Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Tabia
ya utunzaji wa mazingira imeelezwa kuwa ni muhimu katika kuendeleza rasilimali
maji mkoani Iringa.
Kauli
hiyo imetolewa na Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Bw. Adam Swai katika
hotuba yake ya uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya maji katika mkoa wa Iringa
yaliyofanyika katika Kata ya Ruaha, Manispaa ya Iringa.
Bw.
Swai amesema “utunzaji wa mazingira ni
kitu muhimu katika kuhakikisha uendelevu wa rasilimali maji. Sote tunafahamu
kuwa rasilimali maji ni muhimu kwa maisha na maendeleo ya binadamu zikiwepo
shughuli za kiuchumi. Bila maji hakuna maendeleo na bila maendeleo hakuna maji,”.
Akiongelea
kusuasua kwa ujenzi wa miradi ya maji, Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Iringa
amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri kusimamia kikamilifu ujenzi wa miradi ya
maji. Aidha, amewataka kuwapatia kazi makandarasi na wataalamu washauri wenye
uwezo na sifa za kufanya kazi zenye ubora. Amewataka kujiridhisha na uwezo wa
makandarasi kabla ya kuwapatika kazi juu ya ubora wa utendaji kazi wao ili miradi
ikamilike kwa wakati.
Akiongelea
juhudi za kuongeza upatikanaji huduma ya maji mijini na vijijini, ameshauri kutumia
teknolojia ya uvunaji wa maji ya mvua. Ameongeza utumiaji wa teknolojia ya
nguvu ya jua na nguvu ya upepo katika kusukuma maji katika ngazi ya kaya na
taasisi kutokana na urahisi wa teknolojia hizo.
Akiongelea hali ya upatikanaji huduma ya maji mkoani
Iringa, Mhandisi wa Maji Mkoa wa Iringa, Mhandisi Shaban Jellan amesema kuwa
hadi kufikia Disemba, 2014, idadi ya watu waliokuwa wakipata huduma ya maji
ndani ya umbali usiozidi mita 400 toka kwenye makazi yao ni 651,917 sawa na
69.3% ya wakazi wote wa Mkoa wa Iringa.
Akiongelea huduma ya maji vijijini, amesema kuwa
wakazi wa vijijini wanaopata huduma ya maji ni 452,524 sawa na 66.1% ya wakazi wote
waishio vijijini. Ameitaja idadi ya wanaopata huduma ya maji kwa kila Halmashauri
kuwa ni 90% sawa na wananchi 14,213 katika Halmashauri ya Manispaa
(vijijini-peri-urban), 69% sawa na wananchi 175,282 katika Halmashauri ya
Wilaya ya Iringa. Katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo ni 60.8% sawa na wananchi
93,722 na Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi 64.8 sawa na wananchi 172,258
wanaopata huduma ya maji.
Maadhimisho ya wiki ya maji
mwaka huu yanaongozwa na kauli mbiu isemayo maji na maendeleo endelevu.
=30=