Serikalili Mkoani Iringa imesema
kuwa haitamvumilia mtu wala kikundi chochote kitakachojitokeza na kutaka
kuvuruga ama kuharibu zoezi la Sensa ya Watu na Makazi linalotarajia kuanza
nchini kote Agosti, 26, mwaka huu.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa
wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma katika moja ya mikutano yake ya hadhara
katika kuhamasisha wananchi kushiriki katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi
uliofanyika katika kijiji cha Ilambilole, katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa.
Dkt. Christine amesema kuwa kila
mwananchi anayo haki ya kuhesabiwa, tena kuhesabiwa mara moja. Amesema
“asitokee mtu wala kikundi cha watu kuwazuia kuhesabiwa wala kuwatoza hela kwa
ajili ya zoezi hili, akitokea mtu wa aina hiyo toeni taarifa kwa Serikali nasi
tutamshughulikia mara moja”. Amesema kuwa zoezi hilo lipo kisheria hivyo ni
wajibu wa kila mwananchi kushiriki kwa uhuru na pasipo hofu wala bugdha yoyote.
Akielezea umuhimu wa Sensa ya Watu
na Makazi ya mwaka 2012, Mkuu wa Mkoa wa Iringa amesema kuwa zoezi hilo lina
umuhimu wa kipekee kwa sababu takwimu zitakazokusanywa katika zoezi hilo
zitatumika katika kutathmini utekelezaji wa mipango mikubwa ya maendeleo
sambamba na utekelezaji wa malengo ya milenia 2015.
Akiongelea mabadiliko ya Sera mbalimbali
za nchi kwa lengo la kuboresha maisha ya wananchi, Mratibu Msaidizi wa Sensa
Mkoa wa Iringa, Conrad Millinga amesema kuwa takwimu hizo zitakazokusanywa
katika Sensa ndizo zitakuwa msingi wa kubadili Sera mbalimbali zilizopo ili
ziendane na hali halisi nchini. Amesema takwimu hizo pia zitasaidia katika
kuainisha maeneo ya kuboreshwa kwa kufanya tafiti mbalimbali za kina kwa lengo
la kupata suluhisho la matatizo yaliyopo.
Millinga amesema kuwa kuanzia
alhamisi tarehe 23 mwezi huu, makarani wa Sensa wataanza kupita katika maeneo
mbalimbali mkoani kukusanya taarifa za dodoso la jamii na kuomba wapewe
ushirikiano. Akifafanua kuhusu dodoso la jamii, amesema kuwa dodoso hilo
litajazwa ndani ya siku tatu kabla ya siku ya Sensa. Mratibu msaidizi wa Sensa
Mkoa amesema kuwa dodoso hilo litakusanya taarifa mahususi zinazohusu huduma za
jamii kama afya, zahanati, masoko, vituo vya afya, shule vyanzo vya maji,
miundombinu na huduma a kifedha.
Amesema katika dodoso hilo viongozi
wa jamii husika ndio watahusika katika kujibu maswali ya dodoso hilo kutokana
na uelewa wao mpana wa huduma zitolewazo katika eneo husika.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa yupo katika
ziara ya kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika Sensa ya Watu na
Makazi ya Mwaka 2012, kukagua shughuli mbalimbali
na kuhamasisha maedeleo na kuwahamasisha wananchi juu ya mchakato wa mabadiliko
ya katiba mpya katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Katika siku yake ya
kwanza amefanya mikutano minne ya hadhara katika vijiji vya Ilambilole,
Uhominyi, Nyang’oro na Ikengeza.
=30=