Wednesday, January 31, 2018

IRINGA YAPONGEZWA USIMAMIZI UJENZI WA HOSPITALI WILAYA KILOLO



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa
Ofisi ya mkuu wa Mkoa wa Iringa imepongezwa kwa usimamizi makini unaozingatia thamani ya fedha katika ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Kilolo unaoendelea.

Pongezi hizo zilitolewa na makamu mwenyekiti wa kamati ya Bunge ya utawala na serikali za mitaa, Mwanne Mchemba alipokuwa akiongea na wataalam wa Mkoa wa Iringa na Wilaya ya Kilolo katika kumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo baada ya kamati yake kukagua ujenzi wa hospitali hiyo hivi karibuni.
 
Mwanne Mchemba, Makamu Mwenyekiti Kamati ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa
Mchemba alisema kuwa ofisi ya mkuu wa Mkoa wa Iringa imefanya kazi nzuri kusimamia ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Kilolo. 

Najua mipango mizuri ya ujenzi wa hospitali hii mliiratibu vizuri tangu mwanzo ndiyo sababu ujenzi unaenda vizuri. Kamati yangu imeridhishwa na hatua ya ujenzi kwa kuzingatia thamani ya fedha” alisema Mchemba. 

Alipongeza wazo hilo kuwa linalenga kuboresha afya za wananchi wa Wilaya ya Kilolo na taifa kwa ujumla kwa kuwapatia huduma bora za afya.

Mchemba aliishauri ofisi ya Rais TAMISEMI kutoa kipaumbele katika ujenzi wa chumba cha upasuaji na chumba cha kuhifadhia maiti. Alisema kuwa ujenzi wa majengo hayo utasaidia kuiwezesha hospitali hiyo kuanza ikiwa na maeneo muhimu ya utoaji huduma. Aidha, alielekeza hospitali hiyo kupatiwa gari la wagonjwa. 

Kutokana na jiografia ya Wilaya ya Kilolo ni muhimu hospitali ya Wilaya kupewa gari la wagonjwa. Gari hilo ni muhumu sana kwa sababu litasaidia kuokoa maisha ya wananchi watakaohitaji huduma ya haraka na dharura hospitali hapo” alisema Mchemba.  

Awali katika taarifa ya ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Kilolo iliyosomwa na mganga mkuu wa Wilaya, Dr. Mohamed Mang’una alisema kuwa mradi huo ulianza kwa gharama ya shilingi 259,451,899 kugharamia ujenzi awamu ya kwanza na ya pili. Alisema kuwa kupitia ruzuku ya maendeleo ya serikali za mitaa kwa mwaka 2011/2012 zilitolewa shilingi 145,744,500 na mwaka 2012/2013 zilitolewa shilingi 113,707,399 kujenga jengo la wagonjwa wa nje.

Hospitali ya Wilaya ya Kilolo imelenga kuhudumia wakazi wanaokadiriwa kuwa 229,146 kutokana na sense ya watu na makazi ya mwaka 2012.
=30=

USHIRIKIANO WA CHAMA NA SERIKALI WAPONGEZWA KILOLO



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa-Iringa
Kamati ya Bunge ya utawala na serikali za mitaa imepongeza ushirikiano baina ya serikali na chama tawala wilayani Kilolo kwa maendeleo ya wananchi.

Pongezi hizo zilitolewa na mjumbe wa kamati ya Bunge ya utawala na serikali za mitaa, Magreth Sitta katika ukumbi wa halmashauri ya Wilaya ya Kilolo wakati kamati hiyo ilipotembelea mradi wa ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Kilolo hivi karibuni.
 
Magreth Sitta, Mbunge wa Urambo
Sitta ambaye ni mbunge wa Urambo alisema kuwa mshikamano baina ya serikali na chama tawala ni muhimu katika kufanikisha dhamira ya serikali ya kuwaletea maendeleo wananchi. Alisema ili mchakato wa maendeleo uende vizuri ni muhimu kwa serikali na chama tawala kuzungumza lugha moja. Chama tawala kinawajibu wa kuisimamia serikali katika utekelezaji wa Ilani ya chama.
=30=

MASENZA AIHAKIKISHIA KAMATI YA BUNGE USALAMA IRINGA



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa- Iringa
Kamati ya Bunge ya utawala na serikali za mitaa imehakikishiwa kufanya kazi kwa amani na usalama mkoani Iringa kutokana na vyombo vya usalama kuwa macho muda wote.

Uhakika huo ulitolewa na mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama Mkoa wa Iringa, Amina Masenza alipokuwa akiongea na kamati ya Bunge ya utawala na serikali za mitaa katika ukumbi wa ofisi ya mkuu wa Mkoa, kamati hiyo ilipofanya ziara mkoani hapa.
 
Mkuu wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza (kusho), kulia ni Mwanne Mchemba, Makamu Mwenyekiti Kamati ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa
Masenza ambaye pia ni mkuu wa Mkoa wa Iringa alisema kuwa Mkoa wa Iringa upo shwari. Hali ya usalama ni nzuri kuiwezesha kamati hiyo kufanya ziara ya kikazi katika hali ya usalama na utulivu. Aidha, aliongeza kuwa wananchi mkoani Iringa wanajitambua katika kutekeleza majukumu yao. 

Wananchi mkoani Iringa hasa wakulima katika msimu huu wa kilimo wanajitambua na hawashurutishwi kutekeleza majukumu yao ya kilimo” alisema Masenza.

Wakati huohuo, makamu mwenyekiti wa kamati ya Bunge ya utawala na serikali za mitaa, Mwanne Mchemba alisema kuwa dhumuni la ziara ya kamati yake ni kukagua miradi ya maendeleo wilayani Kilolo kwa fedha zilizotolewa na serikali mwaka 2016/2017. 

Tunajua kuwa mkuu wa Mkoa ni jembe katika usimamizi wa uhamasishajai wa maendeleo. Hivyo, kamati inataka kujiridhisha na matumizi ya fedha za serikalai hasa thamani ya fedha kabla ya serikali kuidhinisha fedha nyingine kwa Wilaya ya Kilolo” alisema Mchemba.    
=30=

RC MASENZA ASHAURI MATUMIZI YA TEHAMA MAHAKAMA KUU IRINGA



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza ameishauri Mahakama kuu kanda ya Iringa kuongeza kasi ya matumizi ya Tehama katika utoaji wa haki kwa wananchi.

Kauli hiyo aliitoa katika salamu zake kwenye uzinduzi wa wiki ya sheria nchini uliofanyika katika uwanja wa Mahakama kuu Iringa jana.
 

Masenza alisema kuwa faida za Tehama katika Mahakama ni kurahisisha utoaji haki kwa wakati kwa wananchi. Aliongeza kuwa Tehama inasaidia kutunza kumbukumbu muhimu za mwenendo wa kesi na hatimae utolewaji wa haki. 

Tehama inaimarisha mawasiliano miongoni mwa wadau. Ni rahisi kuwapa taarifa wadau huko waliko wakahudhuria Mahakamani kwa wakati pale wanapohitajika bila taarifa kupotea. Tehama huimarisha maadili ya utoaji wa haki kwa wananchi, vifaa kama CCTV camera na vifaa vingine vya aina hiyo ni muhimu katika kuimarisha maadili ya haki” alisisitiza Masenza.

Katika hotuba ya Jaji mfawidhi wa Mahakama kuu kanda ya Iringa, mheshimiwa Mary Shangali alisema kuwa wiki ya sheria nchini imelenga Mahakama kujipambanua kwa wananchi na kueleza majukumu ya Mahakama na kutoa elimu kwa wananchi kuwa mahkama kuu ya Tanzania ipo kwa ajili ya wananchi na haki zao.

Mheshimiwa Shangali aliongeza kuwa wiki hiyo inalenga kupima utendaji kazi wa Mahakama. Alisema katika maadhimisho hayo, vituo vya kutolea elimu na kupokelea maoni ya wananchi vimeandaliwa katika shule ya sekondari ya wasichana Iringa, shule ya sekondari ya Miyomboni na chuo kikuu cha Iringa.
=30=