Wednesday, August 3, 2016

JAMII IMETAKIWA KUTUMIA CHUMVI YENYE MADINI JOTO KUEPUKA ULEMAVU



Na Mwandishi Maalum Mbeya

Jamii imetakiwa kutumia chumvi yenye madini joto ili kujenga ukuaji wa akili na kuepukana na ulemavu.

Kauli hiyo litolewa na Afisa Lishe Manispaa ya Iringa, Anzael Msigwa alipokuwa akifafanua umuhimu wa madini ya joto katika chumvi ya majumbani kwa wananchi waliotembelea banda la maonesho la Manispaa ya Iringa lililopo katika uwanja wa John Mwakangale jijini Mbeya.

Msigwa alisema “madini joto ni madini ambayo yanawekwa kwenye chumvi ili kuzuia ugonjwa wa tezi la shingo na kwa mama wajawazito madini hayo yanazuia baadhi ya ulemavu wa viungo kwa watoto. Madini joto yanasaidia ubongo wa mtoto akiwa tumboni kukua vizuri na kuzuia udumavu”.

Akiongelea umuhimu wa madini joto mwilini, Msigwa alisema kuwa madini joto yanahitajika kwa wingi wakati wa mabadiliko ya kimwili hasa kuvunja ungo, kubalehe na wakati wa ujauzito. Faida nyingine ya madini hayo ni kusaidia ukuaji wa mtoto aliye tumboni na ukuaji wa maendeleo yake baada ya kuzaliwa. Madini hayo pia husaidia ukuaji wa mwili na akili.

Afisa lishe huyo alisema kuwa kukosekana kwa madini joto mwilini, husababisha uvimbe wa tezi la shingo, ugumu katika kuelewa na kufundishika na kudumaa mwili na utaahira. Athari nyingine ni kuharibika kwa mimba na mtoto kuzaliwa akiwa na uzito pungufu na mtoto kuzaliwa akiwa na ulemavu wa viungo.

Alishauri kuwa chumvi inatakiwa kuhifadhiwa katika kasha kavu, lenye mfuniko na kuhifadhiwa mbali na joto.

Alisema kuwa kwa mujibu wa sheria ya chumvi ya mwaka 2010, inatoa idhini kwa maafisa wenye dhamana kukagua chumvi sehemu za kuhifadhi na kuuza chumvi.

=30=




No comments:

Post a Comment