Sunday, April 22, 2018

RAS Iringa Netboli yaibugiza Ngorongoro Magoli 54-3



Timu ya Netiboli ya RAS Iringa imeiduwaza timu ya netiboli ya mamlaka ya hifadhi ya taifa ya Ngorongoro kwa kuibugiza magoli 54-3.

Katika mchezo ulioanza kwa kasi kubwa ilionekana dhahiri kabisa kuwa timu ya RAS Iringa imedhamiria kuibuka na ushindi ambapo dakika za mwanzo walionekana kuwapeleka kasi Ngorongoro jambo lilitotafsiriwa na wengi kuwa timu hiyo toka kaskazini mwa nchi ilipata hofu hata kabla ya mchezo.

Mchezo huo uliochezwa katika uwanja wa chuo kikuu cha kikatoliki cha Ruaha (RUCU) ulishuhuriwa na mamia ya wananchi wapenda michezo.

Baada ya mchezo huo, mratibu wa timu zote za RAS Iringa, Issa Matea alisema kuwa ushindi huo ni salamu za awali kwa timu pinzani. Akiongelea ushindi huo, alisema kuwa ni ushindi huo ni chachu na hamasa aliyoitoa katibu tawala mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu kwa timu hiyo yenye wanadada mahiri.
=30=

RAS Iringa yaiburuza 2-0 MUHAS Kamba



Timu ya kuvuta kamba ya RAS Iringa wanawake imeishinda timu ya kuvuta kamba ya MUHAS wanawake kwa mivuto 2-0. Katika mvutano wa aina yake uliofanyika katika uwanja wa shule ya msingi Mlandege na kushuhudiwa na mamia ya wapenda michezo wa mkoa wa Iringa na wageni kutoka sehemu mbalimbali waliofika mkoani hapa kwa ajili ya sherehe za Mei Mosi, 2018. 

Akiongea baada ya mvutano huo, Mratibu wa timu zote za RAS Iringa, Issa Matea alisema kuwa timu ya RAS Iringa maarufu kama Kisiki imepata ushindi huo kutokana na mshikamano na kujituma. Alitoa rai kwa timu washindani kuwa chonjo kwa sababu timu hiyo inalojukumu moja tu katika michezo hiyo. 

Alilitaja jukumu hilo kuwa ni kulinda heshima ya mkoa wa Iringa kwa kuibuka na ushindi katika mivuto yote katika michezo ya Mei Mosi, 2018.
=30=

Friday, April 20, 2018

Saratani ya Kizazi kuua Wanawake Iringa



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa
Saratani ya mlango wa kizazi imekuwa ikichangiwa na kujamiiana katika umri mdogo na kuwa na wapenzi wengi na kusababisha vifo vya wanawake wengi mkoani Iringa.

Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza alipokuwa akifungua mkutano wa wadau wa mapambano dhidi ya saratani ya mlango wa kizazi uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa chuo kikuu huria jana.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza

Masenza alisema kuwa saratani ya mlango wa kizazi inachangiwa na mambo mengi. “Saratani ya mlango wa kizazi inachangiwa na vitu vingi ikiwemo kuanza kujamiana katika umri mdogo, kuwa na wapenzi wengi, kuwa na ndoa za mitala, kuzaa watoto wengi, na uvutaji wa sigara” alisema Masenza.

Akiongelea dalili za saratani hiyo, alisema kuwa mara nyingi hujitokeza ikiwa imeshasambaa mwilini. Dalili hizo alizitaja kuwa ni kutokwa damu ya hedhi bila mpangilio pamoja na kutokwa damu baada ya kujamiana. Nyingine alizitaja kuwa ni maumivu ya mgongo, miguu na kiuno. Nyingine ni kuchoka, kupungua uzito, kupungukiwa au kokosa hamu ya kula, kutokwa uchafu wa rangi ya kahawia au wenye damu kwenye uke, maumivu ya miguu au kuvimba. 

“Dalili mbaya zaidi zinazoweza kujitokeza ni pamoja na kuishiwa damu, figo kushindwa kufanya kazi, kupatwa na fistula, na uvimbe wa tezi” alisisitiza Masenza.

Mkuu wa mkoa wa Iringa alielezea mkakati utakaotumika katika utoaji chanjo hiyo kuwa ni utaratibu wa kawaida katika vituo vya kutolea huduma za chanjo, baadhi ya shule zitachaguliwa na maeneo katika jamii na chanjo itatolewa kwa njia za huduma za mkoba.

Chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi itatolewa katika vituo vya kutolea huduma za afya vya serikali na binafsi bila malipo.
=30=

Monday, March 26, 2018

Viongozi Iringa kupunguza Maambukizi ya Kifua Kikuu-RC Masenza



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa
Viongozi mkoani Iringa wametakiwa kujipanga kuhakikisha maambukizi ya kifua kikuu yanapungua ili wananchi waweze kutekeleza shughuli za maendeleo.

Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza aliyekuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya siku ya kifua kikuu duniani yaliyofanyika ngazi ya mkoa katika mji wa Ilula wilayani Kilolo hivi karibuni.
 
Masenza alisema kuwa viongozi katika ngazi zao wanajukumu la kuhakikisha maambukizi ya kifua kikuu yanapungua katika jamii inayowazunguka ili jamii hiyo iweze kufanya kazi za kuzalisha mali. “Kwa hiyo katika vikao vyote vitakavyofanyika katika maeneo yetu ya kazi, katika ngazi zote kifua kikuu iwe ni agenda ili kuweza kupanga mikakati ya uboreshaji wa huduma za kifua kikuu” alisema Masenza. 

Aidha, alizitaka Halmashauri katika mkoa wa Iringa kupanga na kufanya shughuli za uchunguzi wa dalili za kifua kikuu katika makundi hatarishi. Aliyataja makundi hayo kuwa ni shule, magareza na maeneo yenye mikusanyiko mikubwa ya watu.

Mkuu wa mkoa alisema kuwa katika kuadhimisha juma la siku ya kifua kikuu duniani, katika eneo la Ilula Sokini, huduma mbalimbali zilikuwa zikitolewa kwa wananchi bila malipo. Huduma hizo alizitaja kuwa ni uchunguzi wa dalili za kifua kikuu na matibabu, upimaji wa maambukizi ya VVU, uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi, uchangiaji na utoaji wa damu, huduma ya uzazi wa mpango, elimu kuhusu lishe, na elimu kuhusu kifua kikuu.

Maadhimisho ya siku ya kifua kikuu duniani yamefanyika ngazi ya mkoa katika mji wa Ilula yakiongozwa na kaulimbiu isemayo ‘viongozi tuwe mstari wa mbele kuongoza mapambano ya kutokomeza kifua kikuu’.
=30=

SERIKALI KUENDELEZA BIASHARA NDOGO- RC MASENZA



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa
Serikali imeandaa mkakati wa kuendeleza biashara ndogo kwa lengo la kufikia uchumi unaotegemea viwanda ifikapo mwaka 2025.

Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza alipokuwa akifungua maonesho ya wajasiriamali wadogo na wa kati katika uwanja wa mashujaa mjini Mafinga jana.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza akikagua bidhaa katika Maonesho ya wajasiriamali mjini Mafinga

Masenza alisema kuwa katika nchini nyingi duniani, asilimia kubwa ya pato la watu binafsi linatokana na biashara ndogo na za kati. 

Hivyo kuendeleza sekta hii ni mkakati wa kutimiza  malengo ya dira ya maendeleo ya kuwa na uchumi imara unaotegemea  uzalishaji katika viwanda  ifikapo 2025” alisema Masenza. Aidha, aliwataka SIDO kuandaa mkakati wa kuwasaidia wajasiriamali waweze kupata masoko ya kudumu ndani na nje ya nchi.

Akiongelea changamoto ya uingizaji bidhaa kutoka nje, mkuu wa mkoa alisema kuwa uzalishaji wa bidhaa nyingi ndiyo suluhisho la kujitegemea kwa mkoa wa Iringa. Alisema kuwa uzalishaji huo utapunguza uagizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi na kuongeza matumizi ya malighafi zinazozalishwa ndani kutumika katika viwanda vya ndani. 

Utaratibu huu utasaidia kulinda viwanda vyetu wenyewe bila kutegemea masoko ya nje tu kwa baadhi ya malighafi zetu” alisema mkuu wa mkoa.

Katika kipindi hiki chenye changamoto za kiuchumi duniani tujitahidi kuzalisha bidhaa kwa wingi na zenye ubora wa hali ya juu ili kuongeza ajira na pato la Taifa. Wananchi wote, wafanyabiashara na viongozi mliobahatika kutembelea maonesho haya, hii ni fursa nzuri ya kuweka miadi na kununua au kuchangia mawazo yenu katika kuboresha bidhaa zetu za hapa nchini, ili kusaidia kujenge msingi imara wa viwanda na uchumi wetu” alisisitiza mkuu wa mkoa.

Maonesho ya wajasiriamali kwa mkoa wa Iringa ni ya kwanza ya aina yake yaliyoandaliwa na T-LED, SIDO, TCCIA, TWCC  kwa kushirikiana na Halmashauri ya mji wa Mafinga.
=30=