Tuesday, September 18, 2012

WIKI YA NENDA KWA USALAMA KITAIFA IRINGA

 Mwenyekiti wa Baraza la Nenda kwa Usalama Barabarani, Salim Abri na Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Gertrude Mpaka (kushoto) wakiwa katika wakati wa furaha ndani ya uwanja wa Samora yanapofanyika maonesho ya Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarari yanayofanyika kitaifa mkoani hapa.


 Maandamano ya wadau mbalimbali wakiingia katika uwanja wa Samora Manispaa ya Iringa kwenye Maonesho ya wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarari yanayofanyika kitaifa mkoani hapa.


 Bendi ikiongoza Maandamano ya wadau mbalimbali kuingia katika uwanja wa Samora Manispaa ya Iringa kwenye Maonesho ya wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarari yanayofanyika kitaifa mkoani hapa.

Picha ya pamoja ya wadau wa Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dkt. Emmanuel Nchimbi (wanne kulia waliokaa) na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma (wa tano kulia waliokaa) katika uwanja wa Samora Manispaa ya Iringa.


MITIHANI YA DARASA LA SABA KUANZA KESHO


Mikoa ya Iringa na Njombe imejipanga kuhakikisha kuwa mitihani ya kumaliza elimu ya msingi kwa mwaka 2012 inafanyika katika hali nzuri na kutokuruhusu mianya yoyote ya udanganyifu na kusababisha kufutiwa kwa matokeo kwa baina ya shule za msingi.

Akifafanua maandalizi ya mitihani hiyo ofisini kwake, Afisa Elimu Mkoa wa Iringa, Mwalimu Joseph Mnyikambi aliyepewa pia jukumu la kusimamia mitihani hiyo kwa mikoa ya Iringa na Njombe amesema kuwa tayari semina zimeendeshwa na kamati ya usimamizi wa mitihani ya mkoa katika Halmashauri zote nane za mikoa ya Iringa na Njombe. Amezitaja Halmashauri hizo kuwa ni Njombe, Mufindi, Makete, Ludewa, Kilolo, Iringa, Njombe Mji na Iringa Manispaa.

Akiongelea maandalizi amesema kuwa maandalizi yote yamekamilika na leo ndiyo siku ya kuwapeleka wasimamizi katika vituo vyao ya kusimamia mitihani hiyo. Amesema “kwa mujibu wa sheria zetu huwezi kumwambia msimamizi atasimamia wapi mtihani huo”. Amesema kuwa lengo ni kuzuia udanganyifu na hongo kutoka kwa jamii kwenda kwa msimamizi na kutoka kwa msimamizi kwenda kwa jamii pamoja na wanafunzi.

Kuhusu taratibu, Mwalimu Mnyikambi amesema kuwa taratibu ni za kawaida na zilizozoeleka isipokuwa kitu kipya ni mwaka huu watahiniwa wote watatumia penseli na fomu maalumu kujibu mitihani hiyo kwa kusiliba kwa sababu kwa mara ya kwanza itatumika teknolojia mpya ya ‘optical mark reader’ (OMR). Amesema kuwa majibu yatasahihishwa kwa kutumia kompyuta.

Amesema kuwa mitihani hiyo itafanyika kwa siku mbili na itaanza kesho tarehe 19 -20 Septemb, 2012. masomo yatakayotahiniwa ameyataja kuwa ni Sayansi, Hisabati na Kiswahili. Mengine ni Kiingereza na Maarifa ya Jamii.

Ni kwa namna gani mkoa umejipanga kukabiliana na udanganyifu unaoweza kusababisha wanafunzi kufutiwa matokea, Afisa elimu mkoa wa Iringa amesema “kama mkoa tumejipanga vizuri kuhakikisha kuwa udanganyifu haufanyiki katika mikoa ya Iringa na Njombe kwa kuzingatia taratibu zote za mitihani”. Ameitaja miongoni mwa mikakati hiyo kuwa ni pamoja na kila mwanafunzi kukaa katika dawati lake na kukaa mmoja ili kuondoa uwezekano wa kutizamiana. Amesema katika semina kwa wasimamizi wa mitihani, msisitizo ulikuwa ni kuhakikisha hakuna udanganyifu wowote utakaopewa nafasi katika mtihani huo ili kuhakikisha kila mwanafunzi anayeingia kidato cha kwanza anajua kusoma na kuandika na anakwenda kwa kufaulu vizuri.

Mwalimu Mnyikambi ameitaja idadi ya wanafunzi watakaofanya mitihani hiyo ya kumaliza elimu ya msingi kwa mikoa ya Iringa na Njombe kuwa ni 43,499 kati yao wasichana ni 23,015 na wavulana ni 20,484. amesema jumla ya shule zote ni 887.
=30=

AJALI ZA BARABARANI ZAENDELEA KUUA NCHINI


Ajali za barabarani zimeendelea kupoteza maisha ya wananchi ambapo zaidi ya abiria 4,500 wamefariki na wengine wakipata ulemavu wa kudumu nchini.

Akihutubia wananchi katika Manispaa ya Iringa, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dkt. Emmanuel Nchimbi aliyemuwakilisha Rais katika ufunguzi wa maadhimisho ya wiki ya nenda kwa usalama barabarani yanayofanyika kitaifa mkoani Iringa, amesema kuwa takwimu za ajali  zinazotolewa na jeshi la polisi zinaonesha kuwa kwa karibu miaka mitano kuanzia mwaka 2008 hadi Juni, 2012 vifo vya abilia vimefikia 4,532 wakati vifo vya watembea kwa miguu vilivyotokana na ajali za barabarani vilifikia 5,117. Ameseam kuwa vifo vya wapanda pikipiki ni 2,414 wakati wapanda baiskeli ni 2,171.
 Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dkt. Emmanuel Nchimbi (kulia) alipotembelea banda la Jeshi la Polisi katika Maonesho ya wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarari yanayofanyika kitaifa katika uwanja wa Samora Manispaa ya Iringa.


Picha ya pamoja ya wadau wa Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dkt. Emmanuel Nchimbi (wanne kulia waliokaa) na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma (wa tano kulia waliokaa) katika uwanja wa Samora Manispaa ya Iringa.

Amesema kuwa madareva wa magari na pikipiki wamekuwa ni sehemu Kubwa ya vyanzo vya ajali kutokana na kutokuzingatia mambo mbalimbali. Ameyataja mambo hayo kuwa ni kuendesha kwa mwendo kasi usioruhusiwa kisheria na kuyapita magari yaliyopo mbele bila ya kuchukua tahadhari. Mambo mengine ameyataja kuwa ni kutokuheshimu alama na ishara za barabarani na kuendesha magari mabovu. Amesema mambo mengine ni kwa wapanda pikipiki kutokuvaa kofia ngumu na kuendesha gari au pikipiki bila leseni.

Nae Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usalama barabarani, Pereira Silima amewataka wananchi kuwa na muamko mkubwa katika kutembelea mabanda katika maonesho yanayoendelea katika uwanja wa Samora ya Wiki ya nenda kwa usalama barabarani ili kuweza kujifunza na kuuliza maswali juu ya masuala yote yanayohusiana na Wiki ya nenda kwa usalama barabarani.

Akiongelea mikakati ya kupunguza ajali za barabarani, Silima ameitaja kuwa ni pamoja na askari kutoe elimu juu ya usalama barabarani katika shule za msingi na sekondari ili kuwajengea wananfunzi uelewa mkubwa juu na dhana nzima ya usalama barabarani. Amesema kuwa kila anayeomba leseni ya udereva ni lazima awe amesomea udereva huo katika chuo kinachotambulika na serikali. Mkakati mwingine ameutaja kuwa ni kuhakikisha kuwa mabasi ya masafa marefu yanakuwa na  madereva wawili ili kusaidiana katika kazi hiyo. Amesema mkakati mwingine ni kuwashirikisha wananchi katika Kutoa taarifa mbalimbali dhidi ya watu wanaovunja taratibu za usalama barabarani ili waweze kuchukuliwa hatua mapema kabla ya kusababisha maafa.

Nae Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma katika salamu zake amesema kuwa Mkoa wa Iringa una mtandao wa jumla ya kilometa 8,051.20 za barabara. Amesema mtandao huo ni chachu na kichocheo kikubwa cha maendeleo katika mkoa huo. Amesema kuwa vyombo vya dola vinafanya kazi ya kuhakikisha usalama barabarani unaimarishwa ili wananchi waweze kutumia barabara hizo vizuri kwa lengo la kujiletea maendeleo.

Dkt. Christine amesema kuwa hivi karibuni Serikali imefanikiwa kufanya matengenezo makubwa ya barabara ta Tanzam kwa urefu wa kilometa 150 kwa gharama ya shilingi bilioni 127.7. amesema matengenezo hayo yameleta matokeo ya kupungua kwa gharama ya usafirishaji kwa kupunguza uharibifu wa magari kutokana na mashimo yaliyokuwepo awali.

Ámesema kuwa changamoto Kubwa ni ajali barabarani kutokana na kuboreshwa kwa barabara kwa sababu magari hienda kasi zaidi. Amesema pamoja na changamoto hiyo wadau wote wakijipanga vizuri inaweza kukabiliwa.

Maadhimisho ya Wiki ya nenda kwa usalama barabarani yanafanyika kitaifa mkoani Iringa na yalianza kuadhimishwa nchini tokea mwaka 1994. Maadhimisho ya mwaka 2012 yanaongozwa na kaulimbiu isemayo ‘pambana na ajali za barabarani kwa vitendo, zingatia sheria’ yatafikia kilele chake tarehe 22 Septemba, 2012 na maonesho mbalimbali ya shughuli zinazoendana na Wiki hii yanaendelea katika uwanja wa kumbukumbu ya Samora katika Manispaa ya Iringa
=30=