Wafanyakazi katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa wametakiwa kudumisha mawasiliano baina yao ili kuweza kuondoa migogoro inayoweza kujitokeza kutokana na uwepo wa nyufa za kimawasiliano.
Ushauri huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma wakati akiongea na wafanyakazi wa ofisi yake kwa lengo la kufahamiana na kuboresha utendaji wa kazi.
Dkt. Ishengoma amesema “mawasiliano baina yetu ni nyenzo muhimu sana na kama kutakuwa na ufa wa kimawasiliano hatuwezi kwenda mbali katika utendaji wetu”.
Mkuu huyo wa Mkoa ambaye pia ni mtaalamu wa tasnia ya mbinu za mawasiliano ameitaka timu ya wataalamu wa ofisi yake kuendeleza utamaduni uliojengeka wa kuandaa taarifa na kuziwasilisha taifani kwa wakati ili kuendelea kulijenga jina zuri la Mkoa wa Iringa.
Aidha, amesisitiza usimamizi madhubuti wa fedha za Serikali kuu na Halmashauri. Amesema katika kuzisimamia Halmashauri “si kwa kukaa ofisini tu bali kwa kuzitembelea Halmashauri na kuwafikia walio vijijini”.
Mkuu huyo wa Mkoa amewataka wafanyazi katika ofiisi yake kushirikiana katika kazi na kutokupigana vikumbo ili kufanikisha utendaji kazi.
Awali akimkaribisha Mkuu wa Mkoa kuongea na wafanyakazi, Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Bibi. Gertrude Mpaka amesema kuwa una jukumu la kuziwezesha na kuzijengea uwezo Serikali za Mitaa, kufikisha huduma bora za kiuchumi na kijamii na kuhakikisha amani, usalama na mshikamano unakuwepo.