Serikali mkoani Iringa imetaka jamii ishirikishwe ipasavyo
juu ya dhana ya utunzani wa barabara ili kuhakikisha barabara zinadumu na
kupitika muda wote.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt.
Christine Ishengoma wakati akifungua kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa wa
Iringa (RCC) kilichofanyika katika ukumbi wa Siasa ni Kilimo mjini Iringa.
Dkt. Christine amesema “katika kuhakikisha tunakuwa na
barabara zinazopitika muda wote, nimeona mapungufu ya ushiriki wa jamii juu ya
utunzaji wa barabara hizo. Wananchi wamekuwa wakifanya shughuli ndani ya
hifadhi ya barabara na kuacha uchafu kwenye barabara na uchafu huo kuziba
mifereji na kuharibu barabara”. Aidha, amewataka wajumbe wa kikao hicho kutoa
elimu kwa wananchi ili washiriki kikamilifu katika utunzaji wa barabara hizo
ili ziweze kudumu na kuwahudumia kwa muda mrefu. Amesema kuwa uchafu unaharibu
mazingira, unaziba mifereji ya barabara na kusababisha mafuriko kwenye makazi
ya wananchi.
Mkuu wa mkoa wa Iringa ametoa rai kwa viongozi na wananchi
kushirikiana na miradi ya ujenzi na ukarabati wa barabara ya Iringa –Dodoma na
Iringa-Mafinga. Amesema kuwa ushirikiano huo na elimu kwa wananchi utasaidia
kukomesha hujuma za wizi hasa wa mafuta na ementi ili miradi hiyo iweze kuwa ya
manufaa kwa mkoa wa Iringa na taifa kwa ujumla na kukamilika kwa muda muafaka.
Aidha, amewataka wajumbe hao kuendela kushirikiana katika
kutoa elimu kwa wananchi juu ya Sheria mpya ya hifadhi ya barabara ambayo ni
mita 30 kil upande kutoka katikati ya barabara. Amesema “wananchi waendelee
kuelimishwa juu ya umuhimu wake kwani wanapojenga na kubomolewa nyumba zao
haipendezi. Inawagharimu na kuwaumiza sana” alisisitiza Mkuu wa mkoa wa Iringa.
=30=