Hakika kila chenye
mwanzo hakikosi mwisho, na kila mwisho wa jambo moja huwa mwanzo wa jingine.
Ingawa huenda ni mapema sana kwangu kutoa tafakuri kamili ya muhula wangu katika
nafasi ya Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, hapana shaka kabisa kuwa nafasi
hiyo imenipa uzoefu maridhawa. Namshukuru Katibu Mkuu BAN Ki-moon kwa
kunipa fursa hii, kuniamini na kwa ushirikiano mkubwa wakati wote
wa utumishi wangu.
Kukitumikia chombo
hiki cha kimataifa kwa muda wa miaka mitano na nusu mfululizo ni heshima ya
pekee ambayo daima nitaienzi kama kilele kimojawapo
cha maisha yangu ya utumishi wa umma. Kila siku
niliyoitumia katika Umoja huo ilikuwa ni darasa la kusukuma mbele mipaka ya
ujuzi na elimu. Nimepata kufahamu mengi zaidi kuhusu Shirika
lenyewe; kuhusu dunia na watu wake, lakini pia kufahamu ukomo wa uwezo wa Umoja
wa Mataifa katika kushughulikia changamoto mbali mbali zinazoikabili dunia
yetu.
Dr. Asha-Rose Migiro
Utumishi wangu katika
Umoja wa mataifa ulikuwa fursa adhimu iliyonipa uzoefu wa pekee. Kazi hii
imeujaza moyo wangu na unyenyekevu wa dhati kwani niliingia Umoja wa Mataifa
wakati ambapo dunia inachagizwa na
madhila makubwa makubwa yakiwemo maradhi, umaskini wa
kupindukia, kutokuwapo kwa usawa wa kijinsia,
kuongezeka kwa vitendo vya ukatili na udhalilishaji kwa wanawake na
watoto; na changamoto nyingine nyingi. Kwa muktadha huu ilikuwa
fursa ya pekee kuchangia juhudi za pamoja za kuimarisha Umoja wa Mataifa katika
kutekeleza majukumu yake katika kipindi cha mazingira magumu ya
kimataifa yaliyojaa changamoto za kipekee kabisa.
Daima nitaendelea
kushukuru na kuthamini kwa dhati jinsi Mhe. Rais Jakaya Mrisho Kikwete, Serikali
na Watanzania wenzangu walivyonitia moyo na kunienzi katika kipindi chote
nilichokuwa Umoja wa Mataifa. Familia yangu, ndugu na marafiki walikuwa karibu
nami kwa dua na kunitia nguvu wakati wote wa utumishi wangu.
Nawashukuru sana.
Hapana shaka
kazi yangu katika Umoja wa Mataifa imeniwezesha kufahamiana
kwa karibu na viongozi wengi wa kimataifa na pia watu mbali
mbali waliopata mafanikio makubwa duniani. Nimeweza
kufahamu kwa undani thamani ya michango yao katika kujenga amani na ustawi wa
dunia.
Zaidi ya yote,
sitasahau hisia nilizopata kila nilipokutana na watu wanyonge waliokuwa
wanahitaji msaada wa Umoja wa Mataifa. Nitakumbuka daima tabasamu
ya mwanamke mmoja niliyekutana naye katika moja ya ziara zangu barani Afrika
nilipotembelea zahanati mojawapo kati ya kadhaa zinazofadhiliwa na Umoja wa
Mataifa. Mama huyo mwenye watoto sita, alikuwa amekikumbatia kitoto
chake kimoja kilichokuwa nyonde nyonde; lakini alikuwa na tabasamu iliyojaa
faraja na matumaini kwa kuwa alikuwa amefanikiwa kupata bure dawa za kunusuru
maisha ya mwanawe.
Maendeleo
Nafasi ya Naibu
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa iliasisiwa na Baraza Kuu la Umoja
wa Mataifa mwaka 1997 kwa madhumuni ya kuongeza ufanisi wa utendaji
wa Sekretariati na kuimarisha uongozi wa Umoja Mataifa katika
medani za uchumi na maendeleo ya jamii. Majukumu ya Naibu Katibu
Mkuu yaliongezeka kadri Shirika lilivyokuwa linapanua shughuli zake. Hatimaye
Naibu Katibu Mkuu akakabidhiwa jukumu la kuoanisha na kuratibu idara zote zilizo
chini ya mwavuli wa Umoja wa Mataifa. Jukumu hili lilikuwa na manufaa makubwa,
hususan tulipoingia katika utekelezaji wa dhana ya “Huduma ya Pamoja ”
(Delivering as One - DaO) ili kuleta ufanisi zaidi katika kazi zetu
hususan za maendeleo.
Kwa bahati nzuri,
ninamaliza kipindi changu kukiwa na maendeleo mazuri yanayotokana na jitihada za
kimataifa za kupambana na umaskini. Takwimu za kuaminika za hivi karibuni
zinatuambia kuwa juhudi zetu za kupunguza idadi ya watu maskini duniani kufikia
angalau nusu ya viwango vya sasa zimeanza kuzaa matunda. Taarifa hii ni ya kutia
moyo licha ya ukweli kwamba dunia inapitia dhahama kubwa ya kiuchumi kuliko
wakati mwingine wowote katika miaka ya hivi karibuni. Pamoja na majukumu
mengine,nguvu zetu tulizielekeza zaidi kwenye kufanikisha malengo ya maendeleo
ya milenia na malengo mengine ya maendeleo yaliyokubaliwa kimataifa.
Nilihamasika sana na dhamira waliyoionesha wadau na washirika wetu wa maendeleo:
serikali, mashirika ya kiraia na mashirika ya biashara. Kwani wote kwa pamoja
waliyatumia malengo hayo kama kilingo cha msingi katika kutokomeza
umaskini.
Katika kufanikisha
utekelezaji madhubuti wa malengo ya maendeleo ya milenia nilipewa jukumu la
kukamilisha ahadi ya Katibu Mkuu aliyoitoa kwa nchi wanachama ya kuunda Mfumo
Kamilifu wa Utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs Integrated
Implementation Framework ). Ninaona fahari kwamba naondoka Umoja wa Mataifa
mfumo huu ukiwa umekamilika ambapo Katibu Mkuu aliuzindua mwezi Juni mwaka huu.
Kwa mara ya kwanza mfumo huu umeweka utaratibu ambao utauwezesha Umoja wa
Mataifa na wadau wote kufuatilia mwenendo wa utekelezaji wa ahadi za kisera na
kifedha. Hapana shaka utaratibu huu utaongeza uwajibikaji wa wadau
na upimaji sahihi wa hatua za maendeleo.
Malengo
ya Maendeleo ya Milenia (MDGs) Barani Afrika
Kwa
mwelekeo huo huo, Katibu Mkuu alizindua Jopo la Viongozi la
Kuhimiza Utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Milenia Barani Afrika (MDG
Africa Steering Group) mwezi September 2007. Kikundi hiki kinajumuisha taasisi
zote kuu duniani zilizo mstari wa mbele katika kuchochea kasi ya maendeleo ya
Afrika. Nilipata bahati ya kukiongoza kikosi-kazi (MDG Africa
Working Group) kilichokuwa mhimili wa Jopo hilo la viongozi. Baada ya
miaka mitano ya majadiliano ya kina, Jopo hilo likiongozwa na Katibu Mkuu
limetoa mapendekezo kamambe ya utekelezaji. Endapo mapendekezo haya
yatazingatiwa basi yatakuwa nyenzo muhimu ya kuweka sera na
mikakati madhubuti itakayosaidia maendeleo katika nchi husika na duniani kwa
ujumla. Napenda kutoa mwito kwa wadau wote kuyapa umuhimu mapendekezo
haya.
Ninafahamu kwamba
tathmini kamili ya mafanikio ya utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo
ya Milenia imepangwa kufanyika Septemba mwaka 2013.
Hata hivyo tayari tunaweza kusema kuwa Malengo haya yameleta
mabadiliko chanya katika maisha ya watu wa kawaida sehemu nyingi
duniani, hususan barani Afrika. Ni dhahiri kuwa jamii nyingi
zimenufaika na utekelezaji wa malengo ya maendeleo ya milenia sio kwa kufanyiwa
hisani bali kwa wao wenyewe kuwa na mikakati maalum ya kupiga hatua madhubuti za
kujiletea maendeleo stahimilivu na yaliyolenga kuleta usawa baina ya
watu.
Mkutano
wa Rio + 20
Ni
jambo la kutia moyo kwamba maendeleo shirikishi na yenye kuleta usawa ni baadhi
ya masuala muhimu yaliyojadiliwa katika mkutano wa Rio +20 uliomalizika hivi
karibuni. Suala hili litachukua nafasi kubwa pia katika kuandaa mfumo wa
maendeleo unaotarajiwa baada ya mwaka 2015, mwaka
uliokusudiwa kufikia malengo ya maendeleo ya milenia.
Nilipokabidhiwa jukumu la kuratibu maandilizi ya ushiriki wetu kwenye
mkutano wa Rio+20 nilitiwa moyo na nia ya dhati ya mashirika ya Umoja wa Mataifa
ya kubuni mkakati wa pamoja wa kutekeleza maazimio ya Rio+20. Napenda
kuzishukuru nchi wanachama kwa kufikia makubaliano katika masuala mengi
yaliyojadiliwa Rio licha ya changamoto nyingi zinazotokana na mtikisiko wa
uchumi duniani. Ninafurahi kwamba maazimio ya mkutano huu yatachangia
upatikanaji wa maendeleo stahimilivu, shirikishi na yenye kuleta usawa na
hususan kuhakikisha kunakuwa na mustakabali mzuri kwa wanawake na
wasichana.
Uwezeshaji wa
wanawake na usawa wa kijinsia
Tukirejea kwenye
suala hili, hata baada ya Mkutano wa Rio + 20 tutawajibika kuendelea na juhudi
za uwezeshaji wa wanawake na kuleta usawa wa kijinsia. Wakati wa
utumishi wangu Umoja wa Mataifa tumefanya bidii kubwa na kutumia muda mwingi
kushughulikia suala hii. Tumetumia hadhi na ushawishi wa ofisi yetu kupaza sauti
za wanawake na wasichana na kukuza ushiriki wao katika jamii. Tumeendesha
kampeni za kupiga vita ukatili kwa wanawake na wasichana.
Tumezihimiza mamlaka katika ngazi za kitaifa na kimataifa kutunga sera na
sheria zinazozingatia haki za wanawake na usawa wa kijinsia, na tumetaka wapewe
fursa kushika nafasi za uongozi katika jamii. Ndiyo maana kwa
upande wetu hatukuweka koleo chini hadi pale tulipokamilisha uanzishwaji wa
idara inayojulikana kwa kifupi kama “UN Women” mnamo Julai 2010. Hii ni idara ya
Umoja wa Mataifa iliyoundwa kwa madhumuni ya kuongoza masuala ya
wanawake na usawa wa kijinsia kwa umakini na ufanisi zaidi kuliko hapo awali.
Tumefanya jitihada hizi kwa kuamini kuwa hakuna uamuzi wowote ule, uwe mdogo au
mkubwa, unaofanywa na Umoja wa Mataifa bila ya kuzingatia maendeleo na ustawi wa
wanawake na wasichana.
Huduma
ya Pamoja
Kwa
upande mwingine ninapenda kuwapongeza kwa dhati wenzangu wote waliomo katika
utumishi wa Umoja wa Mataifa,wake kwa waume,walioutumia ujuzi na weledi wao wote
kuchangia maendeleo ya nchi na jamii tunazozihudumia. Natoa shukrani za pekee
kwa wale wote waliopo kwenye ofisi na vituo vya Umoja wa Mataifa nje ya Makao
Makuu na ambao wanafanya kazi katika mazingira magumu na yenye changamo nyingi.
Hao wote wanadhihirisha umuhimu wa kuwapo kwa Shirika hili kama chombo cha
kuhimiza maendeleo katika ngazi zote za kitaifa, kikanda na
kimataifa. Katika kutekeleza dhana ya “Huduma ya Pamoja” (Delivering as One)
Waratibu Wakaazi wa Umoja wa Mataifa wamekuwa na mchango muhimu sana.Uratibu wao
umeongeza ubora na wepesi wa utoaji huduma kwa nchi wanamowakilisha Shirika.
Hatuna budi kuwashukuru kwa mchango wao mkubwa katika kufanikisha dhana ya
“Huduma ya Pamoja”. Ni dhahiri kwamba uwezo wa nchi
mwanachama kumiliki mchakato wa maendeleo yake unakuwa imara
zaidi pale ambapo kuna mtiririko mzuri wa huduma za Umoja wa
Mataifa na fursa za kukuza ushirikiano endelevu na wadau wengine wa
maendeleo. Wakati uamuzi rasmi kuhusu maendeleo ya dhana hii
ukisubiri kukamilika kwa majadiliano ya nchi wanachama, ninaamini kwa dhati kuwa
utaratibu wa kutoa “Huduma ya Pamoja” kupitia mpango mmoja
uliokubaliwa na wote ni mwelekeo sahihi na wenye
tija.
Nchini
mwetu Tanzania, mashirika ya Umoja wa Mataifa yamekuwa yakifanya kazi kwa
ushirikiano wa karibu sana toka mwaka 2011 kupitia mpango mmoja uitwao “Mpango
wa Umoja wa Mataifa wa Kusaidia Maendeleo” (United Nations Development Plan –
UNDAP). Mpango huu unakwenda sambamba na mwaka wa fedha wa Serikali yaani Julai
1 hadi Juni 30 na kwa mantiki hiyo kuuwezesha kuzingatia vipaumbele vya
Serikali. Kupitia mpango huu Umoja wa Mataifa umejiwekea utaratibu wa kujipima
na kujitathmini ambao unatoa fursa kwa hatua za haraka kuchukuliwa inapobidi.
Utaratibu huu unapatikana kwenye tovuti. Kwa upande wa uendeshaji, mfumo huu wa
utendaji kazi kwa pamoja umetuwezesha kutekeleza majukumu mengi kwa kutumia
raslimali chache ambapo“ziada” iliyopatikana imeelekezwa kwenye shughuli
nyingine za maendeleo.
Afya ya
Jamii
Katika eneo la afya, ambamo wanawake na watoto ndiyo
wanaathirika zaidi, hatua muhimu zinachukuliwa kupunguza
vifo nakuhakikisha kwamba kila mwanamke na kila mtoto
anakingwa na maradhi, hususan kuzuia maambukizi ya virusi vya UKIMWI kutoka kwa
mama kwenda kwa mtoto. Tukiwa Nairobi Aprili mwaka 2011, Katibu
Mkuu Ban Ki-moon, Michel Sidibe, Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Umoja wa
Mataifa linaloshughulikia UKIMWI (UNAIDS) pamoja nami tulishuhudia
mfano hai wa jitihada za Umoja wa Mataifa. Tulipata fursa ya kukutana na
mwanamke aliyeathirika na virusi ambaye alijaaliwa kupata mapacha watatu
waliozaliwa bila ya maambukizi. Nikiwa mjumbe wa Kamisheni ya Umoja
wa Mataifa iliyoshughulikia taarifa na uwajibikaji katika masuala ya afya ya
mama na mtoto (Commission on Information and Accountability on Women's and
Children's Health) ambayo iliendeshwa kwa umahiri na Rais Kikwete wa Tanzania na
Waziri Mkuu Harper wa Canada, nina imani kwamba jumuiya ya kimataifa
hivi sasa imepata mfumo madhubuti utakaohakikisha kwamba kunakuwa na
ufuatiliaji, usimamizi na uwajibikaji kuhusu afya ya mama na mtoto. Hakuna shaka
kwamba mfumo huu utafikia hatua ya utekelezwaji siku za hivi
karibuni.
Hali kadhalika, kazi
nzuri imekuwa ikifanywa na Mkurugenzi Mwendeshaji wa
Shirika la Mpango wa Uzazi Duniani (UNFPA), Babatunde Osotimehin, na
Margaret Chan, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) ya kuboresha
afya ya mama na mtoto. Matokeo ya jitihada za wenzangu hawa yalikuwa chachu ya utekelezaji wa majukumu ya Naibu Katibu
Mkuu katika nyanja zote za maendeleo. Ama kwa hakika matunda ya kazi zao
yanaimarisha imani yangu kuwa Umoja wa Mataifa ni Shirika lenye umuhimu mkubwa;
na kwamba mchango wetu, japo mdogo, unasaidia sana katika kufikia malengo ya
maendeleo ya milenia. Nilijawa na imani kama hiyo nikiwa katika ziara nyingine
za kikazi. Kwa mfano nikiwa Montevideo, Uruguay, Novemba 2011,
pamoja na wenzangu Michelle Bachelet, Helen Clark na Alicia
Barcena, tulisimama kidete kuunga mkono kampeni ya kitaifa ya
kupiga vita vitendo vya ukatili kwa wanawake.
Nilipozuru Haiti
mwezi Aprili2010, miezi michache baada ya tetemeko ambalo lilikuwa kubwa kuliko
yote yaliyowahi kutokea nchini humo kwa kipindi cha takriban karne moja,
nilikutana na watu ambao walikuwa wameathirika vibaya sana: waliopoteza familia
nzima, waliopata ulemavu wa maisha, waliopoteza mali zao zote! Lakini bado watu
hawa walikuwa na nyuso za matumaini wakitarajia mchango wa Umoja wa Mataifa na
wa wadau wengine wa jumuiya ya kimataifa. Mnamo Novemba 2010 tulizuru Laos,
ambako Umoja wa Mataifa unashirikiana kwa karibu na Serikali na wadau wengine
wengi katika utoaji wa misaada muhimu ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kuisaidia
Laos kupambana na janga la mabaki ya mabomu ya“cluster
munitions”.
Hii ni mifano
michache tu inayojibu hoja za wakosoaji wa Umoja wa Mataifa.Ujumbe wangu kwao ni
huu: wanyonge na wenye kutaabika sehemu zote duniani ni mashuhuda na watetezi
wakubwa wa Umoja wa Mataifa. Kwa wanyonge na wahitaji walio wengi
Shirika hili ni nguzo ya kutumainiwa katika jitihada zao za kila siku za
kujiletea maisha yenye utu na heshima.
Mageuzi
katika menejimenti na usimamizi wa mabadiliko
Ukweli
huu haumaanishi kuwa Umoja wa Mataifa hauna kasoro au upungufu. La hasha! Ndiyo
maana wakati wa utumishi wangu tulijielekeza kikamilifu kwenye kuboresha masuala
ya utawala, uendeshaji na namna tunavyofanya kazi. Ni wazi kwamba hivi sasa
Umoja wa Mataifa umebadilika kutoka chombo cha huduma za mikutano na kuwa
mtendaji mwenye majukumu muhimu nje ya kumbi za mikutano. Kwa ushirikiano na
msaada maridhawa wa wafanyakazi wenzangu, tulijikita katika kuhamasisha
mabadiliko ya kiutendaji katika Umoja wa Mataifa, ikiwa ni pamoja na kujenga
desturi ya uwajibikaji, uadilifu na kufanya kazi kwa tija zaidi huku tukitumia
rasilmali chache.
Ilitubidi pia kuweka
mifumo thabiti ya kusimamia mabadiliko yaliyokuwa yakijitokeza. Katika kufanya
hivyo tulitambua wazi kwamba hakukuwa na njia ya mkato wala njia mbadala ya
kuliimarisha Shirika letu na kulifanya liwe la kisasa zaidi katika kutekeleza
majukumu yake.Tulihakikisha kwamba utendaji kazi wetu unakwenda sambamba na
changamoto zilizopo, lakini pia tulizingatia ufinyu wa bajeti, misimamo tofauti
na wakati mwingine inayaokinzana ya nchi wanachama wa Umoja wa
Mataifa. Katika hali hii ilitulazimu kuwa wabunifu zaidi ili
kuleta muafaka baina ya nchi wanachama na kuhakikisha kwamba raslimali
chache zilizopo zinatoa tija kubwa zaidi.
Wafanyakazi ndiyo
rasilmali kubwa kupita zote. Hivyo kila tulipoendelea na jitihada za kuboresha
Shirika ilitubidi kuwekeza vilivyo kwa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa kwa
kuwapatia fursa za mafunzo na msingi imara wa maendeleo yao kazini. Ni jambo
lililo dhahiri kuwa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa wanatekeleza
majukumu yao katika mazingira hatarishi na yenye kubadilika mara kwa mara.
Tunafahamu, tena kwa uchungu mkubwa, kuwa Bendera ya Umoja wa Mataifa
- “bendera ya bluu” - hivi sasa si kinga
tena. Haituhakikishii usalama kwani wengi wa watumishi wetu mahiri
wamekuwa wahanga wa matukio ya kikatili ya ugaidi. Nilishuhudia tukio la aina
hii huko Abuja, Nigeria, ambako watumishi wenzetu walipoteza maisha kutokana na
shambulio la kigaidi la tarehe 26 Agosti 2011. Na mara nyingi wenzetu
wanapotangulia mbele ya haki, wapendwa wao wanaachwa katika hali ngumu ya
maisha. Ni faraja kubwa kwangu kuwa miongoni mwa masuala ambayo tuliyasimamia
kabla ya kumaliza utumishi wangu ni kuanzisha mchakato wa kubaini namna bora ya
kuwasaidia wahanga wa majanga hayo pamoja na familia
zao.
Utawala
wa sheria
Mojawapo ya majukumu
ya Umoja wa Mataifa ni kukuza sera zinazolenga kulinda haki za binadamu na
kuendeleza utawala wa sheria katika ngazi za kitaifa na kimataifa. Leo hii, nchi
nyingi zimelipa kipaumbele suala la kuimarisha utawala wa sheria,
hususan kufuatia umuhimu wake katika ajenda za ujenzi wa amani (peace-building)
na maendeleo stahimilivu. Kwa mantiki hiyo, nilifurahi nilipopata fursa ya
kusimamia ujenzi wa mfumo madhubuti wa sera na mwongozo wa utekelezaji wa
shughuli za utawala wa sheria nikishirikiana na nchi wanachama. Kwa upande wao
nchi wanachama zimepanga kufanya mkutano wa ngazi ya juu wakati wa kikao cha
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwezi Septemba 2012. Nia kubwa ni kuendeleza
jitihada katika suala hili ili kukuza heshima ya watu wote duniani na kujenga
amani kati ya mataifa.
Hitimisho
Japokuwa muda wangu
wa utumishi katika Umoja wa Mataifa umefikia tamati, naamini hakuna tamati
katika utekelezaji wa malengo, misingi na maadili ya Umoja wa Mataifa.
Ili mradi bado kuna umaskini duniani na mahitaji ya chakula; bado kuna
changamoto ya kutunza utu na heshima ya binadamu na haja ya kuimarisha amani
duniani basi hakika nitaendelea kuunga mkono jitihada, misingi na malengo ya
Umoja wa Mataifa popote pale nitakapokuwa. Kwani ni dhahiri kwamba njia bora ya
kukabiliana na changamoto kubwa zilizo mbele yetu ni kujenga ubia na ushirikiano
wa karibu baina ya serikali, asasi za kiraia, wafanyabiashara, mashirika ya
hisani, taasisi za kitaaluma na watu binafsi.
Aidha,
ninaaamini kuwa vijana, kizazi ambacho kina kila sababu ya kuwa na kiu ya kuishi
kwenye dunia yenye utu, usawa, haki na amani, watauchukulia Umoja wa Mataifa
kuwa mbia wa kuaminika katika kujenga mustakabali
wao.
Asha-Rose
Migiro