Na. Mamlaka ya
Majisafi na Usafi wa Mazingira Jiji la Mbeya
Mamlaka ya Majisafi na usafi wa mazingira Jiji la Mbeya
ina uwezo wa kutoa maji lita za ujazo 51,000 kupitia vyanzo vyake 13 vya maji.
Katika risala ya wafanyakazi wa Mamlaka ya Majisafi
na usafi wa mazingira Jiji la Mbeya iliyosomwa kwa mgeni rasmi na Fundi Mkuu,
Kanda namba 1 Amiri Abdallah Sapi Mkwawa amesema kuwa mahitaji halisi ya maji
katika Jiji la Mbeya ni mita za ujazo 38,000 kwa siku. Amesema kuwa mahitaji
hayo hupanda wakati wa kiangazi kufikia mita za ujazo 43,000 kwa siku katika
miezi ya Septemba hadi Novemba. Amesema kuwa Mamlaka ina jumla ya vyanzo 13 vya
maji vyenye uwezo wa kutoa mita za ujazo 49,000-51,000 kwa siku. Amevitaja
vyanzo hivyo kuwa ni Ivumwe I na Ivumwe II, Nzovwe, Imeta, Sisimba, Hanzya,
Mfwizimo. Vyanzo vingine ni Nsalaga, Lunji, Mwatezi, Mkwanana, Iduda na Halewa.
Amesema kuwa baadhi ya vyanzo vinapungukiwa maji wakati wa kiangazi kutokana na
ukame na shughuli za kibinadamu kama uchomaji wa moto, kilimo na ukataji wa miti
kwa ajili ya kuni na mkaa.
Mkwawa amesema kuwa katika kuhakikisha rasilimali
maji inaendelea kuwepo, Mamlaka kwa kushirikiana na wadau imeendelea na
jitihada za kuhakikisha kuwa vyanzo vya maji vinahifadhiwa. Amesema kuwa
Mamlaka yake inahakikisha kuwa miundombinu ya majisafi na majitaka iliyopo
inatunzwa. “Ili kulipa uzito suala hili Mamlaka kwa kushirikiana na wadau
mbalimbali wakiwemo Jeshi la Polisi, Jeshi la kujenga Taifa, JWTZ, Wakala wa
Misitu Tanzania (TFS), Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira
(NEMC) imeunda kamati ya mazingira kwa lengo la kuhifadhi vyanzo vya maji
vilivyomo kwenye safu za mlima Mbeya ambapo leo hii utaikabidhi kamati sehemu
ya vitendea kazi” Mkwawa.
Mkuu, Kanda namba 1 amesema kuwa Mamlaka imeweza
kuzalisha majisafi na salama na kuyasambaza kwa asilimia 96 ya wakazi wa Jiji
la Mbeya. Amesema katika kuboresha miundombinu ya majisafi na majitaka katika Jiji
la Mbeya fedha za ndani na fedha za wafadhili zimeendelea kutumika. Mradi wa
awamu ya pili na mradi wa kupeleka maji uwanja wa Ndege wa Songwe ni miongoni
mwa maboresho yaliyofanyika.
Amesema katika kukabiliana na uharibifu wa
miundombinu dira za maji, Mamlaka imeendelea kuwabaini na kuwachukulia hatua za
kisheria baadhi ya wezi wa maji. Hatua nyingine ni kuhifadhi vyanzo vya maji
kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.
Akiongelea changamoto zinazoikabili Mamlaka ya Maji,
Mkwawa amezitaja kuwa ni baadhi ya wateja hasa taasisi za umma kutokulipa ankara
za maji kwa wakati au kutokulipa kabisa. Changamoto nyingine ni baadhi ya
vyanzo vya maji vimeendelea kupungukiwa na maji, kutokana na uharibifu wa
mazingira na mabadiliko ya tabia nchi akitolea mfano chanzo cha mto Lunji na
Mfwizimo na Iduda.
No comments:
Post a Comment