Mkuu wa Mkoa wa Iringa amewataka wananchi kuachana na tabia ya kukwepa kulipa kodi na kuwa wazalendo kwa mkoa wao na Taifa lao kwa ujumla wakati akikemea tabia ya wafanyabiashara wanaokwepa kutumia mashine za kieletroni za kutolea risiti.
Mkuu wa Mkoa amesema hayo katika hotuba yake kwenye
maadhimisho ya siku ya mlipakodi iliyofanyika katika ukumbi wa chuo kikuu huria
tawi la Iringa iliyosomwa kwa niaba yake na Mkuu wa Wilaya ya Iringa Dkt.
Leticia Warioba.
Dkt. Warioba amesema “bado wapo walipakodi ambao sio
wazalendo.Walipakodi ambao mpaka sasa wanakwepa kodi. Tabia hii ya kukwepa kodi
siyo ya kizalendo na ningependa kuwaasa muiache mara moja”. Amesema kuwa
ukadiliaji na ukusanyaji wa kodi vinafanyika kwa mujibu wa sheria za kodi na ni
muhimu kwa kila mlipa kodi kuheshimu sheria na taratibu nchi ilizojiwekea.
Amesema tabia ya kukwepa kodi imekuwa ikiwafanya
wafanyabiashara kupitisha bidhaa vichochoroni badala ya kupitisha bidhaa hizo
kwenye ofisi za forodha zilizopo mipakani. Amesema kuwa utaratibu huo
unafanyika kinyume na sheria za nchi na kutaka tabia hiyo iachwe mara moja.
Akiongelea matumizi ya mashine ya kieletroniki za
kutolea risiti, Dkt. Leticia amesema “matumizi ya mashine hizo ni changamoto
katika utendaji kazi wa Mamlaka ya Mapato nchini, ningependa kuwafahamisha
kuwa, matumizi ya mashine hizi ni agizo la Serikali na lengo lake ni
kuhakikisha kodi ya ongezeko la thamani inakusanywa ipasanyo”.
Amewataka wale wote waliosajiliwa na kodi ya ongezeko
la thamani kutumia mashine za kieletroniki za kutolea risiti kwa kila mauzo
wanayofanya. Amesema kuwa mashine hizo zinatumika kwa mujibu wa sheria ya bunge
hivyo utekelezaji wake ni lazima.
Wakati huohuo,
Mamlaka ya Mapato Mkoa wa Iringa imefanikiwa kuvuka lengo kwa kukusanya zaidi
ya asilimia 100 ya lengo iliyowekewa la idara ya ushuru wa forodha na kodi za
ndani. Katika maelezo ya Meneja wa mamlaka ya mapata Mkoa wa Iringa, Rozalia
Mwenda amesema kuwa kwa mwaka wa fedha 2011/2012 Mkoa wa Iringa ulipangiwa
kukusanya jumla ya shilingi 23,761,800,000/= lengo la idara ya ushuru wa forodha likiwa shilingi
110,100,000/= na lengo la idara ya kodi za ndani likiwa shilingi
23,651,700,000/=. Amesema
kwa kipindi hicho Mkoa ulikusanya shilingi 24,730,752,185 sawa na asilimia 105
ya utendaji.
Akiongelea ubora wa huduma
kwa wateja, Rozalia amesema “mamlaka ya
mapato makao makuu, mikoani hadi wilayani, inatekeleza sera ya ubora ambayo
inaelekeza utendaji kazi wenye lengo la kutoa huduma bora inayokidhi na hata
kupita matarajio ya mteja”. Amesema “baada ya kufanyika kwa ukaguzi wa ubora wa huduma zetu na
kampuni ya wakaguzi wa nje, mamlaka ilitunukiwa cheti cha kimataifa cha ubora
wa viwango cha ISO 9001:2008”. Amesema kuwa mamlaka yake imepanga kutathmini
mara kwa mara viwango vya huduma tunazotoa kwa walipa kodi ili kuhakikisha kuwa
mahitaji ya walipakodi yanazingatiwa katika mipango ya mamlaka ya kimkakati.
Amesema kuwa mamlaka yake
inaendeleza ushirikiano baina yake na mlipakodi kwa lengo la kudumisha ushirikiano wa kulipa kodi kwa mujibu wa
sheria kwa kutoa huduma bora. Amesisitiza kuwa urafiki baina mamlaka na
mlipakodi sharti uongeze tija katika kukusanya mapato ya Serikali kwa lengo la
kutokumuumiza mlipa kodi na wala Serikali.
Meneja
wa mamlaka ya mapato mkoa wa Iringa ameahidi kuongeza juhudi katika utendaji
kazi, amesema “mimi na wafanyakazi wa mamlaka
ya mapato Mkoa wa Iringa tunaahidi kuongeza, juhudi, maarifa na uadilifu katika
kuhakikisha tunavuka malengo tuliyopangiwa kama tulivyokwishaonesha kipindi
kilichopita. Kwa mshikamano na mikakati tuliyonayo, tunaamini malengo ya mwaka
2012/2013 ambayo ni shilingi 33.4 bilioni yanafikiwa”.
Wiki ya maadhimisho ya 6 ya
sherehe ya mlipakodi kitaifa ilianza tarehe 01-07 Novemba, 20122 ikiongozwa na
kaulimbiu isemayo “ulipaji kodi wa
hiari Kwa Taifa lenye mafanikio” ikiwa na lengo kuu la kuboresha huduma kwa
mlipakodi.
=30=