Friday, November 18, 2016

MAKAMPUNI YA ULINZI YATAKIWA KUTUMIA WASTAAFU WA MAJESHI YA ULINZI


Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Makampuni ya ulinzi mkoani Iringa yametakiwa kuwatumia askari wastaafu kutoka majeshi ya ulinzi kwa mujibu wa sheria ili kunufaika na ujuzi walionao na kuimarisha usalama wa nchi.

Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza alipokuwa akifungua mkutano mkuu wa chama cha makampuni binafsi ya ulinzi mkoa wa Iringa (TSIA) kilichofanyika katika bwalo la Polisi mjini Iringa jana.

Masenza alisema “wito  wangu  kwenu  ni  kwamba  hakikisheni wasimamizi wa makampuni ya ulinzi wanakuwa wastaafu kutoka majeshi ya ulinzi kwa mujibu wa sheria. Wastaafu hawa wanauzoefu na ujuzi katika kusimamia masuala yote ya kiulinzi na usalama”. Aliongeza kuwa wastaafu hao wanauwezo wa kudhibiti nidhamu na kufundisha maadili mema kwa walinzi. 

Alisema kuwa walinzi wengi katika makampuni hayo wanakabiliwa na tatizo la nidhamu na maadili hivyo kuwatumia askari wastaafu kutawasaidia kuimarisha nidhamu na maadili kwa walinzi wa makampuni hayo.

Mkuu wa mkoa wa Iringa alipongeza juhudi zinazofanywa na makampuni ya ulinzi mkoani hapa. Alisema “mimi binafsi nichukue nafasi hii kutambua juhudi mbalimbali zinazofanywa na makampuni ya ulinzi katika kuimarisha hali ya amani miongoni mwa jamii na taasisi mbalimbali. Makampuni ya ulinzi yana mchango mkubwa katika kulinda mali za raia wa Tanzania. Pasingekuwepo makampuni haya vyombo vyetu vya ulinzi haviwezi kulinda peke yao kwa kuwa watanzania ni wengi na askari ni wachache lakini pia mali za watanzania ni nyingi na ukizingatia wahalifu wanaongezeka na kubuni mbinu mpya kila kukicha”

Mkuu wa mkoa wa Iringa ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya usalama ya mkoa aliagiza makampuni yote ya ulinzi mkoani Iringa kuhakikisha walinzi wake wote wanapitia mafunzo ya JKT au mgambo. “Walinzi wanapaswa kupitia mafunzo ya JKT au mgambo. Mafunzo haya huwajengea uwezo wa kupambana na majambazi, kuzuia matendo ya kihalifu na kulitumikia Taifa kizalendo” alisisiza mkuu wa mkoa. 

Awali afisa upelelezi mkoa wa Iringa, Deusdedit Kasindo waliwakumbusha wamiliki wa makampuni ya ulinzi kuwa ni wabia wa jeshi la Polisi kwa sababu wanafanya kazi zinazofanana za kulinda raia na mali zao. Alisisitiza kuwa viongozi wa makampuni hayo wanatakiwa kuwa na taaluma ya ulinzi na walinzi wao wanatakiwa kuwa na taaluma ya ulinzi.
Kasindo aliwakumbusha wamiliki wa makampuni ya ulinzi kuwa wanatakiwa kuwa na silaha mbili angalau tofauti na maeneo mengi ambayo walinzi wanakuwa na silaha moja jambo ambalo ni rahisi kuvamiwa. Aliwakumbusha kuwa kuazima silaha ni kosa kisheria. Aidha, aliwataka wamiliki wa makumpuni hayo kuhakikisha walinzi wao wanajua kutumia silaha kikamilifu.
=30=

No comments:

Post a Comment