Wednesday, November 21, 2012

KAMPUNI ZAIDI YA 10 KUSAMBAZA MBOLEA IRINGA




Kampuni za mbolea zaidi ya 10 zimejitokeza kuhudumia wakulima katika Wilaya ya Iringa kwa ajili ya kusambaza vocha za pembejeo za kilimo kwa mwaka 2012/2013 na 2013/2014.

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa utoaji wa pembejeo zenye ruzuku kwa msimu wa kilimo wa mwaka 2011/2012 na maandalizi ya kilimo msimu wa mwaka 2012/2013 katika kikao cha kamati ya pembejeo cha mkoa wa Iringa, Afisa Kilimo, Mifugo na Ushirika wa Wilaya ya Iringa, Lucy Nyalu amesema kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa imepokea utaratibu mpya kutoka Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika wa usambazaji wa pembejeo zenye ruzuku ya Serikali kwa wakulima wa mahindi na mpunga kwa msimu wa kilimo wa mwaka 2012/2013.

Amesema kuwa utaratibu wa kutumia vocha utaendelea ila mawakala watakaosambaza pembejeo hizo kwa wakulima wanufaika na kampuni ya pembejeo ndiyo itasambaza pembejeo hizo badala ya kamati ya pembejeo ya wilaya kama ilivyokuwa awali.
Amesema lengo la kampuni za pembejeo kupewa jukumu la kuteua mawakala ni kuhakikisha pembejeo zenye ubora zinawafikia wakulima kwa wakati muafaka. Amesema kuwa kazi ya kamati ya pembejeo ya wilaya itakuwa ni kusimamia na kufuatilia utaratibu mzima wa pembejeo katika mchakato wote.

Lucy amesema jumla ya kampuni 13 za mbolea na mbegu zimejitokeza kuhudumia wakulima wa Wilaya ya Iringa. Amesema makampuni hayo yameteua mawakala wawakilishi saba na mawakala wasaidizi 46. Akiongelea uhamasishaji wa matumizi ya mbolea ya minjingu mazao pamoja na utaratibu wa usambazaji wa vocha za pembejeo za kilimo kwa wakulima kwa kipindi cha mwaka 2012/2013 na 2013/2014 umefanyika katika vijiji vya Nyabula, Lupembelwasenga, Usengelindeti, Makombe, Kihanga, Ng’enza, Magulilwa na Tagamenda. Uhamasishaji huo unaendelea sambamba na usambazaji wa vocha za pembejeo.

Wakati huohuo, Halmashauri ya Wilaya ya Iringa imepokea mgao wa pembejeo zenye ruzuku kwa mwaka 2012/2013 zenye thamani ya shilingi 1,828,654,000. Akielezea aina ya pembejeo hizo, Afisa Kilimo, mifugo na ushirika amesema kuwa mbolea ya kupandia vocha (22,000), mbolea ya kukuzia (22,000), mbegu ya mahindi (chotara) (5,409),mbegu ya mahindi mchanganyiko (9,309), mbegu ya mpunga (7,282).

Lucy ameyataja mafanikio yaliyotokana na mfumo wa vocha kuwa ni upatikanaji wa pembejeo katika ngazi ya kijiji umefikiwa ambapo wakulima wanaweza kununua pembejeo katika maeneo ya vijiji vyao. Mafanikio mengine ameyataja kuwa ni ongezeko la uzalishaji kutoka gumia 3-5 za mahindi hadi kufikia wastani wa gunia 12-22 kwa ekari, kwa zao la mpunga ongezeko kutoka gunia 8-10 hadi kufikia wastani wa gunia 16-25.  Aidha, idadi ya wakulima wanaolima kitaalamu imeongezeka na matumizi ya pembejeo kwa wakulima yameongezeka.

Akifungua kikao hicho Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma amekiaarifu kikao hicho kuwa msimu wa kilimo umefika na kuwa mvua zimeanza kunyesha katika baadhi ya maeneo ya Wilaya ya Mufindi na wakulima wameanza kupanda. Aidha, aliwataka wataalamu wa kilimo kuwa karibu na wakulima katika kuwafundisha na kuwaelekeza mbinu bora za kilimo. 

=30= 

JAPAN KUSHIRIKIANA NA TANZANIA KATIKA AFYA



Serikali ya Japan imeahidi kuendeleza ushirikiano uliopo baina yake na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika sekta mbalimbali hasa sekta ya afya na kilimo.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma akimkabidhi kitabu cha profile ya Mkoa wa Iringa Balozi wa Japan nchini Tanzania

Ahadi hiyo imetolewa na Balozi wa Japan nchini Tanzania Masaki Okada alipotembelea ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa katika ziara iliyolenga kusaini mkataba wa ukarabati wa hospitali ya Tosamaganga iliyopo katika halmashauri ya wilaya ya Iringa.

Balozi Okada amesema kuwa Serikali yake itaendeleza ushirikiano na Tanzania katika kuhakikisha uchumi unakuwa kwa kasi zaidi kwa kukuza biashara baina ya nchi mbili hizo. Amesema kwa kuwa zaidi ya asilimia 80 ya watanzania wanategemea kilimo, ni lazima kipato chao kiongezeke ili waweze kunufaika na kilimo hicho kama shughuli yao kuu ya kiuchumi. Amesema kuwa Serikali yake inao mpango wa kuisaidia sekta ya kilimo nchili ili kuhakikisha kilimo cha mpunga kinaongezeka mara dufu kwa kuwa nchi ya Japan inasifika kwa uzalishaji wa mpunga duniani.

Aidha, amezipongeza juhudi za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuwaletea maendeleo wananchi wake na kuahidi kuziunga mkono juhudi hizo kwa karibu.

Awali katika salamu za Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma amesifu juhudi za Serikali ya Japan katika kusaidia maendeleo kwa mkoa wa Iringa na kusema ni juhudi za kupongezwa sana. Amesema kupitia misaada ya Japan, Halmashauri ya Wilaya ya Iringa imeweza kupata ufadhili katika utekelezaji wa miradi ya afya, elimu, kilimo, maji na umwagiliaji.

Akiongelea maambukizi ya virusi vya ukimwi na ukimwi, Mkuu wa Mkoa wa Iringa amesema kuwa kwa kujibu wa utafiti wa mwaka 2008, mkoa wa Iringa ulikuwa na takribani asilimia 16 ya maambukizi, kiwango ambacho ni karibu mara tatu ya kiwango cha maambukizi kitaifa. Amesema kuwa hali hiyo haikubaliki na zinaihitajika juhudi za pamoja kati ya Tanzania na Japan katika kuendeleza mapambano hayo. Aidha, amezipongeza juhudi za Serikali ya Japan za kuisaidia Tanzania katika sekta ya afya na ustawi wa jamii kupitia miradi mbalimbali kwa lengo la kuboresha afya ya mama na familia katika  mkoa wa Iringa.

Balozi wa Japan nchini Tanzania yupo mkoani Iringa kwa ajili ya utiaji saini mkataba wa ukarabati wa hospitali ya Tosamaganga unaogharimu dola za kimarekani 123,339 kwa lengo la kuongeza ubora wa huduma za afya na kupunguza vifo vya wanawake na watoto mkoani Iringa.
=30=