Wednesday, August 3, 2016

NTINIKA ALITAKA JIJI MBEYA KUJIKITA KATIKA USAFI



Na Mwandishi Maalum Mbeya 

Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Paul Ntinika amelitaka jiji la Mbeya kujikita katika kudhibiti taka ili liwe jiji la mfano nchini kwa kuwahakikishia wakazi wake afya njema na usafi wa mazingira ili kuepukana na magonjwa.

Kauli hiyo aliitoa baada ya kufanya ziara ya kukagua hali ya usafi katika baadhi ya madampo ya taka jijini Mbeya leo asubuhi.

Katika ziara hiyo Ntinika aliyeambatana na Afisa Afya wa Jiji hilo na mjumbe wa kamati ya usalama ya Wilaya ya Mbeya alibaini uchafu uliotakapaa katika madampo ya taka katika shule za msingi za Manga, Sinde na Mbata zilizopo katikati ya jiji hilo. Katika maeneo yote hayo yaliyotembelewa makasha ya kuhifadhia taka yalikuwa yamejaa huku uchafu mwingine ulikuwa umetakapaa chini. Alimtaka Afisa Afya wa jiji hilo kuhakikisha uchafu huo unazolewa na kupelekwa katika dampo kubwa kwa ajili ya kuhifadhiwa ili wananchi waweze kutekeleza majukumu yao.

Ntinika alisema kuwa anataka jiji la Mbeya liwe la mfano katika usafi ili majiji mengine wajifunze kutoka hapo. Alisema usafi ni agenda yake ya mbele kwa sababu usafi utawafanya wananchi wa jiji hilo kuwa na afya njema na uhakika wa maisha marefu na kuepukana na magonjwa ya mlipuko.

Katika shule ya msingi Sinde iliyopo Kata ya Sinde jijini hapa, Semeni Kemendu, mwanafunzi wa darasa la saba alisema kuwa hali ya usafi katika dampo lililopo shuleni hapo imekuwa mbaya kwa kipindi kirefu. Alisema kuwa pembeni mwa dampo hilo kuna kina mama ntilie wanaopika chakula katika mazingira hayo machafu. Aliongeza kuwa kutokana na hali ya uchafu masomo kwa baadhi ya wanafunzi yamekuwa ya kusuasua. 

Mara nyingi wanafunzi huumwa tumbo na kulazimika kuomba ruhusa mara kwa mara” alisema Kemendu.

=30=

No comments:

Post a Comment