Wednesday, June 25, 2014

IRINGA DC YAKOPESHA VIJANA MIL 34



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Halmashauri ya wilaya ya Iringa imetoa mikopo ya zaidi ya shilingi milioni 34 kwa ajili ya kuviwezesha vikundi vya vijana vinavyojihusisha na ujasiliamali ili kuongeza mtaji na kujiletea maendeleo.
Kauli hiyo imetolewa na mkuu wa wilaya ya Iringa, Dkt. Leticia Warioba katika risala ya utii kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliyosomwa na Afisa Utumishi Mkuu wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru wilayani Iringa iliyosomwa katika eneo la Isimani tarafani wilayani Iringa.
Dkt. Warioba amesema “katika kipindi cha mwaka 2013/2014 halmashauri ya wilaya imetoa mikopo yenye jumla ya shilingi 34,500,000 kwa vikundi 18 vya ujasiliamali vya vijana”. Amesema kuwa halmashauri hiyo ina vikundi 177 vya vijana vyenye jumla ya wanachama 1,358 kati yao wanaume 825 na wanawake 531.
Akiongelea mikopo kwa vikundi vya wanawake, mkuu wa wilaya ya Iringa amesema “katika kipindi cha mwaka 2013/2014 halmashauri imetoa mikopo yenye jumla ya shilingi 74,950,000 kwa vikundi 50 vya ujasiliamali vya wanawake.
Kuhusu ujumbe wa Mwenge wa Uhuru, mkuu wa wilaya amesema kuwa ujumbe uliobebwa mwaka huu 2014 “katiba ni sheria kuu ya nchi” chini ya kauli mbiu isemayo ‘jitokeze kupiga kura ya maoni tupate katiba mpya’.
Amesema kuwa katika kutekeleza ujumbe huo wananchi na viongozi wa serikali, vyama vya siasa na madhehebu ya dini wameshiriki kikamilifu katika mchakato wa kupata katiba mpya kwa kupiga kura ya maoni kupitia mabaraza ya katiba yaliyoundwa katika halmashauri ya wilaya ya Iringa. Amesema kuwa wananchi wote walishiriki kikamilifu katika mchakato wa kupata katiba mpya. Amesema kuwa pamoja na wananchi kushiriki kupitia makundi mbalimbali serikali imeendelea kuwahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kwenda kupiga kura ya maoni ili kupata katiba mpya.
=30=








No comments:

Post a Comment