Thursday, February 13, 2014

MKOA WA SHINYANGA KUNUFAIKA NA KONGAMANO LA UWEKEZAJI KANDA YA ZIWA



Na. Magdalena Nkulu
 
Mkoa wa Shinyanga ni kati ya mikoa sita ya kanda ya Ziwa inayoshiriki katika kongamano la uwekezaji kanda ya ziwa litakalofanyika jijini Mwanza kuanzia tarehe 13-16 Februari 2014.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe.Ally N.Rufunga ametoa taarifa hiyo Jumanne ya wiki hii katika mkutano na waandishi wa Habari ofisini kwake.

Mhe.Rufunga amesema, kongamano la uwekezaji kanda ya Ziwa ni mkutano ulioandaliwa kwa ajili ya kutangaza fursa za uwekezaji na kuwashawishi wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuwekeza katika mikoa ya kanda ya Ziwa ambayo ni Mwanza,Shinyanga,Mara,Kagera,Geita na Simiyu.

Mkoa wa Shinyanga unashiriki kwenye kongamano hilo kwa sababu ya kutangaza fursa zilizopo katika mkoa ambazo ni

·        Mazingira mazuri yanayofaa kwa utalii na kilimo
·        Hali ya usalama na amani hivyo hali ya matukio ya uhalifu ni ndogo
·        Nguvu kazi ya kutosha
·        Uwepo wa taasisi mbalimbali za Elimu zinazotoa ujuzi tofauti
·        Miundombinu ya usafiri na usafirishaji kutokana na mkoa kuunganishwa na mikoa mingine ndani na nje ya nchi kama Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, na DRC.

Kutokana na kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo mkoani Shinyanga kupitia kongamano hilo,serikali inatarajia mafanikio makubwa ya kiuchumi na kijamii.
 Kupitia shughuli mbalimbali za uwekezaji katika viwanda za uzalishaji bidhaa, biashara, vyuo na taasisi wananchi wa mkoa wa Shinyanga na maeneo ya jirani wategemee kupata ajira, wataboresha na kuongeza thamani ya mazao ya mifugo na kilimo ili kuzalisha malighafi na fursa nyingi zitaongezeka.

Tayari mkoa wa Shinyanga imekwisha anza kunufaika na shughuli za uwekezaji wa viwanda ambavyo baadhi ya wawekezaji hasa wa nje ya nchi wamejenga na wameanza uzalishaji kama kiwanda cha ngozi (Ibadakuli),kiwanda cha kutengeneza nyuzi (Nhelegani),kiwanda cha mafuta ya kupikia (Nhelegani) na kiwanda cha mwekezaji mzawa cha Maji na soda cha “Jambo Group of Companies”.

Kongamano hili ni kutokana na mkakati wa serikali wa kukuza uchumi kupitia sekta ya uwekezaji hivyo ni muhimu kutangaza fursa zilizopo ili kuwavutia zaidi wawekezaji kuja katika mkoa wa Shinyanga.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Shinyanga

No comments:

Post a Comment