Friday, November 18, 2016

WATAALAM IRINGA WATAKIWA KUBUNI JINSI YA KUWASAIDIA WANUFAIKA WA TASAF


Na. Mwandishi Maalumu, Iringa
Wataalam mkoani hapa wametakiwa kujikita katika kutafuta mbinu za kuwasaidia wanufaika wa mpango wa kunusuru kaya masikini Tasaf III ili wajikwamue katika lindi la umasikini.

Agizo hilo lilitolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu alipokuwa akifungua kikao kazi cha wataalam wa wilaya na mkoa wa Iringa cha kupanga mikakati ya jinsi ya kuzisaidia kaya masikini zinazonufaika na ruzuku ya Tasaf kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Bonde la Rufiji mjini Iringa.

Ayubu alisema “lengo la kikao kazi hiki ni kuwashirikisha ninyi wataalam wa sekta za afya, elimu, kilimo, mifugo, maendeleo ya jamii na ushirika ambazo kwa kiasi kikubwa zimeguswa na walengwa wa mpango huu wa Tasaf. Mnafahamu kuwa walengwa wengi wa Tasaf wapo vijijini na wameanzisha miradi midogomidogo ya ufugaji wa kuku, bata, simbilisi, nguruwe, mbuzi na kondoo. 

Aidha, wengine wanaboresha makazi yao, wote hawa wanahitaji msaada na ushauri wa kitaalam na ufuatiliaji wa karibu”. Aliongeza kuwa wataalam wa serikali wanawajibu wa kuwasaidia na kuwaelekeza wanufaika hao kuweza kufikia malengo yao. Aliwataka kuona kuwa kuwasaidia wanufaika hao ni jukumu lao na kuwataka kuweka katika mpango kazi wao na ratiba ya kazi ya kila mwezi.

Akiongelea wanufaika wanaopata ruzuku yenye masharti ya elimu na afya, Katibu Tawala Mkoa aliwataka kuwasimamia walengwa ili watimize masharti hayo. “Mfano, upande wa afya mlengwa atapata ruzuku kama ametimiza sharti la kupeleka mtoto kliniki aliye chini ya umri wa miaka mitano. Kwa upande wa elimu mlengwa atapata ruzuku kama atahakikisha mtoto wake anahudhuria shuleni siyo chini ya asilimia 80 ya mahudhurio yanayohitajika” alisisitiza Ayubu. Ni jukumu la kikao kazi hiki kujadili na kupanga namna bora ya kufanya ufuatiliaji wa karibu na kutoa ushauri kwa walengwa ili malengo ya serikali ya kupunguza umasikini yaweze kutimia. 

Awali Mratibu wa Tasaf Mkoa wa Iringa, William Kingazi alimtaarifu Katibu Tawala Mkoa kuwa mkoa wa Iringa ulipata fedha kupitia mpango wa Tasaf III kwa ajili ya kuziwezesha kaya masikini sana ili ziweze kujikimu. Mpango huo ulianza mwezi Januari, 2015 ambapo kaya 26,321 zilitambuliwa kuwa masikini sana. Hadi kufikia mwezi Septemba, 2016 mkoa ulipokea shilingi 6,525,080,001.
=30=

No comments:

Post a Comment