Wednesday, June 25, 2014

MWENGE KUTEKELEZA MIRADI YA BIL. 3.1



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Mwenge wa Uhuru kutekeleza miradi ya maendeleo yenye zaidi ya shilingi bilioni 3.1 katika siku nne za kukimbizwa kwake mkoani Iringa.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma alipowasilisha taarifa ya mkoa wa Iringa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa kupokea Mwenge wa Uhuru kutoka mkoa wa Morogoro leo.
Dkt. Ishengoma amesema Mwenge wa Uhuru katika Mkoa wa Iringa utaweka mawe ya msingi, utakagua, utazindua na kufungua jumla ya miradi ya maendeleo 42 yote ikiwa na thamani ya shillingi 3,109,958,020”.
Amesema kuwa kati ya fedha hizo serikali kuu imechangia shilingi 1,329,471,899, halmashauri za wilaya na manispaa shilingi 946,005,221. Amesema kuwa michango ya wananchi ni shilingi 500,877,000 na shilingi 333,603,900 ni michango ya wadau wa maendeleo.
Amesema kuwa Mwenge wa Uhuru ukiwa mkoani Iringa utakimbizwa katika halmashauri nne za Kilolo, Iringa, Manispaa ya Iringa na Mufindi. Amesema kuwa Mwenge huo utakimbizwa umbali wa kilometa 1,159 na kukabidhiwa mkoani Njombe tarehe 28 Juni, 2014.

Akiongelea ujumbe wa Mwenge wa Uhuru mwaka 2014, Dkt. Ishengoma ameutaja ujumbe huo kuwa ni “katiba ni sheria kuu ya nchi” wenye kaulimbiu ‘jitokeze kupiga kura ya maoni tupate katiba mpya’.
Akiongelea mchanganuo wa miradi hiyo, mkuu wa mkoa wa Iringa amesema kuwa jumla ya miradi 10 itafunguliwa, miradi 16 itazinduliwa, miradi 7 itawekwa mawe ya msingi na miradi 9 itakaguliwa. Ameitaja miradi hiyo kuwa inatokana na sekta za kilimo, ufugaji, maji, maliasili, ujenzi na barabara, afya, elimu na maendeleo ya jamii.
=30=



No comments:

Post a Comment