Tanzania imefanikiwa kupunguza idadi
ya vifo vya watoto walio na umri chini ya miaka mitano kwa asilimia 45 kutokana
na kuhimiza matumizi ya chanjo dhidi ya kujikinga na magonjwa mbalimbali
nchini.
Hayo yamesemwa na mratibu wa chanjo
kitaifa toka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Zebina Msumi wakati akiwasilisha
mada juu ya hali ya chanjo nchini katika semina ya waandishi wa habari wa mikoa
ya Iringa, Njombe na Ruvuma kuhusu kuanzishwa kwa chanjo mpya za pneumococcal
na rotavirus iliyofanyika katika ukumbi wa chuo kikuu huria tawi la Iringa.
Zebina amesema kuwa Tanzania kama
nchini nyingine zinazoendelea inafanya juhudi kubwa ili kufikia malengo ya
milenia ya nne na tano ifikapo mwaka 2012. Amesema katika juhudi hizo, Tanzania
imefanikiwa kupunguza vifo vya watoto walio na umri chini ya miaka mitano
kutoka 147 mwaka 1999 hadi kufikia vifo 81 kwa kila watoto 1,000 waliozaliwa
hai, hilo likiwa ni punguzo la asilimia 45. Aidha, vifo vya watoto chini ya
mwaka mmoja vimepungua kutoka 99 hadi kufikia 51 ilikuwa ni punguzo la asilia
49.
Amesema kuwa mafanikio hayo yanatokana na viwango vya chanjo kuendelea
kupanda kutoka asilimia 50 miaka ya 60 hadi kupindukia asilimia 90 mwaka 2011.
Akielezea huduma ya chanjo nchini, mratibu
huyo amesema kuwa imethibitika kitaalamu kuwa chanjo mkakati muafaka katika
kutokomeza maradhi na kupunguza vifo vya watoto na kupunguza gharama kubwa
ambazo familia na taifa kwa ujumla limetumia katika kutibu maradhi yatokanayo
na magonjwa yanayozuilika kwa chanjo. Ameyataja magonjwa yanayokingwa kupitia
mpango wa chanjo kuwa ni kifua kikuu, polia, dondakoo, pepopunda, kifaduro,
homa ya ini, homa ya uti wa mgongo, surua na vichomi.
Kwa upande wa changamoto zilizopo, Zenina
amezitaja kuwa ni vimelea vya “Streptococcus pneumoniae” ni kisababishi kikuu cha maradhi na vifo vitokanavyo ugonjwa wa
vichomi na homa ya uti wa mgongo. Ameongeza kuwa vimelea vya “rotavirus” kwa
upande mwingine husababisha takribani asilimia 80 ya maradhi na vifo
vitokanavyo na kuharisha kukali kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano
duniani.
Ameitaja mikakati iliyopo kuwa ni chanjo
ya “pneumococcal” (PCV13) kukinga maambukizi ya vichomi kwa asilimia 38 na homa
ya uti wa mgongo kwa karibia asilimia 87 na chanjo ya “rotavirus” inayokinga kuharisha
kukali kunakosababisha vifo vya watoto kwa asilimia 80; na kwa sehemu kubwa
kukinga ugonjwa wa kuharisha unaosababishwa na vimelea vya aina nyingine pia.
Mikakati
mingine ameitaja kuwa ni Serikali na Wadau wa maendeleo kuhakikisha kuwa chanjo zinapatikana kwa
walengwa wote na kwa muda unaotakiwa na miundombinu ya kuhifadhi na kusafirisha
chanjo imeimarishwa kuwezeshwa kutunza.
Vilevile,
chanjo za PCV13 na Rotarix zimeshawasili nchini na zimesambazwa mikoa yote na watumishi kupatiwa mafunzo ya jinsi ya
kutoa chanjo hizi mpya.
Mtoa mada amewata wanahabari hao
kuwahimiza akina mama kunyonyesha maziwa ya mama pekee kwa miezi sita na kuimarisha
usafi wa mazingira na kunawa mikono kwa sabuni husaidia kupunguza mambukizo ya
magonjwa ya kuhara.
Vilevile, amesisitiza kuwa chanjo ya
Rotarix itatolewa pamoja na chanjo zingine
zinazotolewa katika kliki na ratiba ya chanjo inatolewa mtoto akiwa na wiki 6 na 10. Chanjo
hii inatolewa bure katika vituo vinavyotoa huduma za chanjo nchini kama ilivyo
kwa chanjo zingine.
=30=