Friday, August 5, 2016

TEKNOLOJIA NA USHIRIKISHAJI WADAU NGUZO YA MAFANIKIO WILAYA YA IRINGA


Na Mwandishi Maalum Mbeya

Nafasi ya teknolojia na ushirikishaji wadau wa sekta ya kilimo, mifugo, uvuvi na ushirika ni ufunguo wa mafanikio kwa mkulima nchini.

Kauli hiyo ilitolewa na Afisa Kilimo, Umwagiliaji na Ushirika wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Lucy Nyalu alipokuwa akielezea mafanikio ya Halmashauri yake kuwa mshindi wa kwanza katika maonesho ya Nanenane Nyanda za juu Kusini mwaka 2015.

Nyalu alisema “Halmashauri ya wilaya ya Iringa imejikita katika mambo makuu mawili; mosi, ni teknolojia ya kilimo na pili ushirikishaji wadau wa sekta ya kilimo, mifugo, uvuvi na ushirika ili kushirikiana nasi katika kumkomboa mkulima wa Halmashauri ya wilaya ya Iringa na taifa kwa ujumla”. 

Alisema kuwa ushindi wa kwanza katika maonesho ya mabanda ya Nanenane Nyanda za juu Kusini mwaaka 2015 ulitokana na chachu ya teknolojia na wadau kwa umoja wao. Aliongeza “maonesho ya Nanenane kwetu ni suala mtambuka, linalohusisha Idara zote za Halmashauri ndiyo maana utaona kila Idara ipo hapa kuonesha ushirikiano na ushirikishaji wa shughuli zinazofanyika katika Halmashauri pamoja na uchache wa rasilimali uliopo. 

Wataalam na wakulima wetu wote wamekuja kufundisha yale yanayofanyika katika Halmashauri yetu kwa ufanisi mkubwa, na kujifunza mambo mapya kwa lengo la kuboresha zaidi utendaji kazi”.

Akiongelea Halmashauri yake ilivyojipanga katika maonesho ya Nanenane mwaka 2016, Nyalu alisema kuwa Halmashauri yake imejipanga vizuri zaidi kwa kuongeza matumizi ya teknolojia katika sekta ya kilimo na ushirikishaji wadau. Teknolojia hizo alizitaja kuwa ni hifadhi bora ya mazao kwa kutumia mifuko ya pics na vihenge vya chuma, teknolojia ya kuvuna maji kwa kutumia sola kwa matumizi ya majumbani na kumwagiliaji, teknolojia ya kufukuza ndege kwenye kilimo cha mpunga, teknolojia ya usindikaji mboga kwa kutumia sola, teknolojia ya usindikaji ngozi na wanafunzi wenye ulemavu wanaochapa kazi katika kompyuta kwa kutumia miguu.

Halmashauri ya wilaya ya Iringa, inatarajia kutetea ushindi wa kwanza katika maonesho ya Nanenane Kanda ya Nyanda za juu Kusini kwa kushirikisha wadau wa John Deere, One Acre Fund, Rudi, Asas Tahea, Vista, Clinton Foundation, SNV na Britain.
=30=