Sekta ya Ushirika iamke
Sekta ya ushirika imetakiwa kujizatiti zaidi ili iweze kuwakomboa wananchi wengi zaidi kutoka katika wimbi la umasikini mkoani Iringa.Katibu Tawala Msaidizi, Sehemu ya Uchumi na uzalishaji mali, Alhaji. Adam Swai
Rai hiyo imetolewa na Katitu Tawala Msaidizi, Sehemu ya uchumi na sekta za uzalishaji mali, Alhaji Adam Swai katika mkutano wa robo ya kwanza ya 2010/2011 wa wataalamu wa sekta ya kilimo, mifugo na ushirika uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Lutheran, wilayani Njombe.
Alhaji Swai amesema “sijaridhika na uendeshaji wa sekta ya ushirika, sababu bado tupo nyuma kidogo”. “Ni kwa kuboresha sekta ya ushirika ndipo tunaweza kuwakomboa wananchi wa mkoa wa Iringa kutoka katika umasikini”. Aidha ameongeza kusema kuwa ushirika ukiboreshwa katika mkoa wa Iringa utawawezesha na kuwahakikishia wananchi upatikanaji wa pembejeo kwa uhakika na wakati.
Akiwasilisha mradi wa kahawa uliofanya vizuri katika mpango wa uedelezaji wa sekta ya kilimo wilayani (DADPs) katika wilaya ya Ludewa, Kaimu Afisa Kilimo na Mifugo wa wilaya ya Ludewa, Ndyetabura Kalokora amesema kuwa wilaya kwa kushirikiana na kituo cha utafiti (TaCRI) wilianzisha vitalu 9 vyenye jumla ya miche 7,759 na jumla ya miche 20,709 imezalishwa, miche 14,019 imepandwa na miche 6,690 bado inaendelea na hatua ya ukuaji vitaluni ikiwa katika viriba.
Amesema kuwa kabla ya mradi wakulima walikuwa wakilima kahawa inayoshambuliwa na magonjwa ya chelebuni na kutu ya majani. Kahawa ilikuwa ikitoa mavuno kidogo kwa mti. Amebainisha tatizo linigine kuwa ni mkahawa kuchelewa kutoa mavuno kwa kuanza kuzaa baada ya miaka mitatu sambamba na ukubwa wa gharama za uzalishaji kuwa kubwa sababu iliyopelekea wakulima kutelekeza mashamba yao na kiwango cha uzalishaji kushuka.
Akielezea hali ya uzalishaji miche ya vikonyo ilivyo sasa Kalokora amesema kuwa uzalishaji wa miche ya vikonyo ulianzishwa mwaka 2006 baada ya wakulima kupata mafunzo katika kituo cha utafiti (TaCRI-Mbinga). Wilaya ilianza na miche mama 2000 iliyopandwa katika vijiji vya Mundindi, Masimbwe, Lufumbu na Mawengi.
Kalokora ameyataja mafanikio yaliyopatikana kuwa ni pamoja na kuanzishwa kwa mashamba mama ya kahawa inayovumilia magonjwa ya kutu ya majani na ugonjwa wa chelebuni yenye jumla ya miche 7,759. Mafanikio mengine ameyataja kuwa ni kuviimarisha vyama vya ushirika kuweza kununua mazao kwa mfumo wa stakabadhi ghalani, kununua kahawa kutoka kwa wakulima kupitia vyama vyao vya ushirika, ari ya wakulima imeanza kurudi tena baada ya kupata miche inayovumilia magonjwa na kupungua kwa gharama za uzalishaji.
Mkutano huo wa wataalamu wa sekta ya kilimo, mifugo, ushirika na uvuvi umewakutanisha wataalamu hao toka sekretarieti ya mkoa wa Iringa na Halmashauri zote, pia umewashirikisha maafisa mipango na maendeleo ya jamii unafanyika kwa siku tatu wilayani Njombe.