Serikali imelipongeza jeshi la polisi
mkoani hapa kwa kazi nzuri linayofanya katika kuhakikisha ulinzi wa wananchi na
mali
zao unalindwa na wananchi wanaendelea kuishi na kufanya kazi kwa amani na
utulivu.
Waziri wa Nchi, OWM- Sera, Uratibu na Bunge William
Lukuvi (katikati) akimjulia hali Padri Angelo Burgeo hatika hospitali ya mkoa
wa Iringa
Pongezi hizo zimetolewa na Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu mwenye dhamana ya Sera, Uratibu na Bunge, William
Lukuvu alipokuwa akiongea na waandishi wa habari katika hospitali ya rufaa ya
mkoa wa Iringa alipofanya ziara ya kiserikali pamoja na mambo mengine kuwajulia
hali na kuwapa pole mapadri Angelo Burgio (60) kutoka Italia na msaidizi wake
Herman Myala wa kanisa katoliki, parokia ya Isimani, jimbo la Iringa
waliojeruhiwa vibaya na watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi.
Lukuvi amesema “napenda kulipongeza
jeshi la polisi chini ya kamanda wa mkoa wa Iringa, Michael Kamhanda kwa
jitihada zao za kuhakikisha kuwa wananchi wanakuwa katika hali ya usalama wao
na mali
zao”. Aidha, amezipongeza jitihada za jeshi hilo za kuhakikisha watuhumiwa wa uhalifu
uliofanyika katika parokia ya Isimani wanakamatwa na kufikishwa katika mkondo
wa sheria. Amesema kuwa ndani ya siku mbili jeshi hilo
limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa wanane jambo linalodhihirisha utendaji
makini wa jeshi hilo .
Kutokana na kazi hiyo nzuri, Waziri
huyo amevitaka vyombo vya habari mkoani hapa kuhakikisha vinatangaza utendaji
na ufanisi wa jeshi hilo ili wananchi waweze kufahamu utendaji huo na
kuondokana na hofu inayoweza kujitokeza na kuendelea na utendaji kazi wao wa
kila siku. Amewahakikishia wananchi kuwa serikali yao ipo makini kuhakikisha usalama wao.
Amesema kuwa ipo dhana iliyojengeka
ndani ya jamii hasa wanapowaona wazungu wanadhani kuwa ni watu wenye fedha
nyingi hivyo kushawishika kufanya uhalifu.
Wakati huohuo, Waziri Lukuvi amesema
kuwa tukio hilo la ujambazi wa kutumia silaha ni
uhalifu wa kawaida kama unavyofanyika uhalifu
mwingine wa aina hiyo nchini hivyo usihusishwe na hisia nyinyine kwa namna
yoyote ile.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa,
Kamishna Mwandamizi Msaidizi Michael Kamhanda, amesema kuwa wananchi wa Isimani
wametoa ushirikiano mkubwa kwa jeshi hilo katika tukio hilo na kuhakikisha
watuhumiwa wa uhalifu huo wanakamatwa mapema na kufikishwa katika mikono ya
sheria. Amesema kuwa watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani hivi karibuni baada
ya upelelezi kukamilika. Amesema kuwa jeshi la polisi limeanzisha program maalumu
kwa mkoa mzima ya kuwaelimisha wananchi na taasisi juu ya ulinzi shirikishi na
mbinu za kujilinda wenyewe.
Waziri wa Nchi, OWM- Sera, Uratibu na Bunge William
Lukuvi (kulia) akimpongeza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa Kamishana Mwandamizi
Msaidizi, Michael Kamuhanda (kushoto) (katikati) ni Afisa Muuguzi Muuguzi
msaidizi mkuu Lustica Tun’gombe.
Akiongelea maendeleo ya mapandri hao,
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Iringa, Dk. Faustine
Gwanchele amesema kuwa mapadri hao wanaendelea vizuri kwa ujumla.
=30=