Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Jamii imetakiwa kulipa uzito tatizo
la utapiamlo ili kupunguza udumavu, ulemavu na vifo vya watoto na wanawake
wanaonyonyesha.
Kauli hiyo imetolewa na mkuu wa mkoa
wa Iringa, Amina Masenza alipokuwa akifungua mkutano wa kamati za lishe za
halmashauri na mkoa wa Iringa kuhusu
masuala ya lishe ya mama na mtoto katika ukumbi wa Veta.
Masenza alisema “matatizo mbalimbali ya utapiamlo yanaendelea kudumaza, kulemaza na hata
kuua watoto wetu na wanawake hasa wale wajawazito na wanaonyonyesha. Pia jamii
kwa ujumla imekuwa ikiathirika kwa njia moja au nyingine kwa kuwepo kwa
utapiamlo”. Masenza aliongeza “pamoja
na maendeleo ambayo nchi yetu imeyapata katika maeneo mbalimbali, bado tatizo
la lishe duni linaendelea kuathiri uchumi na kuchangia kuwepo kwa umasikini.
Lishe duni pia huathiri ukuaji na maendeleo ya mtoto kimwili na kiakili hivyo
kufifisha mchango wake katika maendeleo ya jamii na taifa”.
Alisema kuwa uboreshaji wa hali ya
lishe nchini ni msingi wa afya njema, ubunifu, maendeleo mazuri ya kiuchumi na
kupunguza umasikini kwa mtu mmoja mmoja na nchi kwa ujumla. Aliongeza kuwa kwa
upande wa watoto lishe husaidia kuongeza uwezo wao kiakili na usanisi shuleni.
Mkurugenzi wa Mwanzo bora Dkt. Daniel
Nyagawa alilitaja lengo kuu la mradi huo kuwa ni kuisaidia serikali katika
kutekeleza mkakati wa taifa wa lishe pamoja na mkakati wa taifa wa kubadili
tabia na mienendo ya maisha.
Aliongeza kuwa mradi wa lishe wa
mwanzo bora unalenga kupunguza upungufu wa damu kwa wajawazito na wanawake
wanaonyonyesha kwa asilimia 20. Aidha, unalenga kupunguza udumavu kwa watoto
chini ya umri wa miaka miwili kwa asilimia 20. Mwisho mradi unalenga kujengea
uwezo wa utekelezaji kwa serikali mashirika yasiyo ya kiserikali na kijamii.
Dkt. Nyagawa alisema kuwa mradi
unatumia mkakati wa mawasiliano yanayolenga kubadili tabia katika masuala ya
lishe. Alisema kuwa mradi unalenga tabia ambazo zikifuatwa zitaleta matokeo
makubwa katika kupunguza udumavu na upungufu wa damu. Aliongeza mradi unalenga
kubadilisha tabia binafsi ambazo zamani miradi mingi haikufanya.
Akiongelea walengwa wa mradi huo,
Dkt. Nyagawa aliwataja “walio ndani ya siku 1,000 tangu kutungwa kwa mimba hadi
mtoto anapofikisha umri wa miaka miwili”.Alifafanua kuwa ni mama mjamzito,
anayenyonyesha na mama mwenye mtoto umri usiozidi miaka miwili. Baba ambaye
mwenza au mke wake ana sifa zilizotangulia na wale wote wanaolea watoto wenye
umri usiozidi miaka miwili.
Mradi wa lishe wa mwanzo bora ni
mradi wa lishe uliofadhiliwa na serikali ya marekani kupitia USAID ukitekelezwa
katika mikoa ya Iringa, Morogoro, Dodoma, Manyara na Mbeya.
=30=