Makete
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , Dk. Mohamed Gharib Bilal amewataka wanawake Mkoani Iringa kuhakikisha wanahudhuria kliniki tokea hatua za awali za ujauzito ili waweze kutapa huduma za kitaalamu mapema.
Kauli hiyo ameitoa katika eneo la Mfumbi wilayani Makete alipokuwa akisalimia wananchi wa wilaya ya hiyo baada ya kuweka jiwe la msingi soko lililojengwa kwa nguvu za wananchi na kupokea taarifa ya Mkoa na wilaya ya Makete alipowasili mkoani Iringa kuanza ziara yake ya siku tatu mkoani hapa akitokea mkoani Mbeya.
Dk. Bilal amewata mkoani hapa kuhudhuria kliniki ili kunufaika na huduma za afya na ushauri kwa wajawazito kutokana na serikali kuwekeza sana katika afya ya mama na mtoto.
Akiongelea maambukizi ya Ukimwi, Makamu wa Rais amesema kuwa taifa bado linakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo idadi ya maambukizi ya Ukimwi na kuitaka jamii kuwa makini zaidi na kujilinda. Vilevile, ameitaka jamii kuendelea kushirikiana na juhudi za serikali kupambana na maambukizi ili kupunguza idadi ya vifo nchini.
Katika taarifa ya maendeleo ya mkoa wa Iringa, iliyowasilishwa kwa Makamu wa Rais na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma, amesema kuwa mkoa umeongeza vituo vya kutolea huduma za Afya hadi kufikia 420 kwa lengo la kutoa huduma bora za afya kwa kuzingatia mahitaji ya makundi maalumuhasa watoto wachanga na walio na umri chini ya miaka mitano, wazee na wanawake walio katika uzazi.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa amesema kuwa katika kutekeleza sera ya zahanati kwa kila kijiji, mkoa umefikia asilimia asilimia 57 ya vijiji vyote kuwa na zahanati wakati asilimia 23 ya kata zote zina vituo vya afya.
Akiongelea huduma za mama wajawazito na watoto, Dk. Ishengoma amesema kuwa katika mwaka 2011 akina mama waliojifungulia kliniki walikuwa ni 54,356 sawa na asilimia 57.3 ya akina mama wajawazito waliotarajiwa kuhudhuria huduma za kliniki.
Amesema kuwa kiwango cha akina mama wajawazito waliojifungulia katika vituo vya tiba imefikia asilimia 76.2.
Amesema kuwa vifo vya wazazi vimepungua kutoka 162/100,000 mwaka 2010 hadi kufikia 138/100,000. Aidha, vifo vya watoto vimepungua kutoka 21/1,000 hadi 17/1,000.
Makamu wa Rais yupo katika ziara ya kikazi ya siku tatu mkoani Iringa.
=30=
MAKETE WATAKIWA KUKITUMIA CHUO CHA VETA
Makete
Wananchi wa Wilaya ya Makete wametakiwa kuonesha kuwa wapo tayari kukitumia chuo cha ufundi stadi VETA kwa kujipanga vizuri kukitumia na kukiendeleza chuo hicho ili kiweze kuwanufaisha wakazi wa wilaya ya Makete na taifa kwa ujumla.
Rai hiyo imetolewa na Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal wakati akizungumza na wakazi wa wilaya ya Makete baada ya kuweka jiwe la msingi ujenzi wa chuo cha ufundi stadi VETA wilayani hapa.
Dk. Bilal amesema kuwa “wilaya ya Makete tumepata fursa kubwa kuwa na VETA Makete” na kuutaka uongozi wa wilaya hiyo kujipanga vizuri kuonesha kuwa wao ni namba moja kwa kujenga uhusiano mzuri kati ya VETA Makete na mamlaka ya ufundi stadi nchini.
Amesema kuwa siku zote VETA lazima iwe karibu na jamii inayoihudumia kwa kutokuweka mwanya kati yake ili jamii inufaike na VETA na kinyume chake.
Makamu wa Rais ameutaka uongozi wa VETA wilaya ya Iringa kutafakari kwa kina kile kinachoitajika katika jamii hasa wakati uliopo sasa na kutoka na masuluhisho ya matatizo yaliyopo katika jamii.
Amesema kuwa ili wananchi wapige hatua hawana budi kukifahamu chuo cha VETA na matarajio yake katika kuihudumia jamii ili kuisaidia kupiga hatua ya kimaendeleo.
Aidha, amekitaka chuo hicho kutoa wanafunzi waliopikika na kuiva ili kukabiliana na ushindani uliopo katika soko na kuleta picha nzuri katika jamii. Amesema wakati mambo mengi yanakua kwa haraka, elimu ya ufundi stadi inatakiwa kupanuliwa zaidi kwa kuhusisha teknolojia ya habari kuwafikia watu wengine wali mbali zaidi na kuwafanya wanufaike na huduma hizo.
Katika taarifa ya Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugu amesema kuwa hivi karibuni nchi za afrika Masharki zitafungua milango yake itakayomtaka mtu mmoja kwenda kusaka ajira katika nchi nyingine. Amesema kwa muktadha huo “hatuna budi kuwaandaa vijana wetu katika elimu ya ufundi stadi ili wasiwe watazamaji”. Amesema kuwa serikali inaendelea na upanuaji wa mafunzo stadi ili kuwawezesha vijana wengi kujiunga na mafunzo hayo. Ameongeza kuwa serikali itaendelea kuongeza kasi ya ujenzi wa vyuo vya ufundi na kuboresha utoaji wa elimu bora ya mafunzo stadi nchini.
Chuo cha ufundi stadi VETA wilaya ya Makete ndicho chuo cha kwanza kwa mujibu wa sera ya chama tawala ya kujenga chuo cha VETA kila wilaya nchini na kinatajia kuanza mwezi Julai 2012 kwa kuanza na wanafunzi 160 katika fani za ujenzi, uashi, uselemala, ufundi wa magari.
=30=
KILIMO CHA MTAMA CHAHIMIZWA IRINGA
Makete
Mkoa wa Iringa unahimiza kilimo cha mtama, mihogo na mazao mengine yanayovumilia ukame ukiwa ni mkakati wa kukabiliana na hali ya ukame wa mara kwa mara unaosababisha upungufu wa chakula kwa baadhi ya maeneo mkoani hapa.
Katika taarifa ya maendeleo ya mkoa wa Iringa iliyowasilishwa kwa Makamu wa Rais, na Mkuu wa Mkoa wa Iringa Dk. Christine Ishengoma amesema kuwa ushauri wa kilimo cha mazao yanayovumilia ukame kama mtama, mhogo na mazao mengine umetolewa kwa Halmashauri zenye maeneo ya ukame ili kukabiliana na hali ya ukame wa mara kwa mara.
Amesema viongozi na wataalamu wa wilaya ya Iringa, Kilolo pamoja na Mkoa walitembelea kilimo cha mtama wilaya ya mpwapwa mwezi Mei, 2011 ili kujifunza uzalishaji wa zao la mtama ili waweze kuhimiza kilimo hicho maeneo yote yanayokabiliwa na ukame katika wilaya hizo.
Katika kuhakikisha hamasa inakuwepo katika kilimo hicho Mkuu wa Mkoa wa Iringa alifanya ziara katika wilaya hizo kuhimiza kilimo cha mazao yanayostahimili ukame ili kuzifanya kaya zinazokabiliwa na upungufu wa chakula kuwa na uhakika wa chakula.
Amesema kuwa kila mkulima amehimizwa kulima ekari mbili za mtama kwa lengo la kuwa na uhakika wa chakula. Amesema kuwa kila shule katika maeneo hayo imetakiwa kulima ekari mbili kwa ajili ya chakula cha wanafunzi wakati wa mchana.
Amesema kuwa viongozi wote kuanzia ngazi ya wilaya hadi kijiji nao wamelima ekari mbili za mtama kila mmoja na muitikio wa agizo hilo umepokelewa vizuri.
Akiongelea sekta ya afya, Mkuu wa Mkoa amesema kuwa hadi kufikia mwaka 2011 akina mama waliohudhuria kliniki ni 54,356 sawa na asilimia 57.3 ya akina mama wajawazito waliotarajiwa kuhudhuria huduma za kliniki. Aidha, amesema kuwa kiwango cha akina mama wajawazito waliojifungulia katika vituo vya tiba imefikia asilimia 76.2.
Amesema kuwa vifo vya wazazi vimepungua kutoka 162/100,000 katika mwaka 2010 hadi kufikia 138/100,000, wakati vifo vya watoto vimepungua kutoka 21/1,000 hadi kufikia 17/1,000.
Akiongelea hali ya maambukizi ya UKIMWI, Dk. Ishengoma amesema kuwa maambukizi yamefikia asilimia 15.7 na mkoa katika kukabiliana na hali hiyo mkoa uliandaa mpango wa miaka minne wa kupambana na maambukizi ya UKIMWI unaoendelea kutekelezwa. Amesema mpango huo ulioandaliwa na wadau wa sekta binafsi na umma ni wa kuanzia Oktoba 2008 hadi Septemba, 2012.
Katika salamu za Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal kwa wananchi wa Mfumbi wilaya ya Makete amesema kuwa taifa bado linakabiliwa na changamoto mbalimbali pamoja na idadi ya maambukizi ya UKIMWI na kuwataka wananchi kuwa makini zaidi na kujilinda. Amewataka kuendelea kushirikiana na serikali katika kuhubiri mapambano hayo ili kupunguza maambukizi.
Dk. Bilal pia amewataka akina mama wajawazito kuhudhuria kliniki mara kwa mara pindi wanapojigundua kuwa ni wajawazito ili waweze kunufaika na huduma hizo zinazotolewa kwa ajili yao .
Makamu wa Rais, anafanya ziara ya kikazi ya siku tatu mkoani Iringa katika wilaya za Makete, Njombe, Mufindi na Iringa na akiwa wilayani makete ameweka jiwe la msingi mradi wa soko lililojengwa kwa nguvu za wananchi katika kijiji cha Mfumbi, kuzindua nyumba ya walimu katika sekondari ya Kitulo na kuweka jiwe la msingi chuo cha VETA.
=30=