Sunday, November 26, 2017
MATUKIO KATIKA PICHA MAHAFARI YA CHUO CHA VETA IRINGA
MATUKIO KATIKA PICHA MAHAFARI YA CHUO CHA VETA IRINGA
MATUKIO KATIKA PICHA UZINDUZI WA SIKU 16 ZA KUPINGA UKATILI WA KIJINSIA MKOANI IRINGA
VETA IRINGA WATAKIWA KUSIMAMIA MAFUNZO
STADI KULINGANA NA UHITAJI WA SOKO LA AJIRA
VETA IRINGA WATAKIWA KUSIMAMIA MAFUNZO STADI KULINGANA NA UHITAJI WA SOKO LA AJIRA
Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, IRINGA
Mamlaka
ya elimu na mafunzo ya ufundi stadi imetakiwa kuendelea kusimamia na kuratibu
mafunzo studi nchini ili mafunzo yanayotolewa yawe na ubora unaokidhi mahitaji
ya soko la ajira.
Kauli
hiyo ilitolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza katika hotuba yake
iliyosomwa kwa niaba yake na Katibu Tawala Msaidizi- Mipango na Uratibu katika
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Nuhu Mwasumilwe katika mahafali ya 21 ya chuo
cha mafunzo ya ufundi stadi na huduma Iringa yaliyofanyika katika viunga vya
chuo cha VETA mjini Iringa.
Mkuu
wa Mkoa alisema “kimsingi mamlaka ya
elimu na mafunzo ya ufundi stadi bado ina kazi kubwa ya kusimamia, kuratibu,
kugharamia, kutoa na kuendeleza mafunzo ya ufundi stadi nchini ili kufikia dhamira
kuu ambayo ni kuhakikisha mafunzo yanayotolewa yanakuwa na ubora unaokidhi
mahitaji ya soko la ajira”. Aidha, aliitaka mamlaka kuendelea kuboresha
fani nyingine zinazohitaji maboresha makubwa kama karakana ya magari.
Akiongelea
hitaji la wahitimu la kuunganishwa na fursa zinazohusu vijana ili kuwawezesha
kuendana na mbadiliko ya teknolojia na soko la ajira, alisema kuwa sualaa hilo
ni changamoto. “Suala hili ni changamoto
kwa mamlaka, wazazi na hata wahitimu pia. Ninapenda kutumia mahafali haya
kuwashauri wazazi kushiriki kikamilifu kuwasaidia ninyi katika hali ya mmoja
mmoja, lakini nikishauri zaidi kwamba ninyi wahitimu kuunda na kusajili vikundi
vyenye utaratibu mzuri wa usimamizi na uzalishaji wenye faida ambavyo vitaweza
kuwapa fursa ya kupata mitaji kupitia taasisi mbalimbali za kifedha pamoja na
mifuko ya vijana inayosimamiwa na halmashauri zetu” alisema mkuu wa Mkoa.
Akiongelea
ombi la serikali kugharamia mafunzo ya vitendo, mkuu wa Mkoa alisema kuwa suala
hilo linahitaji majadilianao na mamlaka husika. Aidha, aliwakumbusha wazazi
kuwa wanawajibu wa kuwasaidia watoto wao kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Katika
risala ya wahitimu wa chuo hicho iliyosomwa na Geofrey Simon ilieleza kuwa
changamoto ni kutokuwa na walimu wa kutosha kukidhi mahitaji na uwiano sahihi
katika kufundisha baadhi ya masomo. Alisema kuwa jambo hilo hupelekea walimu
waliopo kuwa na mzigo mkubwa wa kufundisha idadi kuwa ya wanafunzi katika
masomo ya hisabati, kiingereza, ujasiriamali na michoro ya maumbo. Changamoto
nyingine ni chuo kukosa gari la kusafirishia wanafunzi waendapo kutembea maeneo
ya mafunzo na michezo.
Simon
aliongeza kuwa karakana nyingi za chuo zina vifaa na mitambo ya kufundishia
iliyopitwa na wakati na kufanya mafunzo kutokidhi ubora wa soko la ajira. “Serikali kutokuwadhamini wanachuo fedha ya
kufanya mafunzo ya vitendo, hivyo wazazi wengi kushindwa kumudu gharama husika
imekuwa ni changamoto kubwa” alisema Simon.
Katika
taarifa ya mkuu wa chuo cha mafunzo ya ufundi stadi na huduma iringa, Raphael
Ng’wandu alisema kuwa chuo chake kimefanikiwa katika kugharamia mafunzo kwa
wanafunzi wote waliodahiliwa. Alisema kuwa mamlaka imekuwa ikigharamia chakula
na malazi kwa wanafunzi wanaokaa bweni.
Ng’wandu
alisema kuwa chuo chake kinakabiliwa na changamoto ya kuwa na vifaa vya muda
mrefu visivyoendana na teknolojia ya sasa. Alisema kuwa chuo chake kina mkakati
wa kuboresha karakana za mafunzo kwa kununua vifaa vipya vya mafunzo vya
kufundishia. Aidha, mamlaka imeendelea kuboresha bajeti ya mafunzo mwaka hadi
mwaka.
Chuo
cha mafunzo ya ufundi stadi cha Iringa kilianzishwa mwaka 1987 chini ya idara
ya mafunzo na majaribio ya ufundi (NVTD) iliyokuwa chini ya wizara ya kazi.
Fani za kwanza kutolewa zilikuwa ni uashi, bomba, useremala na umeme.
=30=
JAMII YATAKIWA KUAMKA KUTETEA USAWA WA KIJINSIA
Na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa-Iringa
Wanawake
na watoto wameendelea kuwa wahanga wa vitendo vya ukatili wa kijinsia na
kukabiliwa na mgawanyo usio sawa wa rasilimali na madaraka kutokana na mwamko
mdogo wa jamii kuhusu usawa wa kijinsia.
Kauli
hiyo ilitolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza katika hotuba yake ya
uzinduzi wa kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia, uliofanyika
ngazi ya mkoa katika halmashauri ya wilaya ya Kilolo na kusomwa kwa niaba yake
na mganga mkuu wa mkoa Dr Robert Salim.
Mkuu
wa Mkoa alisema “katika mkoa wetu wa
Iringa, vitendo vya ukatili wa kijinsia vimekuwa vikifanyika katika maeneo
mbalimbali, wanawake na watoto wamekuwa ndiyo wahanga wakubwa. Kwa mfano,
wanawake wameendelea kukabiliwa na mgawanyo usio sawa wa rasilimali na madaraka
kati yao na wanaume, kukosekana kwa usawa kunakichangiwa na mfumo dume uliopo
katika jamii, wanawake kunyanyaswa, kubaguliwa, kupigwa, kutelekezwa na watoto,
kutokushirikishwa katika maamuzi hata yale yanayohusu maisha yao”.
Aliongeza
kuwa watoto pia wamekuwa wakinyimwa haki zao za msingi katika jamii.
Mkuu
wa mkoa alisema kuwa kumekuwa na matukio ya watoto kubakwa na kulawitiwa, mimba
za utotoni, kupigwa na kuterekezwa. ”Idadi
ya watoto waliofanyiwa ukatili wa aina tofauti kwa kipindi cha kuanzia Julai
2016- hadi Oktoba, 2017 imefikia watoto 606. Watoto 306 wameripotiwa kufanyiwa
ukatili wa kingono na watoto 300 ukatili mwingine kama kupigwa na kadharika.
Inashangaza kuona kwamba idadi kubwa ya vitendo vya ukatili dhidi ya watoto
vimekuwa vikifanywa majumbani, shuleni au njiani, ukatili huu umekuwa ukifanywa
na watu au ndugu wa karibu wa familia husika” alisisitiza Mkuu wa Mkoa.
Mkuu
wa Mkoa alisema kuwa kwa kipindi cha miaka miwili, wanawake 904 wamefanyiwa
ukatili. Ukatili huo umewaathiri kiafya, kijamii, kisaikolojia na kiuchumi.
Ukatili wa kijinsia umekuwa ukichangia kuongezeka kwa maambukizi ya virusi vya
ukimwi na magonjwa mengine yatokanayo na ngono.
=30=
TANZANIA MSTARI WA MBELE KUPINGA UBAGUZI KWA WATOTO NA WANAWAKE
Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa-IRINGA
Tanzania
ipo mstari wa mbele katika kuheshimu haki na utu wa mwanamke kwa kutekeleza
mkataba wa umoja wa mataifa wa kupinga aina zote za ubaguzi dhidi ya watoto na
wanawake.
Kauli
hiyo ilitolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu katika maelezo
yake wakati wa uzinduzi wa kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia uliyofanyika
ngazi ya mkoa katika halmashauri ya Wilaya ya Kilolo na kusomwa na Afisa
maendeleo ya jamii katika Ofisi ya mkuu wa mkoa, Saida Mgeni.
Katibu
Tawala Mkoa alisema kuwa nchi ya Tanzania ipo mstari wa mbele katika kuheshimu
haki na utu wa mwanamke kwa kutekeleza mkataba wa umoja wa mataifa wa kupinga
aina zote za ubaguzi dhidi ya wanawake na watoto ambao Tanzania imeusaini na
kuuridhia.
Serikali kwa kushirikiana na wanasiasa, viongozi wa dini, mashirika
ya hiyari na watu binafsi wamekuwa wakitumia kampeni hii kuhamasisha jamii kwa
lengo la kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto.
Alisema kuwa maadhimisho haya yalenge kutafakari mafanikio na changamoto
zinazoikabili jamii na kuandaa mkakati wa kukabiliana na vitendo vya ukatili wa
kijinsia.
Katibu
Tawala Mkoa alisema kuwa kwa kipindi cha miaka miwili kuanzia Januari
2016-septemba, 2017, wanawake 904 wamefanyiwa ukatili wa aina moja au nyingine.
Aliongeza kuwa ukatili wa kijinsia unachangia maongezeko ya maambukizi ya
virusi vya ukimwi.
“Mkoa wa Iringa ni
miongoni mwa mikoa yenye kiwngo kikubwa cha mambukizi ya vvu. Watu wenye umri
wa miaka 15-49 ambao ni asilimia 9.1 na maambukizi ya wanawake ni asilimia 10.2
ikilinganishwa na asilimia 6.9 ya wanaume. Kitaifa ni asilimia 5.1 ambapo
wanawake ni asilimia 6.3 na wanaume asilimia 3.5” alisisitiza Katibu Tawala
Mkoa.
Kampeni
ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia ilizinduliwa ngazi ya Mkoa, katika Kijiji
cha Lyasa, Kata ya Image Wilaya ya Kilolo chini ya kaulimbiu ya isemayo ‘funguka!
Ukatili dhidi ya wanawake na watoto haumuachi mtu salama chukua hatua’.
=30=
Subscribe to:
Posts (Atom)