Washarika wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, usharika
wa Iringa Mjini wametakiwa kushiriki kikamilifu katika mchakato wa mabadiliko
ya uundwaji wa Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kufanikisha
uundwaji wa Katiba hiyo kwa kujumuisha mapendekezo ya watu wengi zaidi.
Wito huo umetolewa na mgeni rasmi Dkt. Christine Ishengoma
katika harambee ya uchangiaji wa ujenzi wa kanisa kuu la mtaa wa Wilolesi
iliyofantik Katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzanaia, Usharika wa Iringa
Mjini leo.
Dkt. Christine ambae pia ni Mkuu wa Mkoa wa Iringa, amesema “ndugu
zangu Washarika natoa rai kwenu kushiriki kikamilifu katika kuhamasisha na
kuwaeleza waumini wengine na wananchi kwa ujumla ili washiriki katika mchakato
huu kwa kutoa elimu na hamasa”. Amesema “napenda kutoa wito kwenu wote kuwa
huru kutoa maoni yenu Tume itakapopita katika maeneo na kukusanya maoni
yenu”.
Amesema kuwa baadhi ya wananchi wanalalamika kuwa Katiba ya sasa
inamapungufu kadhaa, hivyo huu ndio wakati wao wa kutoa maoni yao ili hayo mapungufu
yaweze kufanyiwa kazi na kuingia katika Katiba mpya. Amesema hili litafanikiwa
pale tu, washarika na wananchi watakapojitokeza kwa wingi kutoa maoni yao pindi
tume ya kukusanya maoni itakapopita katika maeneo yao. Amewataka kuwa makini
katika kusikiliza tarehe na sehemu ambazo mikutano hiyo itakuwa ikifanyika ili
waweze kuwasilisha maoni yao kwa tume hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa amewataka wananchi kuwa huru katika kutoa
maoni yao na kuwahakikishia kuwa ukusanyaji wa maoni hayo hauhusiani na itikadi
yoyote. Amesema ili Katiba hiyo mpya iwe ya mafanikio ni lazima maoni ya
wananchi wengi yaweze kukusanywa na mafanikio hayo yanatokana tu, na wananchi
kujitokeza kwa wingi kutoa maoni yao kwa tume hiyo.
=30=