Saturday, September 4, 2010

wanafunzi 45,104 kufanya mtihani wa darasa la Saba Iringa

Jumla ya wanafunzi 45,104 wanatarajiwa kufanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi (PSLE) mwaka huu 2010 mkoa ni Iringa imeelezwa.


Mwl. Leonard Msigwa, Afisa Elimu Takwimu Mkoa wa Iringa


Takwimu hizo zimetolewa na Afisa Elimu –Taaluma wa mkoa wa Iringa, Ndg. Leonard Msigwa katika mahojiano maalumu na mwandishi wa habari hii ofisini kwake leo.


Ndg. Msigwa amesema “wanafunzi wanaotarajia kumaliza elimu ya msingi katika mkoa wa Iringa jumla yao ni 45,104”. Ameongeza kuwa kati yao wasichana ni 23,620 na wavulana ni 21,484.


Afisa Elimu taaluma amesema kuwa mkoa unao wanafunzi wasioona 13 wanaotumia maandishi ya vinundu na kati yao 8 ni wavulana na 5 ni wasichana. Amezitaja shule wanazosoma kuwa ni shule ya msingi Mwaya katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo (wanafunzi 3) na Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi (wanafunzi 10). Aidha ameongeza kuwa mkoa unao wanafunzi wenye uoni hafifu 20 katika shule 8 tofauti na kati yao wasichana ni 10 na wavulana ni 10. ameongeza kuwa Halmashauri ya Manispaa ina shule 3 zenye wanafunzi (13), Halmashauri ya Wilaya ya Makete wanashule 2 zenye wanafunzi (4), Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi wanashule 2 zenye wananfunzi (2) na Njombe Mji wanashule 1 yenye mwanafunzi (1).


Kwa upande wa maandalizi amesema kuwa maandalizi yote yamekamilika na kusema “mitihani yote imekamilika kadri ya mahitaji na kuna ziada ya bahasha zaidi ya 70 kwa kila somo”. Aidha zoezi la kusambaza mitihani hiyo kwa kila Halmashauri limekamilika jana jioni.


Ndg. Msigwa ameongeza kuwa elimu imetolewa kwa maafisa elimu wa wilaya zote za mkoa wa Iringa na kuapishwa kwa Maafisa Elimu msingi, Maafisa Elimu sekondari na wataaluma wote wa msingi na sekondari juu ya kutunza mitihani, pia wasimamizi watakao kuwa madarasani wote wataapishwa.


Kuhusu wizi na uvujaji wa mihihani amesema kuwa umefanyika mchakato makini wa kuwapata watu waadilifu kwa kushirikiana na usalama wa taifa na makamanda wa polisi wa wilaya zote. “Wasimamizi wazembe wote wamezuiliwa kusimamia sababu kumbukumbu zao zipo wazi” amesisitiza.


Mkoa wa Iringa una jumla ya shule za msingi 850 na mtihani wa kumaliza elimu ya msingi (PSLE) mwaka 2010 utaanza tarehe 6 Septemba, 2010 kwa masomo ya Sayansi, Hisabati na Kiswahili na kuendelea siku ta tarehe 7 Septemba, 2010 kwa masomo ya Kiingeleza na Maarifa ya Jamii.