Monday, June 23, 2014

IRINGA WATAKIWA KUKIMBIZA MWENGE KWA UTULIVU



Na. Dajari Mgidange, IRINGA

Wananchi wametakiwa kujitokeza kwa wingi kuulaki Mwenge wa Uhuru katika maeneo mbalimbali utakayokimbizwa mkoani Iringa.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya mapokezi ya Mwenge wa Uhuru mkoani Iringa mwaka 2014 ofisini kwake leo.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma

Waandishi wa Habari wa Mkoa wa Iringa
Dkt. Ishengoma amesema kuwa ni vizuri wananchi wakajitokeza kwa wingi kuulaki Mwenge wa Uhuru pindi utakapopita katika maeneo yao. Amesema “ninawasihi wananchi kuendela kudumisha amani na utulivu wakati wote ambapo Mwenge wa Uhuru utakuwa ukikimbizwa katika mkoa wetu na hata baada ya kuhitimisha mbio hizo katika mkoa wetu”.
Akiongelea uhamasishaji katika halmashauri, Mkuu wa Mkoa amesema “ninapenda kutumia fursa hii kuviomba vyombo vya habari na ninyi waandishi wa habari kuwahamasishwa wananchi katika halmashauri zote za Mkoa wa Iringa kujitokeza kwa wingi kuulaki Mwenge wa Uhuru katika maeneo yote ambako utapita, kushiriki katika mikesha ya Mwenge pamoja na kupokea ujumbe wa Mwenge wa Uhuru wa mwaka huu 2014”.
Amesema kuwa Mwenge wa Uhuru ukiwa katika Mkoa wa Iringa utakagua, kuweka mawe ya msingi, kufungua na kuzindua jumla ya miradi ya maendeleo 42 yenye thamani ya Tsh. 3,109,958,020/=. Amesema kuwa Mwenge wa Uhuru utatoa ujumbe katika maeneo yote ambako utakimbizwa. Ameitaja miradi itakayotembelewa na Mwenge wa Uhuru kuwa ni miradi ya barabara, elimu, afya, kilimo na ufugaji. Miradi mengine ameitaja kuwa ni miradi ya vijana na wanawake na hifadhi ya mazingira.
Mwenge wa Uhuru mwaka 2014 unaongozwa na ujumbe usemao “katiba ni sheria kuu ya nchi’’ wenye kauli mbiu isemayo ’ jitokeze kupiga kura ya maoni tupate katiba mpya’.
=30=

TAARIFA YA MHE.DR CHRISTINE G. ISHENGOMA, MKUU WA MKOA WA IRINGA KWA WAANDISHI WA HABARI KUHUSU MAANDALIZI YA KUUPOKEA MWENGE WA UHURU KIMKOA TAREHE 23 JUNI, 2014



Ndugu Waandishi wa Habari,
Mkoa utapokea Mwenge wa Uhuru kutoka Mkoa wa Morogoro tarehe 24 Juni 2014. Makabidhiano yatafanyika katika kijiji cha Ruaha Mbuyuni kuanzia saa 2.00 hadi saa 3.00 asubuhi.

Maeneo ambako Mwenge utakimbizwa
Baada ya kuupokea Mwenge wa Uhuru kutoka Mkoa wa Morogoro Mkuu wa Mkoa wa Iringa atamkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Kilolo ili aanze kuukimbiza katika Wilaya yake. Ukitoka Wilaya ya Kilolo Mwenge wa Uhuru utakimbizwa Katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa tarehe 25 Juni, 2014, Manispaa ya Iringa utakimbizwa tarehe 26 Juni, 2014 na Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi utakimbizwa tarehe 27 Juni, 2014 kuanzia saa 2.00 hadi saa 3.00 asubuhi.

Ndugu Waandishi wa Habari,
Baada ya Mwenge wa Uhuru kukimbizwa katika Mkoa wa Iringa utakabidhiwa kwa Mkoa wa Njombe tarehe 28 Juni, 2014.

Ndugu Waandishi wa Habari,
Mwenge wa Uhuru ukiwa katika Mkoa wa Iringa utafanya shughuli za kukagua Miradi ya Maendeleo, kuweka mawe ya msingi, kufufungua na kuzindua jumla ya Miradi ya Maendeleo 42 yenye thamani ya Tsh. 3,109,958,020/=
Aidha, Mwenge wa Uhuru utatoa ujumbe katika maeneo yote ambako utakimbizwa. Miradi ambayo itatembelewa na Mwenge wa Uhuru ni miradi ya Barabara, Miradi ya Elimu, Miradi ya Afya, Miradi ya Kilimo na ufugaji, Miradi ya Vijana na wanawake na Miradi ya Hifadhi ya Mazingira.

Ndugu Waandishi wa Habari,
Kila mwaka Mwenge wa Uhuru hubeba ujumbe maalumu ambao hukusudiwa kuwasilishwa kwa wananchi kuhusu jambo muhimu linalohusu Taifa katika wakati uliopo. Ujumbe maalumu wa Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2014 unasema: ‘’katiba ni Sheria kuu ya Nchi’’ wenye kauli Mbiu’ jitokeze kupiga kura ya maoni tupate katiba mpya. Sambamba na ujumbe maalumu, Mwenge wa Uhuru kila huwa unatoa elimu na kuhamasisha wananchi kupambana na maadui watatu wa maendeleo ambao ni Rushwa, Matumizi ya Dawa za Kulevya na ugonjwa wa UKIMWI.

Ndugu Waandishi wa Habari,
Ninapenda kutumia fursa hii kuviomba vyombo vya habari na ninyi waandishi wa habari kuwahamasishwa wananchi katika Halmashauri zote za Mkoa wa Iringa kujitokeza kwa wingi kuulaki Mwenge wa Uhuru katika maeneo yote ambako utapita, kushiriki katika mikesha ya Mwenge pamoja na kupokea ujumbe wa Mwenge wa Uhuru wa mwaka huu 2014.

Ndugu Waandishi wa Habari,
Ninawasihi wananchi kuendelea kudumisha amani na utulivu wakati wote ambapo Mwenge wa Uhuru utakuwa ukikimbizwa katika Mkoa wetu na hata baada ya kuhitimisha Mbio za Mwenge katika Mkoa wetu.

Ahsanteni sana kwa kunisikiliza.

MWENGE WA UHURU OYEEE!
IRINGA OYEEE!