Na.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Serikali inatambua
na kuthamini mchango unaotolewa na wadau wa maendeleo katika kuongezea mahali
ambapo serikali inaishia katika kuwahudumia wananchi.
Kauli hiyo
ilitolewa na mwakilishi wa mganga mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dr Atupele Mwandiga
alipokuwa akifunga kikao cha kuutambulisha mradi wa ‘USAID Tulonge Afya’
kilichofanyika katika ukumbi wa hoteli ya Gentle Hills mjini Iringa jana.
Dr Mwandiga alisema
kuwa wadau wa maedeleo wamekuwa msaada mkubwa katika kuchangia juhudi za
serikali za kuwaletea maendeleo wananchi wake.
“Wadau wa maendeleo wamekuwa wakitoa mchango mkubwa sana katika
kuwaletea maendeleo na kuboresha afya za wananchi wetu. Uwepo wenu katika Mkoa
huu umeongeza kasi ya serikali ya Mkoa na Halmashauri zake ya kuwafikia
wananchi katika jitihada zao mbalimbali za kukabiliana na changamoto za maisha,
hasa kujikwamua kiuchumi na kuimarisha afya zao” alisema Dr Mwandiga.
Dr Mwandiga
aliwapongeza waandaaji wa mradi huo kwa kuchagua kutumia mbinu za mabadiliko ya
tabia kwa wanajamii (SBCC). Alisema kuwa mbinu hiyo imekuwa ikitoa matokeo
chanya inapotumika vizuri.
Dr Mwandiga
aliwaagiza waganga wakuu wa Wilaya kusimamia vizuri na kutoa ushirikiano katika
utekelezaji wa mradi huo kupitia mbinu za mabadiliko ya tabia kwa wanajamii.
=30=