Wednesday, August 3, 2016

NTINIKA ATAKA ACB KUJITANGAZA



Na Mwandishi Maalum Mbeya 

Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Paul Ntinika ameitaka benki ya kibiashara ya Akiba (Akiba Commercial Bank) kujitangaza zaidi katika vyombo vya habari ili iweze kufahamika zaidi kwa wananchi.

Ushauri huyo aliutoa alipotembelea benki hiyo katika viwanja vya John Mwakangale katika maonesho ya Nanenane jijini Mbeya.

Ntinika alisema kuwa ili benki hiyo na huduma zake ziweze kufahamika zaidi kwa wananchi lazima benki hiyo itengeneze mkakati wa kujitangaza kwa wananchi kupitia vyombo vya habari. “Pamoja na huduma nzuri mnazozitoa lakini kama hamjitangazi si rahisi kwa wananchi kuwafahamu na kufahamu huduma zenu. Tumieni fursa hii ya maonesho ya kilimo Nanenane kujitanga zaidi na hasa kutangaza mipango yenu ya kumnufaisha mkulima pamoja na mambo mengine” alisema Ntinika.

Ntinika ambaye pia ni mtaalam mbobezi katika masuala ya fedha na ukaguzi wa mahesabu, alisema kuwa wananchi wengi hawana uelewa wa masuala ya kibenki hivyo kukosa huduma na fursa nyingi zinazopatikana kupitia taasisi za kifedha. Aliitaka benki hiyo kupanua wigo wake wa huduma ili kuwanufaisha wananchi wengi wa wilaya ya Mbeya.

Nae Afisa mikopo wa benki ya kibiashara ya Akiba, Anthony Kunambi alisema kuwa benki yake inalenga wajasiliamali wadogo na wa kati kwa kuwapa elimu ya ujasiliamali ili waweze kufanya kazi zao kwa tija na faida zaidi. Alisema kuwa miongoni mwa huduma wanazotoa ni pamoja na akaunti za amana, hundi, akaunti maalumu ya wafanyabiashara na huduma za kuwaleta karibu Vicoba na taasisi za kifedha na kuwaelimisha umuhimu wa Vicoba kutumia huduma za kibenki badala ya mfumo wa awali wa kujiwekea akiba majumbani.

Akiongelea jinsi benki yake inavyojishughulisha na kilimo, Kunambi alisema kuwa benki hiyo imekuwa ikitoa huduma ya mikopo kwa wakulima na wafugaji. 

Kwa mkoa wa Mbeya tumekuwa tukitoa mikopo kwa wafugaji wanaofuga kisasa lakini katika mkoa wa Arusha tumekuwa tukifanya kazi na wafugaji wanaofuga kizamani. Katika mkoa wa Arusha tumekuwa tukifadhili mradi wa kunenepesha ng’ombe na wanyama wamekuwa wakikatiwa bima ili kumhakikishia mfugaji uhakika kwa mifugo yake endapo janga litatokea”.

Sabina Stanley ambaye ni msimamizi wa mikopo wa benki hiyo tawi la Mbeya, alisema kuwa benki hiyo imaendelea na mradi wa majaribio katika sekta ya kilimo kwa kuanza na miradi michache katika mikoa ya Mbeya, Arusha na Dodoma. Alisema kuwa benki yake ilitoa mikopo kwa wakulima wa Litenga zaidi ya shilingi bilioni moja kwa vikundi 39 vya wakulima mwaka 2015. Nyingine ni mashine ya kukaushia kahawa yenye thamani ya dola za mimarekani 200 na kampuni ya Rogimwa iliyokopeshwa milioni 200.

Benki ya kibiashara ya Akiba (ACB) ina jumla ya matawi 18 kati ya matawi hayo, 13 yapo mkoani Dar es Salaam, wakati mikoa ya Mbeya, Mwanza, Arusha, Kilimanjaro na Dodoma ikiwa na tawi mojamoja.
=30=


No comments:

Post a Comment