Tuesday, May 22, 2018

MWENGE WA UHURU KUTEMBELEA MIRADI 40 YA MAENDELEO IRINGA


Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa
Mwenge wa Uhuru utatembelea miradi ya maendeleo 40 yenye thamani ya shilingi 24,427,360,696.40 mkoani Iringa na kutoa ujumbe maalum wa mwaka 2018.

Akitoa taarifa ya ujuo wa Mwenge wa Uhuru kwa wananchi kupitia vyombo vya habari vya mkoa wa Iringa, mkuu wa mkoa wa Iringa Amina Masenza alisema kuwa Mwenge wa uhuru utatembelea, kagua, kuzindua, kufungua na kuweka mawe ya msingi,  jumla ya miradi 40. Aliongeza kuwa miradi hiyo ina thamani ya shilingi 24,427,360,696.40. 
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza akiongea na waandishi wa Habari

Miradi hiyo inatoka sekta za elimu (10), afya (7), maji (4) maliasili (1), kilimo (5), viwanda viwili (2) uvuvi (1) na mapambano dhidi ya rushwa (4). Gharama za miradi hiyo zimetokana na michango ya wananchi shilingi 1,251,610,850.00, Serikali kuu shilingi 8,638,969,449.40, Halmashauri shilingi 253,564,461.00 na wadau wa maendeleo shilingi 14,283,215,936.00   

Akiongelea ujumbe wa mwenge wa uhuru mwaka 2018, mkuu wa mkoa wa Iringa alisema kuwa Mwenge wa Uhuru utatoa ujumbe maalumu na ujumbe wa kudumu katika maeneo yote ambako utakimbizwa. Ujumbe maalumu wa Mwenge wa Uhuru wa mwaka 2018 ni: ‘Elimu ni Ufunguo wa Maisha; Wekeza sasa kwa maendeleo ya Taifa letu’. Ujumbe huu unalenga kutilia mkazo umuhimu wa uwekezaji katika elimu unaofanywa na serikali pamoja na Wananchi ikiwa ni mkakati madhubuti katika kupiga vita umaskini na kujenga taifa lenye maendeleo ya viwanda alisema mkuu wa mkoa.

Pamoja na kutoa ujumbe mahususi, Mwenge wa Uhuru utaendelea kuhimiza mapambano dhidi ya UKIMWI chini ya kauli mbiu isemayo ‘mwananchi jitambue; pima afya yako sasa’. Ujumbe mwingine aliutaja kuwa ni mapambano dhidi ya Malaria chini ya kauli mbiu isemayo ‘Shiriki kutokomeza Malaria kwa manufaa ya Jamii’

Ujumbe mwingine ni mapambano dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya chini ya kauli mbiu isemayo ‘Tuwasikilize na kuwashauri watoto ili wasitumie dawa za kulevya’ na Mapambano ya kutokomeza Rushwa chini ya kauli mbiu isemayo:-‘Kataa Rushwa- Jenga Tanzania’.

Mwenge wa Uhuru utakimbizwa mkoani Iringa kwa siku tano na kukabidhiwa mkoani Njombe tarehe 28/5/2018.
=30=

No comments:

Post a Comment