Thursday, June 6, 2013

DKT. ISHENGOMA AKEMEA KILIMO KANDO YA RUAHA




Mkuu wa Mkoa wa Iringa Dkt. Christine Ishengoma amekemea tabia ya ulimaji kandokando ya mto Ruaha ili kukulinda na kuhifadhi mazingira na vyanzo vya maji.

Kauli hiyo ameitoka katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Naibu Meya wa Manispaa ya Iringa Hamza Ginga ambaye ni diwani wa Kata ya Kwakilosa katika kijiji cha Kiwere Wilayani Iringa.

Dkt. Christine amesema kuwa tatizo la ulimaji kandokando ya mto Ruaha na mito mingine ni chanzo cha uharibifu wa mazingira. Amesema kuwa maeneo ya kando kando ya mito katika wilaya zote mkoani Iringa yamevamiwa na watu ambao wamekuwa wakilima hadi kwenye kingo za mito.amesema kuwa pamoja na kuwepo kwa sheria zinazozuia ulimaji huo, bado utekelezaji wake ni hafifu. Aidha, katika kudhibiti uharibifu huo amezitaka Halmashauri kuchukua hatua za kisheria dhidi ya waharibifu hao. 

Mkuu wa Mkoa ameziagiza Halmashauri na vijiji kuhakikisha ulimaji kandokando ya mito na kwenye vyanzo vya maji unaachwa mara moja. Amesema kuwa watu wanaolima kandokando ya mito na kwenye vyanzo vya maji na maeneo mengine yaliyokatazwa kisheria wachukuliwe hatua za kisheria. Amesema kuwa tabia ya ulimaji wa vinyungu umechangia sana kupunguza maji katika mito kutokana na kupungua kwa akiba ya maji katika maeneo oevu. Amewataka wananchi kuzingatia sheria ya maji ambayo mtu haruhusiwi kulima karibu na kingo za mito katika umbali wa mita 100 kutoka kwenye kingo ya mto. 

Dkt. Christine amewaagiza wananchi kuhakikisha kuwa miti iliyopandwa inatunzwa na kuzuia moto kichaa kuchoma miti hiyo. Aidha, ameutaka uongozi wa wilaya kusimamia kwa umakini na kuwachukulia hatua kali wale wote watakaobainika kujihusisha na uchomaji moto miti. Amewataka wananchi kuwajibika kuzuia misitu isiungue moto na kuhakikisha kuwa hakuna moto kichaa mahali popote.

Akiongelea vyanzo vya maji, Mkuu wa Mkoa wa Iringa amesema “vyanzo vya maji ni urithi wa taifa kila mtanzania ana haki ya kufaidika na rasilimali hii. Hivyo kila mtanzania ana wajibika kutunza vyanzo vya maji”. Amewataka wale wote waliovamia vyanzo vya maji na kukata miti na kulima katika maeneo hayo  waondoke mara moja na Serikali za vijiji ziwachukulie hatua wavamizi hao. 

Siku ya mazingura duniani katika mkoa wa Iringa ilitanguliwa na shughuli mbalimbali zikiwemo kutoa mafunzo maalumu kuhusu vyanzo vya maji na elimu juu ya mpango wa usimamizi shirikishi wa misitu, kutoa elimu juu ya madhara ya uharibifu wa mazingira, kufanya kampeni za kuzuia ulimaji kandokando ya vyanzo vya majina kutengeneza barabara za moto kuzuia misitu ya asili na ya kupandwa kuungua.
=30=

UJANGILI KUWAMALIZA TEMBO NCHINI




Ujangili na uharibifu wa mazingira vinachangia sana kupunguza idadi ya tembo duniani na hasa Tanzania kutokana na tembo wengi kuuliwa na kusababisha kuathiri utalii na baadhi ya spishi za wanyamapori kuwa hatarini kupotea.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu katika mkutano wa wadau wa mtandao wa kuboresha ulinzi wa maeneo ya hifadhi kusini mwa Tanzania uliofanyika katika ukumbi wa Siasa ni Kilimo Wilaya ya Iringa.

Nyalandu amesema kuwa tafiti zinaonesha kuwa ujangili na uharibifu wa mazingira kwa pamoja vimechangia kupungua kwa idadi ya tembo dunia. Amesema kuwa kwa mujibu wa takwimu za mwaka 1930 kulikuwepo na tembo milioni 50 na sasa wamepungua na kubaki tembo 402,067 tu. Amesema kuwa ujangili huo unahatarisha kupotea kwa tembo na baadhi ya spishi za wanyamapori zinazotegemea wcolojia waliopo tembo. Amesema kuwa ugangili huo unaathiri utalii pia. 

Naibu waziri wa maliasili amesema kuwa hali hiyo inaashiria kutokuwepo kwa amani na usalama katika hifadhi na uchumi wa nchi. Amesema athari ya kiuchumi ni kubwa kwa sababu ujangili unaathiri uchumi kwa sababu idadi ya watalii wanaotembelea inapungua na hatimae kupunguza pato la taifa. Amesema kuwa ujangili unaathiri sana uchumi wan chi kwa sababu asilimia 17 ya pato la taifa linategemea utalii.

 Akiongelea mbinu za kukabiliana na mtandao wa ujangili unaotumia silaha za kisasa, amesema vi vema kuongeza uwezo wa kukabiliana na njama zinazotishia kupotea kwa tembo katika sura ya dunia. Aidha, ameutaka mkutano huo kujadili kwa kina kutoka na ufumbuzi wa changamoto zinazoikabili sekta ya ulinzi wa rasilimali za wanyamapori hasa tembo. 

Akielezea malengo ya mkutano huo, mratibu wa mradi wa kuboresha mtandao wa maeneo ya hifadhi kusini mwa Tanzania (SPANEST) ambao pia ni waandaaji wa mkutano huo, Godwell Ole Meing’ataki ameyataja malengo kuwa ni kutoa fursa kwa wadau na viongozi wa ngazi mbalimbali katika mikoa ya nyanda za juu kusini kubadilishana uzoefu, mbinu na mikakati ya kuboresha shughuli za uhifadhi katika mikoa ya nyanda za juu kusini. Lengo jingine amelitaja kuwa ni Kuweka mikakati ya kukabiliana na wimbi la ujangili wa tembo kwa kushirikisha wadau mbalimbali kwa kutambua kuwa hakuna mamlaka moja au mdau ambaye anaweza kukabiliana na janga hili bila ya ushirikiano wa wadau wengine pamoja na Kujadili kwa undani juu ya wimbi la ujangili wa tembo katika maeneo ya hifadhi na mapori ya wanyamapori katika maeneo ya nyanda za juu kusini na nchi kwa ujumla.

=30=