Wafanyakazi katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa wametakiwa kuzipenda kazi zao na kufanya kazi kwa bidii ili kuweza kufikia mafanikio ya kiuchumi.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma wakati akiongea na wafanyakazi wa ofisi yake kwa ajili ya kujitambulisha na kufahamiana na wafanyakazi wake.
Dkt. Ishengoma amesema “napenda kila mmoja apende kazi yake na asitamani kazi ya mwenzake na mambo yatajipa yenyewe hasa akiifanya kwa bidii”.
Aidha, amewataka wafanyakazi hao kuitumia fursa iliyopo Mkoani hapa ya wingi wa vyuo na vyuo vikuu kujiendeleza kitaaluma. Amesema “elimu haina mwisho na wafanyakazi wasisite kujiendeleza kielimu kwa sababu hakuna atakayekusukuma kujiendeleza”. Amesisitiza kuwa kila jambo jema chini ya jua linatokana na malengo madhubuti na kuwataka wafanyakazi hao kutokuridhika na kile walichonacho na kutamani kuendelea zaidi.
Aidha, amewataka wafanyakazi hao kuwa na wivu wa maendeleo. Amesema kinachomsaidia mwanadamu ni nia ya dhati ya kufanikiwa katika njia zilizo za halali.
Awali Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Bibi. Gertrude Mpaka alitoa pongezi kwa uteuzi wa Dkt. Ishengoma kuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa. Aidha, aliahidi kwa niaba ya wafanyakazi wote kutoa ushirikiano unaostahili kwa Mkuu huyo wa Mkoa ili kuufanya Mkoa wa Iringa uzidi kusonga mbele katika kuimarisha ustawi wa wananchi.
Ikumbukwe kuwa Dkt. Ishengoma aliteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa akitokea Mkoa wa Ruvuma alipokuwa pia Mkuu wa Mkoa.