Friday, November 18, 2016

HOSPITALI YA RUFAA IRINGA YAVUKA LENGO UPIMAJI SUKARI


Na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa IRINGA
Kliniki maalumu ya kupima ugonjwa wa kisukari na shinikizo la damu mkoani Iringa imevuka lengo kwa kufanikiwa kupima wananchi zaidi ya 2,000.

Kauli hiyo ilitolewa na Mganga mkuu wa mkoa wa Iringa Dkt Robert Salim alipokuwa akiongea na waandishi wa habari katika hitimisho la siku tano za kliniki hiyo iliyofanyika katika viwanja vya bustani ya Manispaa mjini Iringa.

Dkt. Salim alisema “kliniki ya kupima ugonjwa wa kisukari na shinikizo la damu imefanikiwa kwa kiasi kikubwa. Tumefanikiwa kuwapima wananchi 2,007 na kuvuka lengo letu la kuwapima wananchi 2,000, hivyo lengo limefikiwa kwa asilimia 100.35”. Alisema kuwa mafanikio haya yanatokana na utayari wa wananchi wa mkoa wa Iringa kujitokeza kupima afya zao pindi fursa zinapojitokeza za upimaji zinapojitokeza.

Mganga mkuu wa mkoa aliwataka waratibu wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza katika halmashauri kuanzisha kliniki za magonjwa yasiyo ya kuambukiza katika halmashauri zao na kutoa huduma za mkoba. Aidha, liwataka kufikiria kuanzisha utaratibu wa kuwapima watumishi katika taasisi mbalimbali ili kuwapa fursa ya kunufaika na huduma za afya kwa magonjwa yasiyo ya kuambukiza.
Dkt Salim aliwatka wananchi wa mkoa wa Iringa kujikita katika kufanya mazoezi kama kutembea na kukimbia ili kujikinga na kisukari. Rai nyingine alitoa kuwa wananchi kuacha tabia ya kula vyakula vyenye mafuta, kupunguza unywaji wa pombe kupita kiasi na uvutaji wa sigara.
Akiongelea ufanisi wa kliniki hiyo, Dtk Tatu Mbotoni wa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Iringa alisema kuwa kliniki hiyo ilifanikiwa kutokana na timu yake ya wataalam kujipanga vizuri kuwahudumia wananchi wote waliojitokeza kwa muda. “Tulipanga timu ya wataalam wa kutosha kutoka hospitali ya rufaa ya mkoa na hospitali ya manispaa Frelimo.

Lengo la kuandaa wataalam wengi ni kuhakikisha kila mwananchi anayehudhuria anahudumiwa haraka sana ili aweze kuendelea na mjukumu yake tukizingatia matakwa ya serikali ya awamu ya tano ya hapa kazi tu’’ alisema Dkt Mbotoni.

Nae Elimina Sanga aliyefika katika kliniki hiyo, alisema ameridhishwa na huduma alizopata na kuomba kliniki hiyo iwe endelevu badala ya kusubiri kwenye maadhimisho ya siku ya kisukari duniani.
=30=  
 

No comments:

Post a Comment