Mkuu
wa Mkoa wa Iringa Dkt. Christine Ishengoma ametoa wito kwa wananchi kuondokana
na hofu pale chanjo ya mpya za magonjwa ya kuhara na nimonia zitakapoanzishwa
mkoani Iringa.
Rai
hiyo ameitoa alipokuwa akifungua kikao cha kamati ya huduma ya afya ya msingi
Mkoa wa Iringa kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa
Mkoa.
Dkt.
Christine amesema kuwa mara nyingi chanjo mpya zinapoanzishwa wananchi wanakuwa
na hofu na minong’ono mbalimbali. Amesema “napenda kuwahakikishia wananchi kuwa
chanjo hizi ni salama na zimefanyiwa utafiti wa kina, hivyo ni salama kwa
matumizi ya binabamu”. Aidha, ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi
kuwapeleka watoto wao kupatiwa chanjo hizo ili kuweza kupunguza na hatimae
kuondoa kabisa vifo vya watoto wadogo.
Akiwasilisha
mada juu ya kuanzishwa kwa chanjo mpya za “Rotavirus na Pneumococcal” Mratibu
wa huduma za chanjo Mkoa wa Iringa, Naftal Mwalongo amesema kuwa chanjo ni moja
kati ya afua madhubuti na nafuu za kuzuia magonjwa na vifo. Amesema chanjo inazuia
magonjwa, ulemavu na inaokoa mamilioni ya watoto kila mwaka.
Akiongelea
nafasi ya chanjo katika utekelezaji wa malengo ya milenia, Mwalongo amesema “chanjo
ni afua muhimu kufikia lengo namba nne la milenia la kupunguza vifo vya
watoto chini ya mwaka mmoja ifikapo 2015”.
Mwalongo
amesema kuwa hali ya ugonjwa wa kuharisha kwa Mkoa wa Iringa mwaka 2010-2011,
idadi ya wagonjwa wa kuharisha chini ya miaka mitano kwa mwaka 2010 ilikuwa ni
35,424 sawa na asilimia 12 kati ya wagonjwa waliopata matibabu ya nje na mwaka
2011 idadi ya wagonjwa wa kiharisha chini ya miaka mitano ilikuwa 34,941 sawa
na asilimia 11 kwa wagonjwa waliopata matibabu ya nje.
Amesema
kuwa chanzo cha ugonjwa wa kuharisha ni kula au kunywa maji yaliyochafuliwa na
kinyesi chenye virusi. Aidha, amesema kuwa muda wa uambukizo hadi dalili
kujitokeza ni kati ya saa 24 hadi 48. Amesema kundi linaloathirika zaidi ni
watoto chini ya umri wa miaka miwili.
Mratibu
wa huduma za chanjo Mkoa wa Iringa, amezitaja dalili za ugonjwa wa kuhara kuwa
ni kuharisha, kutapika, kupungukiwa maji na chumvi mwilini na mara chache
huambatana na homa.
Amesema
kinga yake ni pamoja na kunyonyesha mtoto maziwa ya mama pekee na kuimarisha
usafi wa mazingira. Kinga nyingine ameitaja kuwa ni kuimarisha usafi wa mtu
binafsi kwa kunawa mikono kwa sabuni na nyongeza ya virutubishovya Zinc
huchangia katika kupunguza kuenea kwa Rotavirus, pamoja na kupatiwa chanjo ya
Rotavirus.
Kikao
hicho kilichojumuisha maafisa waandamizi, viongozi wa dini, waandishi wa habari
na watu maarufu, wataalamu toka sekta ya afya kilikuwa na lengo la kutoa uelewa
wa pamoja kwa ajili ya kuwaelimisha wananchi juu ya chanjo hizo zitakazoanza mapema
mwezi Januari, 2013.
=30=