Thursday, February 13, 2014

SHULE BBINAFSI ZAPONGEZWA KUFANYA VIZURI KITAALUMA




Serikali imezipongeza shule zisizo za serikali kwa kufanya vizuri katika matokeo ya kitaifa kwa mitihani ya kuhitimu darasa la saba, kidato cha nne na sita kanda ya Nyasa.
 Gerald G. Guninita,

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Gerald Guninita katika ukumbi wa mikutano wa hoteli ya Kalenga mjini Iringa.

Dkt. Ishengoma amesema “niwapongeze sana kwa namna ya pekee kutokana na ukweli kwamba, ninyi mmekuwa ni mfano bora wa malezi ya mtoto wa kike kwani mara nyingi wanafunzi hufanya vizuri kitaifa katika matokeo ya mitihani ya kuhitimu darasa la saba, kidato cha nne na cha sita. Shule zisizo za serikali zinaongoza katika kufanya vizuri”. Amesema kwa matokeo haya inaonesha wazi mmejipanga vizuri kulisaidia taifa kutoa elimu yenye manufaa na tija kwa watanzania.

Amesema mafanikio hayo yanadhihirisha nia njema waliyonayo wamiliki wa shule binafsi katika kulielimisha na kuliendeleza taifa. Amepongeza juhudi za kukutana na kujadili na kupeana uzoefu na kubadilishana mbinu za ufundishaji katika kutoa elimu bora kwa wanafunzi.

Mkuu wa Mkoa amesema kuwa pamoja na kufanya vizuri kwa shule binafsi, zipo zinazofanya vibaya pia kutokana na wanafunzi wengi kutohudhuria masomo kwa kukosa ada, gharama kubwa ya masomo. Sababu nyingine amezitaja kuwa ni uhaba wa walimu kwa baadhi ya masomo, uongozi mbaya na migogoro katika shule pamoja na mambo mengine.

Akiongelea mikakati ya kuboresha elimu itolewayo nchini, amesema kuwa serikali imeamua kufanyia marekebisho sera ya elimu na mafunzo ya ufundi ya mwaka 1995. Amesema kuwa tayari kuna mambo mengi ambayo yamerekebishwa kwa lengo la kuendana na mahitaji ya utoaji wa elimu bora inayopatikana kwa wote.

Aidha, amewashauri kujenga vyuo vya ualimu na vyuo vingine ili kukidhi hitaji kubwa la walimu katika shule zote za serikali na binafsi na wataalamu wengine.
=30=

No comments:

Post a Comment