Wednesday, August 3, 2016

WATEJA WA MAMLAKA YA MAJI MBEYA MJINI WATAKIWA KUWA WALINZI WA MIUNDOMBINU YA MAJI MBEYA



Na Mwandishi Maalum Mbeya

Wateja wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira mjini Mbeya wametakiwa kuwa walinzi wa miundombinu ya maji ili idumu na kuwanufaisha kwa muda mrefu zaidi.

Kauli hiyo ilitolewa na Afisa huduma kwa wateja wa Mamlaka ya majisafi na usafi wa mazingira mjini Mbeya, Hilda Nzary alipokuwa akielezea umuhimu wa mkataba wa huduma kwa mteja wa mamlaka hiyo katika viwanja vya Nanenane jijini Mbeya.
Afisa Huduma kwa Wateja, Hilda Nzary

Nzary alisema “kwa mujibu wa mkataba wa huduma kwa mteja, wajibu wa mteja ni kuzuia wizi, uharibifu mchepusho wa mita na vitendo vya rushwa ikiwa watumishi wa mamlaka wameomba”

Aliongeza kuwa mteja anawajibu wa kutoa taarifa kwa uongozi wa mamlaka juu ya vitendo vyovyote vinavyohatarisha usafi na usalama wa maji ili huduma hiyo iendelee kuwa salama kwa jamii nzima na kuwa endelevu. Mteja pia anawajibu wa kulipia huduma ya majisafi na majitaka na kutunza dira ya maji inayopima wingi wa maji yanayotumika.

Afisa huduma kwa wateja alisema kuwa, kwa wateja kutimiza wajibu huo, watarajie huduma bora ya uhakika na yenye ufanisi wa hali ya juu katika muda mfupi na kurejeshewa huduma ya maji katika muda usiozidi saa 24 baada ya kulipia ankara yake yote. Aliongeza kuwa mteja anayo haki ya kutoa taarifa kwa maandishi iwapo haridhiki na huduma anazopata.

Akiongelea ubora wa huduma zitolewazo na mamlaka hiyo, alisema kuwa mamlaka hiyo itahakikisha inaendelea kuimarisha viwango vya ubora wa huduma zinazotolewa kwa kupitia hali ya utendaji kila baada ya miezi mitatu. Mamlaka imeweka mtandao wa kukusanya habari kutoka kwa wateja wa ndani na wateja wa nje ili iweze kupata taarifa sahihi zitakazoisaidia kufanya maamuzi sahihi ya kuboresha huduma kwa wateja.

Mamlaka ya majisafi na usafi wa mazingira mjini Mbeya ilianzishwa mwaka 1998 kwa Sheria namba 8 ya Maji, ya mwaka 1997 kifungu 3(1) ikiwa inahudumia wateja 48,000.
=30=

No comments:

Post a Comment