Thursday, March 26, 2015

MYUYU AWATAKA WATENDAJI WA KATA KUOMARISHA MAWASILIANO IRINGA



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Uimarishaji wa mawasiliano baina ya watendaji wa kata na maafisa tarafa umeelezwa kuwa ni nyenzo muhimu katika utekelezaji wa kazi za serikali.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Tawala Msaidizi, Sehemu ya Menejimenti ya Serikali za Mitaa, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Bw. Wilfred Myuyu alipokuwa akiwasilisha mada kuhusu majukumu ya watendaji wa kata katika usimamizi wa shughuli mbalimbali za maendeleo wilayani Kilolo.

Bw. Myuyu amesema kuwa katika kutekeleza majukumu, mtendaji wa kata anatakiwa kuwasiliana mara kwa mara na afisa tarafa. Amesema kuwa kwa mujibu wa miongozo ya mawasiliano serikalini, afisa tarafa anajukumu la kusimamia watendaji wa kata ili watekeleze majukumu yao ipasavyo. Amesema kuwa kwa mujibu wa sheria ya Tawala za Mikoa Na. 19 ya mwaka 1997 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2006 inaweka wazi kuwa majukumu ya afisa tafara ni kusimamia shughuli za watendaji wa kata, vijiji na mitaa katika eneo lake.

Akiongelea majukumu ya watendaji wa kata katika ujenzi wa maabara unaoendelea, Bw. Myuyu amesema kuwa watendaji wa kata wanawajibu wa kuwatambua wadau mbalimbali wa maendeleo wanaoweza kuchangia na kuwahamasisha kwenye shughuli za ujenzi wa maabara ikiwa ni pamoja na wananchi. Ameongeza kuwa wanalo jukumu la kufanya ufuatiliaji na tathmini ya ujenzi unaoendelea ili kujiridhisha na uzingatiwaji wa viwango kusudiwa pamoja na kasi ya ujenzi. Amesema kuwa katika ufuatiliaji huo wanalojukumu la kufahamu changamoto zilizopo kushauri na kuzipatia ufumbuzi.

Jukumu linguine amelitaja kuwa ni kuhakikisha michango inayotolewa na wananchi na wadau inatumika kwa kuzingatia taratibu zinazoongoza matumizi ya fedha za umma na kutoa taarifa ya matumizi ya fedha hizo kwa wananchi.    

Bw. Myuyu ameongeza kuwa jukumu lingine ni kutoa taarifa za maendeleo ya ujenzi wa maabara juu ya hatua za utekelezaji zilizofikiwa, changamoto zilizopo na hatua za utatuzi wa changamoto.
=30=

MAJI MBEYA KUTOA LITA ZA UJAZO 51,000



Na. Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jiji la Mbeya
Mamlaka ya Majisafi na usafi wa mazingira Jiji la Mbeya ina uwezo wa kutoa maji lita za ujazo 51,000 kupitia vyanzo vyake 13 vya maji.

Katika risala ya wafanyakazi wa Mamlaka ya Majisafi na usafi wa mazingira Jiji la Mbeya iliyosomwa kwa mgeni rasmi na Fundi Mkuu, Kanda namba 1 Amiri Abdallah Sapi Mkwawa amesema kuwa mahitaji halisi ya maji katika Jiji la Mbeya ni mita za ujazo 38,000 kwa siku. Amesema kuwa mahitaji hayo hupanda wakati wa kiangazi kufikia mita za ujazo 43,000 kwa siku katika miezi ya Septemba hadi Novemba. Amesema kuwa Mamlaka ina jumla ya vyanzo 13 vya maji vyenye uwezo wa kutoa mita za ujazo 49,000-51,000 kwa siku. Amevitaja vyanzo hivyo kuwa ni Ivumwe I na Ivumwe II, Nzovwe, Imeta, Sisimba, Hanzya, Mfwizimo. Vyanzo vingine ni Nsalaga, Lunji, Mwatezi, Mkwanana, Iduda na Halewa. Amesema kuwa baadhi ya vyanzo vinapungukiwa maji wakati wa kiangazi kutokana na ukame na shughuli za kibinadamu kama uchomaji wa moto, kilimo na ukataji wa miti kwa ajili ya kuni na mkaa.

Mkwawa amesema kuwa katika kuhakikisha rasilimali maji inaendelea kuwepo, Mamlaka kwa kushirikiana na wadau imeendelea na jitihada za kuhakikisha kuwa vyanzo vya maji vinahifadhiwa. Amesema kuwa Mamlaka yake inahakikisha kuwa miundombinu ya majisafi na majitaka iliyopo inatunzwa. “Ili kulipa uzito suala hili Mamlaka kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo Jeshi la Polisi, Jeshi la kujenga Taifa, JWTZ, Wakala wa Misitu Tanzania (TFS), Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) imeunda kamati ya mazingira kwa lengo la kuhifadhi vyanzo vya maji vilivyomo kwenye safu za mlima Mbeya ambapo leo hii utaikabidhi kamati sehemu ya vitendea kazi” Mkwawa. 

Mkuu, Kanda namba 1 amesema kuwa Mamlaka imeweza kuzalisha majisafi na salama na kuyasambaza kwa asilimia 96 ya wakazi wa Jiji la Mbeya. Amesema katika kuboresha miundombinu ya majisafi na majitaka katika Jiji la Mbeya fedha za ndani na fedha za wafadhili zimeendelea kutumika. Mradi wa awamu ya pili na mradi wa kupeleka maji uwanja wa Ndege wa Songwe ni miongoni mwa maboresho yaliyofanyika. 

Amesema katika kukabiliana na uharibifu wa miundombinu dira za maji, Mamlaka imeendelea kuwabaini na kuwachukulia hatua za kisheria baadhi ya wezi wa maji. Hatua nyingine ni kuhifadhi vyanzo vya maji kwa kushirikiana na wadau mbalimbali. 

Akiongelea changamoto zinazoikabili Mamlaka ya Maji, Mkwawa amezitaja kuwa ni baadhi ya wateja hasa taasisi za umma kutokulipa ankara za maji kwa wakati au kutokulipa kabisa. Changamoto nyingine ni baadhi ya vyanzo vya maji vimeendelea kupungukiwa na maji, kutokana na uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabia nchi akitolea mfano chanzo cha mto Lunji na Mfwizimo na Iduda.