Thursday, November 23, 2017

IRINGA WATAKIWA KUACHA UNYANYAPAA WAGONJWA WA TB



Na. Dennis Gondwe, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa-IRINGA
Jamii imetakiwa kuacha unyanyapaa kwa wagonjwa wa kifua kikuu kwa sababu nao ni sehemu ya jamii badala yake kuwapa ushirikianao wa hali ya juu.

Kauli hiyo ilitolewa na mratibu wa kifua kikuu na ukoma mkoa wa Iringa, Dr. Tecla Orio alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kuhusiana na madhara ya unyanyapaa kwa wagonjwa wa kifua kikuu katika bustani ya Manispaa ya Iringa hivi karibuni.
 
Dr Tecla Orio

KIKUKI

Dr. Orio alisema kuwa wagonjwa wa kifua kikuu wamekuwa wakipata unyanyapaa toka kwa jamii na kuwaathiri kisaikolojia.  Aliongeza jamii imekuwa ikiwaangalia na kuwasemea maneno mabaya wagonjwa wa kifua kikuu na familia zao. 

Wagonjwa hawa na familia zao wamekuwa wakitengwa katika shughuli za kijamii na kuwafanya waendelee kujiona wanyonge katika jamii” alisema Dr. Orio. Kutokana na hali hiyo ya unyanyapaa, wagonjwa wa kifua kikuu wanakuwa katika hali ya huzuni, upweke, wasiwasi na kutokujiamini na kukata tamaa. 

Hali ya unyanyapaa imewafanya wagonjwa kuchelewa kupata vipimo na matibabu na kuendelea kueneza ugonjwa huo kwa watu wengine. Lakini unyanyapaa huo umekuwa pia na athari kwa kuwafanya wagonjwa kujificha kuzuia wasitoe taarifa kuhusu hali zao” alisisitiza Dr. Orio.

Akiongelea sababu za unyanyapaa, mratibu wa kifua kikuu na ukoma mkoa wa Iringa, alizitaja kuwa ni ukosefu wa elimu kuhusu ugonjwa wa kifua kikuu hasa njia zinazosababisha maambukizi. 

Uhusiano wa ugonjwa wa kifua kikuu na virusi vya ukimwi, ugunduzi na matibabu yake. Wagonjwa wa kifua kikuu kuonekana hawakuwa makini katika kujikinga” alisema Dr Orio. Sababu nyingine aliitaja kuwa ni ukosefu wa vifaa vya kujikinga kwa wahudumu wa afya walio katika hatari ya kuambukizwa.

Mratibu huyo aliitaka jamii kuwapa ushirikiano wagonjwa wa kifua kikuu na kuwatia moyo ili wakamilishe matibabu yao na kuendelea na utekelezaji wa majukumu yao. Aidha, aliikumbusha jamii kuwa mgonjwa wa kifua kikuu akishaanza matibabu hawezi kuambukiza watu wengine.

Katibu wa kikundi cha kudhibiti kifua kikuu mkoa wa Iringa (KIKUKI), Lucas Mallya alisema kuwa ugonjwa wa kifua kikuu ni kama ugonjwa mwingine unaotibiwa katika vituo vya kutolea huduma za afya.

Mgonjwa wa kifua kikuu anapoanza dawa hupona kabisa na hupewa elimu ya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo. Bahati nzuri matibabu ya kifua kikuu ni bure kabisa” alisema Mallya.

Matibabu ya ugonjwa wa kifua kikuu huchukua miezi sita hadi nane na hutolewa bure katika vituo vya kutolea huduma vya serikali na binafsi.
=30= 

No comments:

Post a Comment