Na. Dennis Gondwe, Ofisi ya Mkuu wa
Mkoa-IRINGA
Jamii
imetakiwa kuacha unyanyapaa kwa wagonjwa wa kifua kikuu kwa sababu nao ni
sehemu ya jamii badala yake kuwapa ushirikianao wa hali ya juu.
Kauli
hiyo ilitolewa na mratibu wa kifua kikuu na ukoma mkoa wa Iringa, Dr. Tecla
Orio alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kuhusiana na madhara ya
unyanyapaa kwa wagonjwa wa kifua kikuu katika bustani ya Manispaa ya Iringa
hivi karibuni.
|
Dr Tecla Orio |
|
KIKUKI |
Dr.
Orio alisema kuwa wagonjwa wa kifua kikuu wamekuwa wakipata unyanyapaa toka kwa
jamii na kuwaathiri kisaikolojia. Aliongeza
jamii imekuwa ikiwaangalia na kuwasemea maneno mabaya wagonjwa wa kifua kikuu
na familia zao.
“Wagonjwa hawa na familia
zao wamekuwa wakitengwa katika shughuli za kijamii na kuwafanya waendelee
kujiona wanyonge katika jamii” alisema Dr. Orio. Kutokana na hali hiyo ya
unyanyapaa, wagonjwa wa kifua kikuu wanakuwa katika hali ya huzuni, upweke,
wasiwasi na kutokujiamini na kukata tamaa.
“Hali ya unyanyapaa imewafanya
wagonjwa kuchelewa kupata vipimo na matibabu na kuendelea kueneza ugonjwa huo
kwa watu wengine. Lakini unyanyapaa huo umekuwa pia na athari kwa kuwafanya
wagonjwa kujificha kuzuia wasitoe taarifa kuhusu hali zao” alisisitiza Dr.
Orio.
Akiongelea
sababu za unyanyapaa, mratibu wa kifua kikuu na ukoma mkoa wa Iringa, alizitaja
kuwa ni ukosefu wa elimu kuhusu ugonjwa wa kifua kikuu hasa njia
zinazosababisha maambukizi.
“Uhusiano wa
ugonjwa wa kifua kikuu na virusi vya ukimwi, ugunduzi na matibabu yake.
Wagonjwa wa kifua kikuu kuonekana hawakuwa makini katika kujikinga” alisema
Dr Orio. Sababu nyingine aliitaja kuwa ni ukosefu wa vifaa vya kujikinga kwa
wahudumu wa afya walio katika hatari ya kuambukizwa.
Mratibu
huyo aliitaka jamii kuwapa ushirikiano wagonjwa wa kifua kikuu na kuwatia moyo
ili wakamilishe matibabu yao na kuendelea na utekelezaji wa majukumu yao.
Aidha, aliikumbusha jamii kuwa mgonjwa wa kifua kikuu akishaanza matibabu
hawezi kuambukiza watu wengine.
Katibu
wa kikundi cha kudhibiti kifua kikuu mkoa wa Iringa (KIKUKI), Lucas Mallya
alisema kuwa ugonjwa wa kifua kikuu ni kama ugonjwa mwingine unaotibiwa katika
vituo vya kutolea huduma za afya.
“Mgonjwa
wa kifua kikuu anapoanza dawa hupona kabisa na hupewa elimu ya kujikinga na
maambukizi ya ugonjwa huo. Bahati nzuri matibabu ya kifua kikuu ni bure kabisa”
alisema Mallya.
Matibabu
ya ugonjwa wa kifua kikuu huchukua miezi sita hadi nane na hutolewa bure katika
vituo vya kutolea huduma vya serikali na binafsi.
=30=