IRINGA WATAKIWA KUSIMAMIA MAFUNZO STADI KULINGANA NA UHITAJI WA SOKO LA AJIRA



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, IRINGA
Mamlaka ya elimu na mafunzo ya ufundi stadi imetakiwa kuendelea kusimamia na kuratibu mafunzo studi nchini ili mafunzo yanayotolewa yawe na ubora unaokidhi mahitaji ya soko la ajira.

Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Katibu Tawala Msaidizi- Mipango na Uratibu katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Nuhu Mwasumilwe katika mahafali ya 21 ya chuo cha mafunzo ya ufundi stadi na huduma Iringa yaliyofanyika katika viunga vya chuo cha VETA mjini Iringa.

Mkuu wa Mkoa alisema “kimsingi mamlaka ya elimu na mafunzo ya ufundi stadi bado ina kazi kubwa ya kusimamia, kuratibu, kugharamia, kutoa na kuendeleza mafunzo ya ufundi stadi nchini ili kufikia dhamira kuu ambayo ni kuhakikisha mafunzo yanayotolewa yanakuwa na ubora unaokidhi mahitaji ya soko la ajira”. Aidha, aliitaka mamlaka kuendelea kuboresha fani nyingine zinazohitaji maboresha makubwa kama karakana ya magari.

Akiongelea hitaji la wahitimu la kuunganishwa na fursa zinazohusu vijana ili kuwawezesha kuendana na mbadiliko ya teknolojia na soko la ajira, alisema kuwa sualaa hilo ni changamoto. “Suala hili ni changamoto kwa mamlaka, wazazi na hata wahitimu pia. Ninapenda kutumia mahafali haya kuwashauri wazazi kushiriki kikamilifu kuwasaidia ninyi katika hali ya mmoja mmoja, lakini nikishauri zaidi kwamba ninyi wahitimu kuunda na kusajili vikundi vyenye utaratibu mzuri wa usimamizi na uzalishaji wenye faida ambavyo vitaweza kuwapa fursa ya kupata mitaji kupitia taasisi mbalimbali za kifedha pamoja na mifuko ya vijana inayosimamiwa na halmashauri zetu” alisema mkuu wa Mkoa.

Akiongelea ombi la serikali kugharamia mafunzo ya vitendo, mkuu wa Mkoa alisema kuwa suala hilo linahitaji majadilianao na mamlaka husika. Aidha, aliwakumbusha wazazi kuwa wanawajibu wa kuwasaidia watoto wao kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Katika risala ya wahitimu wa chuo hicho iliyosomwa na Geofrey Simon ilieleza kuwa changamoto ni kutokuwa na walimu wa kutosha kukidhi mahitaji na uwiano sahihi katika kufundisha baadhi ya masomo. Alisema kuwa jambo hilo hupelekea walimu waliopo kuwa na mzigo mkubwa wa kufundisha idadi kuwa ya wanafunzi katika masomo ya hisabati, kiingereza, ujasiriamali na michoro ya maumbo. Changamoto nyingine ni chuo kukosa gari la kusafirishia wanafunzi waendapo kutembea maeneo ya mafunzo na michezo.

Simon aliongeza kuwa karakana nyingi za chuo zina vifaa na mitambo ya kufundishia iliyopitwa na wakati na kufanya mafunzo kutokidhi ubora wa soko la ajira. “Serikali kutokuwadhamini wanachuo fedha ya kufanya mafunzo ya vitendo, hivyo wazazi wengi kushindwa kumudu gharama husika imekuwa ni changamoto kubwa” alisema Simon.

Katika taarifa ya mkuu wa chuo cha mafunzo ya ufundi stadi na huduma iringa, Raphael Ng’wandu alisema kuwa chuo chake kimefanikiwa katika kugharamia mafunzo kwa wanafunzi wote waliodahiliwa. Alisema kuwa mamlaka imekuwa ikigharamia chakula na malazi kwa wanafunzi wanaokaa bweni.

Ng’wandu alisema kuwa chuo chake kinakabiliwa na changamoto ya kuwa na vifaa vya muda mrefu visivyoendana na teknolojia ya sasa. Alisema kuwa chuo chake kina mkakati wa kuboresha karakana za mafunzo kwa kununua vifaa vipya vya mafunzo vya kufundishia. Aidha, mamlaka imeendelea kuboresha bajeti ya mafunzo mwaka hadi mwaka.

Chuo cha mafunzo ya ufundi stadi cha Iringa kilianzishwa mwaka 1987 chini ya idara ya mafunzo na majaribio ya ufundi (NVTD) iliyokuwa chini ya wizara ya kazi. Fani za kwanza kutolewa zilikuwa ni uashi, bomba, useremala na umeme.  
=30=

JAMII YATAKIWA KUAMKA KUTETEA USAWA WA KIJINSIA



Na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa-Iringa
Wanawake na watoto wameendelea kuwa wahanga wa vitendo vya ukatili wa kijinsia na kukabiliwa na mgawanyo usio sawa wa rasilimali na madaraka kutokana na mwamko mdogo wa jamii kuhusu usawa wa kijinsia.

Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza katika hotuba yake ya uzinduzi wa kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia, uliofanyika ngazi ya mkoa katika halmashauri ya wilaya ya Kilolo na kusomwa kwa niaba yake na mganga mkuu wa mkoa Dr Robert Salim.

Mkuu wa Mkoa alisema “katika mkoa wetu wa Iringa, vitendo vya ukatili wa kijinsia vimekuwa vikifanyika katika maeneo mbalimbali, wanawake na watoto wamekuwa ndiyo wahanga wakubwa. Kwa mfano, wanawake wameendelea kukabiliwa na mgawanyo usio sawa wa rasilimali na madaraka kati yao na wanaume, kukosekana kwa usawa kunakichangiwa na mfumo dume uliopo katika jamii, wanawake kunyanyaswa, kubaguliwa, kupigwa, kutelekezwa na watoto, kutokushirikishwa katika maamuzi hata yale yanayohusu maisha yao”. 

Aliongeza kuwa watoto pia wamekuwa wakinyimwa haki zao za msingi katika jamii.

Mkuu wa mkoa alisema kuwa kumekuwa na matukio ya watoto kubakwa na kulawitiwa, mimba za utotoni, kupigwa na kuterekezwa. ”Idadi ya watoto waliofanyiwa ukatili wa aina tofauti kwa kipindi cha kuanzia Julai 2016- hadi Oktoba, 2017 imefikia watoto 606. Watoto 306 wameripotiwa kufanyiwa ukatili wa kingono na watoto 300 ukatili mwingine kama kupigwa na kadharika. Inashangaza kuona kwamba idadi kubwa ya vitendo vya ukatili dhidi ya watoto vimekuwa vikifanywa majumbani, shuleni au njiani, ukatili huu umekuwa ukifanywa na watu au ndugu wa karibu wa familia husika” alisisitiza Mkuu wa Mkoa.

Mkuu wa Mkoa alisema kuwa kwa kipindi cha miaka miwili, wanawake 904 wamefanyiwa ukatili. Ukatili huo umewaathiri kiafya, kijamii, kisaikolojia na kiuchumi. Ukatili wa kijinsia umekuwa ukichangia kuongezeka kwa maambukizi ya virusi vya ukimwi na magonjwa mengine yatokanayo na ngono.
 =30=