Sunday, August 12, 2012

DKT. ISHENGOMA AFUTURISHA MKOANI IRINGA



Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma amewaomba viongozi wa dini kuendelea kutoa elimu na hamasa kwa wananchi juu ya umuhimu wa zoezi la Sensa ya Watu na Makazi litakalofanyika nchi nzima kuanzia tarehe 26 Agosti, 2012.

Ameyasema hayo katika viwanja vya Ikulu Ndogo ya Iringa alipokuwa akitoa neno la shukrani kwa viongozi wa dini mbalimbali na wageni waalikwa katika futari aliyoiandaa kwa ajili yao kwa ajili ya kutakiana heri katika mfungo mtukufu wa Ramadhani.

Amesema viongozi hao wa madhehebu ya dini wanao wajibu na mchango mkubwa katika kuwahamasisha wananchi washiriki katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi ili kuhakikisha kuwa zoezi hilo linafanikiwa kwa maslahi ya nchi.

Dkt. Ishengoma amesema kuwa jukumu hilo linakuja kutokana na dhamana waliyonayo ya kuliwakilisha na kuliongoza kundi kubwa la waumini katika jamii. Amesema kutokana na umuhimu huo anawaomba viongozi hao washiriki kikamilifu ili Serikali iweze kupanga sawia mipango ya maendeleo. Amesema kuwa mipango ya maendeleo ili ifanikiwe takwimu za watu zinahitajika sana.

Akiongelea umuhimu wa zoezi hilo amesema kuwa zoezi hilo litaisaidia  Serikali kupanga mipango ikiwa na lengo la kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi wake. Amesema kujulikana kwa idadi hiyo ya watu ni muhimu kwa sababu kutaisaidia Serikali kuyatambua makundi mbalimbali ya watu katika jamii na kuwafikishia mahitaji yao maalumu ili waweze kufurahia uhuru wao katika nchi yao.

=30=


No comments:

Post a Comment